(Kanuni
ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge,
2013)
UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika,
Mwaka huu Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania imefikisha umri wa nusu karne tangu ilipozaliwa tarehe 26 Aprili,
1964. Kama anavyosema Waziri Mkuu Mh. Mizengo Pinda katika hotuba yake ya tarehe
7 Mei, 2014 ‘Kuhusu Mapitio na Mwelekeo wa Kazi za Serikali na Makadirio ya
Matumizi ya Fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Bunge kwa Mwaka 2014/2015’:
“Miaka 50 kwa lugha yoyote ile siyo
kipindi kifupi.” Waziri Mkuu ametumia takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya
mwaka 2012 zinazoonyesha kwamba asilimia 90.6 ya Watanzania wote “wamezaliwa ndani ya Muungano na nchi
wanayoifahamu ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” Kwa maneno ya Waziri
Mkuu, “sote tunawajibika kuwatendea haki
watu hawa kwa kuulinda, kuuimarisha na kuudumisha Muungano wetu.”
Mheshimiwa Spika,
Kama ilivyo kwa Watanzania
wengine wengi, na mimi pia nimezaliwa ndani ya Muungano. Ninaamini kwamba
ukweli huu unawahusu pia waheshimiwa wabunge wengi waliomo ndani ya Bunge hili
tukufu. Na sisi pia tunaomba kutendewa haki kuhusu Muungano huu. Hata hivyo,
Mheshimiwa Spika, haki tunayoomba kutendewa ni moja tu: kuambiwa ukweli juu ya
Muungano huu na historia yake, hali yake ya sasa na mwelekeo wake wa baadaye.
Haki tunayoomba kutendewa ni kwa watawala kuacha propaganda na uongo juu ya
Muungano na kutuambia ukweli wote juu ya Muungano huu.
Bob Marley, aliyekuwa mwanamuziki
mpigania uhuru wa watu weusi maarufu kutoka Jamaica, aliwahi kusema katika
wimbo wake ‘Get Up, Stand UP, Stand Up For
Your Rights’ (‘Amkeni, Simameni,
Simameni kwa Haki Zenu’) kwamba: “You
can fool some people some time, but you cannot fool all the people all the
time”, yaani, unaweza kuwadanganya baadhi
ya watu kwa muda fulani, lakini huwezi kuwadanganya watu wote kwa muda wote!
Baada ya nusu karne ya uongo na propaganda kuhusu Muungano huu, Watanzania wa
kizazi hiki cha Muungano wanataka ukweli.
Na Watanzania hawa hawataulinda,
wala kuuimarisha au kuudumisha Muungano huu endapo wataendelea kudanganywa au
kufichwa ukweli juu ya mambo mengi yanayouhusu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Spika, sisi
kizazi cha Muungano tunahitaji kutendewa haki: acheni propaganda na uongo
kuhusu Muungano huu ndipo muweze kutuambia tuulinde, tuuimarishe na tuudumishe!
SHEREHE ZA MUUNGANO NA ‘WAASISI’
WA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Sherehe za Miaka 50 ya Muungano
ni mahali pazuri pa kuanzia kudai ukweli juu ya Muungano huu. Mtu yeyote
anayetembea sasa katika Barabara ya Nyerere kuanzia Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere hadi katikati ya jiji la Dar es Salaam; au Barabara
ya Ali Hassan Mwinyi kuanzia Morocco hadi katikati ya jiji, ataona kila
mlingoti wa taa za barabarani umepambwa kwa picha za Waasisi rasmi wa Muungano,
yaani Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume, wakiwa katika
matukio mbali mbali ya siku za mwanzo za Muungano. Picha hizo za Waasisi hao
pia zimepambwa karibu kila mahali katika barabara za katikati ya Eneo Kuu la
Kibiashara (CBD) la Jiji la Dar es Salaam.
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika, kwa
upande wa Zanzibar, barabara zote kuu za Mji wa Zanzibar, ikiwamo ile inayotoka
Mji Mkongwe kupitia Ikulu ya Zanzibar hadi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Abeid Amani Karume, hakuna picha hata moja ya Waasisi wa Muungano katika
matukio yanayoonyeshwa kwenye picha zilizoko Dar es Salaam. Badala yake,
barabara hizo zimepambwa kwa picha za Marais wa Zanzibar toka Mapinduzi ya
mwaka 1964 hadi wa sasa. Ni ndani ya eneo la wageni maarufu (VIP) pekee ndio
kuna picha moja ya Mwalimu Nyerere na Sheikh Karume. Hii ni katika wiki ambayo
Muungano huu umeadhimisha miaka hamsini tangu kuzaliwa kwake!
Kwa jinsi ambavyo tangu mwaka huu
uanze Watanzania tumepigwa propaganda za kila aina juu ya Muungano na TBC na
vyombo vingine vya habari vya serikali na vya binafsi, kukosekana kwa dalili
yoyote ya sherehe za Muungano kwa upande wa Zanzibar wakati wa kilele cha
sherehe hizo kunatilia shaka juu ya uimara wa misingi ya Muungano wenyewe. Hii
ndio kusema kwamba pengine kuna ukweli katika hitimisho la Tume ya Mabadiliko
ya Katiba kwamba Tanganyika ndiyo imevaa koti la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Na pengine ndio maana Muungano huu haujawahi kuungwa mkono Zanzibar kwa
kiasi ambacho wanaopenda kutuaminisha vinginevyo wamekuwa wakidai. Aidha,
pengine ndio maana hata picha za kuchanganya udongo zinazoonyeshwa na TBC kila
kukicha zinamwonyesha Mwalimu Nyerere akichanganya udongo peke yake, wakati
Sheikh Karume haonekani kabisa!
Mheshimiwa Spika,
Kuna jambo lingine
linalofikirisha sana kuhusu picha hizi za Sherehe za Miaka Hamsini ya Muungano
zilizopamba mitaa ya Dar es Salaam. Baadhi ya picha hizo zinawaonyesha watu
wengine ambao wamefutwa kabisa katika historia rasmi wanayofundishwa watoto
wetu mashuleni na vyuoni. Hivyo, kwa mfano, katika picha maarufu ya Mwalimu
Nyerere na Sheikh Karume wakisaini Hati za Makubaliano ya Muungano wapo pia,
kwa upande wa Tanganyika, Oscar Kambona, Bhoke Munanka na Job Lusinde, wakati
kwa upande wa Zanzibar wanaoonekana kwenye picha hiyo ni Abdallah Kassim Hanga,
Abdulaziz Twala na Ali Mwinyigogo. Aidha, kuna picha inayowaonyesha Mwalimu
Nyerere, Sheikh Karume na Kassim Hanga wakitabasamu kwa furaha kubwa.
Katika kitabu chake Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru! Zanzibar na
Mapinduzi ya Afrabia kilichochapishwa mwaka 2010, Harith Ghassany ameonyesha
jinsi ambavyo Oscar Kambona, Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na Saleh
Saadalla Akida walitoa mchango mkubwa katika kufanikisha Mapinduzi ya Zanzibar
ya Januari 12, 1964, na baadaye kufanikisha Muungano na Tanganyika wa Aprili 26
ya mwaka huo. Katika kitabu chake The
Partner-ship: Muungano wa Tanganyika na Zanzibar: Miaka 30 ya Dhoruba, Rais
wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Alhaj Aboud Jumbe ameeleza kwamba ni
Kambona, Bhoke Munanka na Job Lusinde ndio waliompelekea Sheikh Karume nakala
za Hati ya Makubaliano ya Muungano kabla ya Hati hizo kusainiwa tarehe 22
Aprili, 1964.
Mheshimiwa Spika,
Swali kuu ambalo sisi tuliozaliwa
ndani ya Muungano tunataka lijibiwe kwa ukweli kabisa ni ‘waasisi’ hawa wengine
wa Muungano, akina Abdallah Kassim Hanga, Abdulaziz Twala na Saleh Saadalla
Akida kwa upande wa Zanzibar; na Oscar Kambona, Bhoke Munanka na Job Lusinde
kwa upande wa Tanganyika walipotelea wapi na kwanini hawatajwi katika historia
rasmi ya Muungano na waasisi wake? Kassim Hanga alikuwa Waziri Mkuu na baadaye
Makamu wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar; wakati Twala alikuwa
Waziri wa Fedha wa Serikali hiyo na Saleh Saadalla alikuwa mjumbe wa Baraza la
Mapinduzi. Kwa upande wa Tanganyika, Oscar Kambona alikuwa Waziri wa Mambo ya
Nje na Ulinzi wakati wa Mapinduzi ya Zanzibar na baadaye wakati wa kuzaliwa kwa
Muungano; Bhoke Munanka alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais mwenye dhamana ya
masuala ya usalama, na Job Lusinde alikuwa Waziri wa Serikali za Mitaa.
Katika Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!, Ghassany ameonyesha jinsi ambavyo
akina Hanga, Twala na Saadalla pamoja na viongozi wengine waandamizi katika
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kama vile Othman Shariff, Mdungi Ussi na Jaha
Ubwa waliuawa na kuzikwa katika handaki moja katika sehemu inayoitwa Kama, nje
kidogo ya mji wa Zanzibar. Sisi wa kizazi cha Muungano tunataka kujua ukweli
juu ya makosa waliyoyafanya hawa waasisi wa Muungano hadi wakauawa na kuzikwa
katika kaburi au handaki moja. Tunataka kujua ukweli kama walifanya makosa
walishtakiwa katika mahakama gani iliyowahukumu adhabu ya kifo. Aidha, tunataka
kuambiwa ukweli kwanini mchango wao katika kuzaliwa kwa Muungano umefichwa kwa
muda wote wa nusu karne ya Muungano huu.
Kuhusu Oscar Kambona, inafahamika
kwamba katika miaka ya mwisho ya ukoloni na miaka ya mwanzo ya uhuru, ‘mwasisi’
huyu wa Muungano alikuwa mtu wa karibu sana wa Mwalimu Nyerere. Mwalimu Nyerere
ndiye alikuwa ‘Best Man’ wa Kambona
wakati wa harusi yake iliyofanyika London, Uingereza mwaka 1960. Inafahamika,
hata hivyo, kwamba mwaka 1967 Oscar Kambona alikosana na Mwalimu Nyerere na
akalazimika kukimbilia uhamishoni nchini Uingereza alikoishi hadi aliporudi
nyumbani wakati wa kurudishwa tena kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka
1992.
Tuliosoma miaka ya sabini na ya themanini
tulifundishwa mashuleni na kuimbishwa nyimbo zilizotuaminisha kwamba Oscar
Kambona alikuwa msaliti aliyetaka kuipindua Serikali yetu tukufu. Hata hivyo,
hatukuwahi kuambiwa kama alishtakiwa katika mahakama yoyote ya hapa nchini na,
kama ni hivyo, kama alipatikana na hatia yoyote na kuadhibiwa na mahakama. Tunachojua
ni kwamba aliporudi nyumbani mwaka 1992, Mzee Kambona hakukamatwa wala
kushtakiwa kwa kosa lolote lile. Sisi tuliozaliwa ndani ya Muungano huu tunataka
tutendewe haki kwa kuambiwa ukweli juu ya tuhuma za usaliti dhidi ya Mzee Oscar
Kambona ambaye sasa anaandikiwa vitabu kuwa ni mmoja wa watu waliotoa mchango mkubwa
katika kuzaliwa kwa Muungano huu.
KUTOLEWA KWA NYARAKA ZA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Katika maoni yake wakati wa Bunge
la Bajeti la mwaka wa fedha 2012/2013, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilipendekeza
kwamba Serikali iweke wazi “nyaraka mbali
mbali zinazohusu historia ya Muungano wetu na ‘mapito’ yake ili Watanzania
waelewe masuala yote yaliyotokea yanayouhusu. Hii ni muhimu zaidi kwa
kuzingatia ukweli kwamba mataifa ya magharibi kama vile Marekani na Uingereza
yalikwishatoa hadharani nyaraka za mashirika yao ya kijasusi pamoja na balozi
zao za Tanzania zinazoonyesha jinsi ambavyo serikali za mataifa hayo zilihusika
katika kuzaliwa kwa Muungano.”
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
ilifafanua kwamba “kuanikwa kwa nyaraka
zilizoko katika mamlaka mbali mbali za Serikali kutasaidia kuthibitisha au
kukanusha taarifa ambazo chanzo chake ni nyaraka za kidiplomasia na kijasusi za
nchi hizo kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulitokana na njama za
kibeberu za kudhibiti ushawishi wa siasa za kimapinduzi za Chama cha Umma na
viongozi wake ndani ya Baraza la Mapinduzi Zanzibar la wakati huo. Aidha,
nyaraka hizo zitatoa mwanga juu ya kilichowasibu viongozi waandamizi wa chama
hicho ambao bila uwepo wao kutambuliwa rasmi, historia ya Mapinduzi ya Zanzibar
na ya Muungano inabaki pungufu.”
Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni ilisisitiza juu ya haja ya taifa letu kuambiwa ukweli juu ya Muungano
huu: “... Miaka karibu hamsini ya
Muungano ni umri wa kutosha kwa taifa la Tanzania kuambiwa ukweli wote juu ya
kuzaliwa kwake na mapito ambayo limepitia katika kipindi hicho.” Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni ilirudia wito wake huo wakati wa kuwasilisha maoni
yake juu ya Bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais mwaka jana.
Mheshimiwa Spika,
Mjadala juu ya nyaraka za
Muungano huu ulichukua picha mpya wakati wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba
walipohoji uwepo wa Hati ya Makubaliano ya Muungano na uhalali wa Muungano
wenyewe wakati wa mjadala juu ya Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu ya Katiba.
Baada ya wajumbe walio wachache wa Kamati Namba Nne kuonyesha ushahidi kwamba
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar haijawahi kuwa na nakala ya Hati hiyo, na
kwamba haijawahi kupelekwa na kusajiliwa katika Sekretarieti ya Umoja wa
Mataifa, Serikali hii ya CCM ililazimika kutoa kile ilichokiita nakala ya Hati
ya Makubaliano ya Muungano.
Hatuhitaji kuzungumzia tofauti
kubwa ya sahihi ya Sheikh Karume iliyoko kwenye Hati hiyo na sahihi ya Sheikh
Karume iliyoko katika Sheria mbali mbali alizosaini kama Rais wa Zanzibar na
wakati mwingine kama kaimu Rais wa Jamhuri ya Muungano. Cha muhimu ni kwamba
mgogoro juu ya Hati ya Makubaliano ya Muungano unathibitisha ukweli kwamba
matokeo ya utamaduni huu wa kufichaficha nyaraka muhimu za nchi ni kwa wananchi
kukosa imani na serikali iliyoko madarakani, kwa kuwa wananchi wanajenga hisia
kwamba nyaraka hizo zinafichwa kwa sababu zina ushahidi wa maovu yaliyofanywa
na serikali hiyo.
Kwa sababu hizi zote, kwa mara
nyingine tena, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM
kutoa nyaraka za Muungano huu hadharani ili Watanzania waweze kuelewa historia
halisi ya Muungano badala kuendelea kulishwa propaganda na TBC na kwenye
majukwaa ya kisiasa ya CCM na Serikali yake! Vinginevyo, chochote
kitakachosemwa na TBC na watawala katika majukwa yao ya kisiasa kuhusu Muungano
huu hakitaaminika tena na wananchi wa Tanzania.
KIELELEZO CHA UMOJA NA MSHIKAMANO
AU UNYONYAJI WA KIKOLONI?
Mheshimiwa Spika,
Katika hotuba ya Waziri Mkuu
Bunge lako tukufu limeambiwa kwamba “Muungano
huu ni wa kipekee na wa kupigiwa mfano duniani kote. Aidha, ni kielelezo kamili
cha umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi....” Ni kweli kwamba
Muungano huu ni wa kipekee kwa sababu haujawahi kuigwa na nchi nyingine zozote
katika Afrika. Na kama Muungano huu ungekuwa wa ‘kupigiwa mfano duniani kote’,
kama inavyodaiwa na Waziri Mkuu, basi kungekuwa na angalau nchi moja iliyoomba
kujiunga katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Angalau kungekuwa na nchi
zilizoiga mfano wa Muungano huu kwingineko Afrika na duniani kote.
Kwa kuwa hakuna nchi hata moja
iliyowahi kuomba kujiunga nasi, na kwa kuwa hakuna nchi nyingine zilizoiga mfano
wa Muungano huu, pengine huu ni muda muafaka wa kuhoji ukweli wa kauli kwamba
Muungano huu ‘ni kielelezo cha umoja,
mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi’ wa Tanganyika na Zanzibar. Mzee
Pius Msekwa, Mwenyekiti Mstaafu wa CCM na Spika Emeritus wa Bunge hili tukufu, aliwahi kusema katika mada yake Hali ya Muungano kwa semina iliyofanyika
Tanga miaka 20 iliyopita kwamba, muundo wa sasa wa Muungano huu umepelekea
wengi kuamini kwamba Muungano huu ni kiini macho tu.
Hii ni kwa sababu, chini ya
Muungano huu, Zanzibar ilikabidhi sehemu muhimu ya mamlaka yake (mahusiano ya
nchi za nje, ulinzi na usalama, uraia, kodi na ushuru, sarafu, nguvu kuu za
kuendeshea uchumi na mengineyo) kwa Tanganyika; na kisha Tanganyika ikajigeuza
jina na kujiita Jamhuri ya Muungano. Spika
Emeritus Msekwa aliongeza kwamba kwa jinsi mambo yalivyo sasa, Zanzibar
inaonekana kama vile ni ‘invited guest’
(mgeni mwalikwa) katika Muungano huu.
Naye msomi mashuhuri wa Kiafrika,
Profesa Ali A. Mazrui katika makala yake ‘Imperialism
after the Empire: Lessons from Uganda and Tanzania’, yaani ‘Ubeberu Baada ya Himaya: Funzo Kutoka Uganda
na Tanzania’, iliyochapishwa katika gazeti la Kenya, The Sunday Nation, la Mei 22, 1994, alisema kwa sababu ya Muungano,
Zanzibar imepoteza kila kitu chake muhimu, wakati Tanganyika imebadilika jina
tu na kuwa Tanzania, huku ikiwa na mamlaka zaidi lakini ikibaki na Rais wake,
nembo yake ya Taifa, wimbo wake wa Taifa na hata kiti chake katika Umoja wa
Mataifa. Kama tunavyoonyesha katika Maoni haya, gharama ya kuyapuuza maneno
haya ya watu hawa wazito imekuwa kubwa kweli kweli, hasa kwa Zanzibar.
MISAADA NA MIKOPO YA KIBAJETI
Mheshimiwa Spika,
Ushahidi wa nyaraka ambazo
zimewasilishwa kwenye Bunge lako tukufu na Serikali hii ya CCM unaonyesha
kwamba Muungano huu ni kielelezo cha unyonyaji na ukandamizaji mkubwa ambao nchi
ndogo ya Zanzibar imefanyiwa na nchi kubwa ya Tanganyika. Ni mfano wa jinsi
ambavyo nchi moja kubwa ya Kiafrika inaweza kuigeuza nchi nyingine ndogo ya
Kiafrika kuwa koloni lake. Kwa sababu maneno haya yanaweza kupotoshwa na wale
ambao wamefaidika na uhusiano huu wa kikoloni kati ya Tanganyika na Zanzibar
naomba kutoa ufafanuzi kama ifuatavyo.
Kwa miaka mingi Zanzibar
imelalamika kwamba inapunjwa katika mgawanyo wa mapato yanayotokana na fedha
zinazotolewa na nchi wafadhili na taasisi za kimataifa kwa Jamhuri ya Muungano.
Kwa sababu ya malalamiko hayo, mwaka jana Kamati ya Kudumu ya Bunge lako tukufu
ya Katiba, Sheria na Utawala iliiagiza Ofisi ya Makamu wa Rais kwamba: “Utaratibu wa mgawanyo wa mapato yanayotokana
na fedha zinazotoka kwa wafadhili ni vyema ukaangaliwa upya kwa Serikali zote
mbili yaani SMZ na SMT.” Aidha, Kamati ilishauri kwamba “Serikali itolee uamuzi mapendekezo ya Tume
ya Pamoja ya Fedha yaliyowasilishwa Serikalini tangu mwaka 2006 na kuwasilishwa
tena mwaka 2010 kuhusu utaratibu wa mgao wa fedha za Serikali zote mbili.”
Serikali hii ya CCM imejibu
maagizo haya ya Kamati kama ifuatavyo: “Serikali
zetu mbili bado zinaendelea kushughulikia mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya
Pamoja ya Fedha. Aidha, kuhusu mgawanyo wa fedha zinazotoka kwa wafadhili, upo
utaratibu wa mgawanyo wake ambapo, kwa upande wa misaada na mikopo ya kibajeti
isiyokuwa na masharti maalum, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ... hupata
gawio la asilimia 4.5.”
Mheshimiwa Spika,
Kauli hii ya Serikali ni ya
uongo. Katika maelezo yake mbele ya Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala, Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano, aliitaarifu Kamati kwamba “Kwa mwaka wa fedha 2013/14, hadi kufikia
mwezi Machi, 2014 SMZ imepata Gawio la Misaada ya Kibajeti (General Budget
Support – GBS) shilingi 27,190,502,190.97/= kati ya shilingi 32,627,535,000/= zilizoidhinishwa
na Bunge.” Hii ndio kusema kwamba kati ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge
lako tukufu kama gawio la misaada na mikopo ya kibajeti kwa Zanzibar, ni
asilimia 83 ndizo zilizolipwa hadi kufikia robo ya tatu ya mwaka huu wa fedha.
Hata hivyo, Mheshimiwa Spika,
hili sio tatizo, kwani kwa mwelekeo wa takwimu hizi, hadi kufikia mwisho wa
mwaka huu wa fedha, gawio lililoidhinishwa na Bunge lako tukufu linaweza kuwa
limelipwa lote. Tatizo kubwa na la msingi ni kwamba gawio lililoidhinishwa na
Bunge hili tukufu sio gawio halali kwa Zanzibar. Hii kwa sababu, kwa mujibu wa Maelezo ya Waziri wa Fedha Mheshimiwa Saada
Mkuya Salum (MB.) Akiwasilisha Mapendekezo ya Mfumo wa Mapato na Matumizi ya
Serikali kwa Mwaka 2014/15 kwa Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, ya tarehe 30 Aprili, 2014, mapato halisi ya Serikali ya Jamhuri
ya Muungano yanayotokana na misaada na mikopo nafuu ya nje ilikuwa shilingi
bilioni 1,163 au trilioni 1.163.
Kama Zanzibar ingepatiwa asilimia
4.5 ya mapato hayo, kama inavyotakiwa kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa na
Serikali hii ya CCM, basi kwa mwaka jana peke yake, gawio halali la Zanzibar la
misaada na mikopo ya kibajeti lingekuwa shilingi bilioni 52.335. Badala ya
kupatiwa shilingi bilioni 52.335 ambazo ni fedha zake halali, Zanzibar
iliidhinishiwa shilingi bilioni 32.627 au asilimia 52 ya fedha zake halali. Fedha
hizo ni sawa na asilimia 2.8 ya fedha zote za misaada na mikopo ya kibajeti kwa
Jamhuri ya Muungano. Fedha zilizobaki, yaani shilingi trilioni 1.130 au
asilimia 97.2 ya fedha zote za misaada ya kibajeti zimetumika na zitatumika Tanganyika.
Kwa ushahidi huu wa nyaraka za Serikali hii ya CCM, kwa sababu ya Muungano huu,
kwa mwaka jana peke yake Zanzibar iliibiwa shilingi bilioni 25.145 au asilimia
48 ya fedha zake halali za gawio la misaada na mikopo ya kibajeti.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mapendekezo yaliyoletwa
kwenye Bunge lako tukufu na Serikali hii ya CCM, Zanzibar itaibiwa fedha nyingi
zaidi kwa mwaka huu wa fedha 2014/15. Hii ni kwa sababu, kwa mujibu wa maelezo
ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano, kwa mwaka huu wa fedha, “fedha zitakazokwenda SMZ zinajumuisha
shilingi 21,639,608,000.00 mgao wa misaada ya kibajeti....” Kwa upande
mwingine, kwa mujibu wa Maelezo ya Waziri
wa Fedha, ‘misaada na mikopo ya kibajeti’ kwa mwaka huu wa fedha itakuwa
shilingi bilioni 992.170. Hii ina maana kwamba kwa mwaka huu wa fedha, Zanzibar
itapata asilimia 2.18 tu ya fedha za misaada na mikopo ya kibajeti. Hii
inaonyesha pia kwamba, kwa mwaka huu, fedha za misaada na mikopo ya kibajeti
ambazo zitabaki na kutumika Tanganyika ni shilingi bilioni 970.531 au asilimia
97.82 ya fedha hizo.
Kama Serikali hii ya CCM
ingeheshimu utaratibu wake wa asilimia 4.5 ya fedha hizo kwa Zanzibar, gawio
halali la Zanzibar kutokana na fedha za misaada na mikopo ya kibajeti kwa mwaka
ujao wa fedha lingekuwa shilingi bilioni 44.647! Kwa maana hiyo, Serikali hii
ya CCM inapendekeza kuilipa Zanzibar asilimia 48.47 ya fedha zake halali.
Endapo Bunge lako tukufu litapitisha mapendekezo haya kama inavyoombwa na
Serikali hii ya CCM, Zanzibar itaibiwa shilingi bilioni 23 au asilimia 51.53 ya
fedha zake halali kwa mwaka ujao wa fedha.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inaitaka Serikali hii ya CCM ilieleze Bunge lako tukufu na iwaeleze Watanzania,
na hasa Wazanzibari, kwa nini fedha halali za Zanzibar kutokana na misaada na
mikopo ya kibajeti inayokuja kwa jina la Jamhuri ya Muungano hazijalipwa kwa
mwaka jana wa fedha. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali
hii ya CCM ilieleze Bunge lako tukufu na iwaeleze Watanzania, na hasa
Wazanzibari, kwa nini inapendekeza kuipatia Zanzibar pungufu ya fedha zake
halali kama gawio la misaada na mikopo ya kibajeti kwa mwaka huu wa fedha.
Vile vile, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inaitaka Serikali hii ya CCM ilete mbele ya Bunge lako tukufu
takwimu za fedha zote zilizopokelewa na Serikali kama misaada na mikopo ya
kibajeti kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita na sehemu ya fedha hizo
zilizolipwa kwa Zanzibar kama gawio lake katika kipindi hicho. Takwimu hizo ni
muhimu ili Watanzania, na hasa Wazanzibari, waweze kufahamu kama Zanzibar
imekuwa ikipata sehemu yake halali ya mapato ya Jamhuri ya Muungano yanayotokana
na misaada na mikopo ya kibajeti. Mwisho, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inalitaka Bunge lako tukufu kuunda Kamati Teule ya Bunge hili itakayochunguza
mgawanyo wa mapato yanayotokana na misaada na mikopo ya kibajeti kati ya
Tanganyika na Zanzibar ili kupata ukweli juu ya uhalali wa malipo ya mapato
hayo kwa Zanzibar.
MISAADA NA MIKOPO ISIYOKUWA YA
KIBAJETI
Mheshimiwa Spika,
Misaada na mikopo ya kibajeti sio
eneo pekee ambapo Zanzibar inanyonywa na Tanganyika kwa sababu ya Muungano huu.
Ukweli ni kwamba hali ni mbaya zaidi kuhusiana na fedha za misaada na mikopo
isiyokuwa ya kibajeti. Hapa pia takwimu za Serikali hii ya CCM zinatisha na
kusikitisha. Hivyo, kwa mfano, kwa mujibu wa Maelezo ya Waziri wa Fedha, kwa mwaka wa fedha 2013/14 fedha za nje
kwa ajili ya miradi ya maendeleo zikijumuisha misaada na mikopo ya Basket Fund
na misaada na mikopo ya miradi zilikuwa shilingi trilioni 2.692 au bilioni
2,692. Fedha hizi zote zilitumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya
Tanganyika. Hapa Zanzibar haikupata kitu chochote!
Maelezo
ya Waziri wa Fedha yanaonyesha
kwamba kwa mwaka wa fedha 2014/15, misaada na mikopo isiyokuwa ya kibajeti
kutoka nje inatazamiwa kuwa shilingi bilioni 2,019.43 au trilioni 2.019. Hizi
zote ni fedha zitakazotumika kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya Tanganyika. Hapa
pia Zanzibar haitapata kitu chochote. Ni muhimu kwa Bunge lako tukufu kukumbuka
kwamba, kwa sababu ya Muungano huu, Zanzibar imenyang’anywa mamlaka ya kuomba mikopo
au misaada kutoka nje bila kwanza kupata kibali cha Wizara ya Fedha ya Jamhuri
ya Muungano, aka Wizara ya Fedha ya
Tanganyika. Sisi tuliozaliwa ndani ya Muungano tunataka kujua unyonyaji na wizi
huu wa fedha za Wazanzibari utakomeshwa lini. Aidha, sisi tulio kizazi cha
Muungano huu tunataka kuambiwa kama mgawanyo wa aina hii wa mapato yanayokuja
kwa jina la Jamhuri ya Muungano ndio kielelezo
cha umoja, mshikamano na upendo miongoni mwa wananchi wa Tanganyika na
Zanzibar ulioletwa na Muungano huu.
Mheshimiwa Spika,
Sio tu kwamba Zanzibar haipati
stahili yake ya mapato yanayopatikana kwa jina la Jamhuri ya Muungano kutoka
vyanzo vya nje, bali pia fedha zinazopatikana kutokana na mambo ya Muungano
zinatumika kwa mambo yasiyo ya Muungano ya Tanganyika. Moja ya matokeo ya
mjadala wa katiba wa mwaka 1983/84 uliopelekea ‘kuchafuka kwa hali ya hewa ya
kisiasa Zanzibar’ na kung’olewa madarakani kwa Alhaj Aboud Jumbe ni kuingizwa
kwa Sura ya Saba inayohusu ‘Masharti Kuhusu Fedha za Jamhuri ya Muungano’
katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, 1977.
Kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Tano ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1984, ibara mpya ya 133 ya Katiba
iliweka masharti kwamba “Serikali ya
Jamhuri ya Muungano itatunza ‘Akaunti ya Pamoja ya Fedha ... ambamo kutawekwa
fedha yote itakayochangwa na Serikali mbili kwa kiasi kitakachoamuliwa na Tume
ya Pamoja ya Fedha ... kwa madhumuni ya shughuli za Jamhuri ya Muungano kwa
Mambo ya Muungano.”
Aidha, ibara ya 134 iliweka
masharti ya kuwa na Tume ya Pamoja ya Fedha yenye majukumu ya “kuchambua mapato na matumizi yanayotokana
na, au yanayohusu utekelezaji wa Mambo ya Muungano na kutoa mapendekezo kwa
Serikali mbili kuhusu mchango na mgawo wa kila mojawapo ya Serikali hizo.”
Majukumu mengine ya Tume hiyo ni “kuchunguza
... mfumo wa shughuli za fedha kwa Jamhuri ya Muungano na pia uhusiano katika
mambo ya kifedha kati ya Serikali mbili.”
Mheshimiwa Spika,
Kwa miaka thelathini tangu
kupitishwa kwa Mabadiliko ya Tano ya Katiba, masuala ya Tume ya Pamoja ya Fedha
na Akaunti ya Pamoja ya Fedha yamekuwa mojawapo ya kile kinachoitwa ‘Kero za
Muungano’ ambayo ufumbuzi wake umeshindikana. Kwa mfano, licha ya Katiba
kuelekeza kuundwa kwa Tume ya Pamoja ya Fedha, sheria ya kuunda Tume hiyo,
yaani Sheria ya Tume ya Pamoja ya Fedha,
ilipitishwa miaka kumi na mbili baadaye, yaani mwaka 1996.
Baada ya hapo Tume
yenyewe iliundwa rasmi mwaka 2003, yaani miaka saba baada ya kutungwa kwa
sheria na miaka 19 tokea Katiba iweke masharti ya kuundwa kwa Tume hiyo. Kwa
upande wa Akaunti ya Pamoja ya Fedha, leo ni mwaka wa thelathini tangu Katiba
kuelekeza Akaunti hiyo kufunguliwa na bado haijafunguliwa. Kutokana na kushindikana
kufunguliwa huko, kwa miaka yote hii, bajeti ya Muungano imekuwa ndio bajeti ya
Tanganyika, kinyume na maelekezo ya Katiba.
Mwaka 2006 Tume ya
Pamoja ya Fedha iliajiri wataalamu waelekezi kutoka kampuni kimataifa ya
uhasibu ya PriceWaterhouseCoopers kuangalia suala la gharama na mgawanyo wa
fedha za Muungano. Wataalamu hao walifanya uchambuzi halisi wa mambo yapi ni ya
Muungano na yapi ni ya Tanganyika na yapi ni ya Zanzibar na gharama za
uendeshaji wa kila moja. Baada ya orodha kupatikana, watafiti hao walitafuta
matumizi halisi ya bajeti ya vifungu hivyo kwa muda wa kiasi cha miaka 10
iliyopita.
Watafiti wa PriceWaterhouseCoopers
walikwenda mbali zaidi ya hapo na kukusanya mapato yote kwa kila kifungu cha
mambo ya Muungano halisi. Mwishowe, wakalinganisha iwapo mapato hayo yanakidhi
matumizi ya Muungano au yana upungufu. Taarifa ya uchambuzi wa
PriceWaterhouseCoopers ilitolewa kama Mapendekezo
ya Tume Kuhusu Vigezo vya Kugawana Mapato na Kuchangia Gharama za Muungano
ya mwezi Agosti 2006.
Taarifa ya Tume ya
Pamoja ya Fedha inaonyesha hali ya kusikitisha kuhusu mapato na matumizi ya
fedha za Muungano, hasa kwa upande wa Tanganyika. Ili kupata picha kamili ya
hali halisi ilivyo, tunaomba kunukuu sehemu ya Taarifa hiyo in extenso, kwenye ukurasa wake wa
18: “Uchambuzi unaonyesha kuwa
mapato yanayotokana na vyanzo vya Muungano yanakidhi matumizi ya Muungano na
kuwa na ziada ya kutosha. Takwimu zinaonyesha kuwa kiasi kidogo cha mapato hayo
kimekuwa kinagharimia matumizi ya Muungano. Kwa mfano, uwiano huu ulikuwa ni (shilingi
bilioni 360.679 kati ya (shilingi bilioni 1,030.513) sawa na asilimia 35 mwaka
1999/2000, (shilingi bilioni 468.450) kati ya (shilingi bilioni 1,801.733) sawa
na asilimia 26 mwaka 2002/03, na (shilingi bilioni 636.078) kati ya (shilingi
bilioni 2,271.710) sawa na asilimia 28 mwaka 2003/04.
“Uchambuzi unaonyesha kuwa kiasi kikubwa
cha ziada ya mapato ya Muungano kimekuwa kinatumika kugharimia mambo yasiyo ya
Muungano. Viwango hivi kwa mwaka 1999/2000 vilikuwa ni (shilingi bilioni 39.822)
sawa na asilimia 5.9 kwa (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) na (bilioni 631.714)
sawa na asilimia 94.1 kwa Tanzania Bara. Viwango hivi vilibadilika kwa kiasi
kikubwa kwa mwaka wa fedha 2003/04 ambapo kwa (Serikali ya Mapinduzi Zanzibar)
kilishuka hadi (shilingi bilioni 37.053) sawa na asilimia 2.3, na (shilingi
bilioni 1,588.494) sawa na asilimia 97.7 kwa (Serikali ya Muungano wa Tanzania).”
Takwimu za utafiti wa
PriceWaterhouseCoopers zinaonyesha kwamba kwa mwaka wa fedha 2003/2004 pekee,
matumizi halisi kwa vifungu vya Muungano yalikuwa shilingi bilioni 537.258
ambayo ni asilimia 20 tu ya bajeti yote ya Serikali ya Muungano kwa mwaka huo.
Mapato halisi ya vyanzo vya mapato vinavyotokana na mambo ya Muungano kwa mwaka
huo yalikuwa ni shilingi bilioni 1,030.826, au takriban shilingi trilioni 1.030.
Kwa maana nyingine, mapato na matumizi ya fedha zinazotokana na vyanzo vya
mambo ya Muungano yaliacha ziada ya shilingi bilioni 493.567 kwa mwaka huo
mmoja. Ziada hii ni nje ya mapato yaliyotokana na misaada na mikopo kutoka nje,
na ilitumika kwa shughuli za maendeleo za Tanganyika zisizo za Muungano.
Kwa sababu Tanganyika imekuwa
inafaidika sana na utaratibu huu, Serikali ya Jamhuri ya Muungano - ambayo
kiuhalisia ni Serikali ya Tanganyika iliyovaa joho la Muungano – imekataa
kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha kwamba uwekwe utaratibu
utakaowezesha kutenganisha mapato na matumizi ya Muungano na yasiyo ya
Muungano. Miaka nane tangu mapendekezo hayo yatolewe mwaka 2006, “Serikali zetu mbili”, kwa maneno ya Mh.
Samia Suluhu Hassan, “bado zinaendelea
kushughulikia mapendekezo yaliyotolewa na Tume ya Pamoja ya Fedha.”
Mheshimiwa Spika,
Kero nyingine kubwa ya Muungano
huu na ambayo ina umri karibu sawa na Muungano wenyewe inahusu hisa za Zanzibar
zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki kabla ya Bodi hiyo
kuvunjwa mwaka 1965 na Benki Kuu ya Tanzania kuanzishwa. Kwa mujibu wa maelezo
ya Waziri Suluhu Hassan, hisa za Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya Afrika
Mashariki ni mojawapo ya “kero zilizobaki
katika orodha ya mambo ya kutafutiwa ufumbuzi....” Kufuatana na maelezo
hayo, “masuala ya Bodi ya Sarafu ya
Afrika Mashariki na mgawanyo wa faida ya Benki Kuu yapo katika ngazi ya
Mawaziri wa Fedha wa (Serikali ya Jamhuri ya Muungano) na (Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar) kwa hatua za majadiliano.”
Alipohojiwa juu ya hisa za
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki mwezi
Januari 2013, Waziri huyo huyo aliiambia Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala
kwamba: “Katika Kikao cha Kamati ya
Pamoja ya SMT na SMZ ya Kushughulikia Masuala ya Muungano kilichofanyika tarehe
14 Januari 2013 imeelezwa kwamba Mawaziri wa Fedha wa SMT na SMZ wamepatiwa
nyaraka maalum zenye taarifa za siri na wamekubaliana kujadili suala hili mwezi
Februari, 2013 baada ya kuzipitia nyaraka hizo.” Kwa vile bado mawaziri
wanajadiliana, kama tulivyosema mwaka jana, “sio
tu kwamba Wazanzibari hawajui ni kiasi gani cha fedha zao zilichukuliwa na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano kufuatia kuvunjwa kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika
Mashariki, bali pia hawana uhakika watazirudishiwa lini!”
Mheshimiwa Spika,
Kwa vile fedha za Zanzibar katika
Bodi ya Sarafu zilichukuliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano baada ya
masuala ya fedha, sarafu na Benki Kuu kufanywa kuwa mambo ya Muungano mwaka
1965, sisi tuliozaliwa ndani ya Muungano tuna haki ya kuambiwa ukweli kwanini
Serikali hii ya CCM imeshindwa kurudisha fedha hizo kwa Wazanzibari kwa
takriban miaka hamsini tangu fedha hizo zinyakuliwe na Serikali ya Jamhuri ya
Muungano aka Serikali ya Tanganyika?
Tunahitaji kuelezwa Serikali hii ya CCM inahitaji muda wa miaka mingapi mingine
ili iweze kurudisha fedha za watu na kuwaepusha Watanganyika na laana ya wizi
wa fedha za Wazanzibari?
Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar au Wazanzibari wenyewe katika
umoja wao, wana haki ya kutumia njia yoyote ile watakayoona inafaa, ikiwamo
kufungua kesi za madai katika mahakama za ndani au mahakama za kimataifa, kudai
fedha zake zote halali ambazo zimeibiwa na Tanganyika kwa kutumia kivuli cha
Muungano katika kipindi chote cha miaka hamsini ya Muungano huu.
Mheshimiwa Spika,
Kwa vyovyote vile, takwimu hizi zinaonyesha
kwamba, kwa sababu ya Muungano huu, uhusiano kati ya Tanganyika na Zanzibar ni
uhusiano wa kinyonyaji. Kwa sababu hiyo, huu ni uhusiano wa kikoloni. Ni
uhusiano kati ya ‘himaya’ ya Tanganyika na ‘koloni’ lake la Zanzibar. Himaya za
kikoloni huwa zinadhibiti masuala yote ya ulinzi na usalama, mambo ya nje na
uhusiano wa kimataifa, uraia, kodi, fedha, sarafu na benki kuu ya makoloni yao.
Na himaya za kikoloni huwa zinatumia nguvu na udhibiti wao wa masuala haya
kuyanyonya makoloni yao kiuchumi, kuyadidimiza kijamii na kuyatawala kisiasa.
Hivi ndivyo ambavyo imekuwa kwa mahuasiano kati ya Tanganyika na Zanzibar tangu
kuzaliwa kwa Muungano huu tarehe 26 Aprili, 1964.
Mheshimiwa Spika,
Tarehe 20 Aprili, 1968, Mwalimu
Nyerere alisema yafuatayo wakati akihojiwa na gazeti la The Observer la London, Uingereza: “If the mass of the people of Zanzibar should, without external
manipulation, and for some reason of their own, decide that the Union was
prejudicial to their existence, I could not bomb them into submission.... The
Union would have ceased to exist when the consent of its constituent members
was withdrawn.” Yaani, “endapo umma
wa wananchi wa Zanzibar wataamua, bila kurubuniwa kutoka nje na kwa sababu zao
wenyewe, kwamba Muungano unaathiri kuendelea kuwepo kwao, sitaweza
kuwalazimisha kwa kuwapiga mabomu.... Muungano hautaendelea kuwepo pale ridhaa
ya washirika wake itakapoondelewa.”
Miaka 45 baada ya kauli hiyo ya
Mwalimu Nyerere, Maalim Seif Shariff Hamad, Makamu wa Kwanza wa Rais wa
Zanzibar, alisema yafuatayo katika Maoni aliyoyatoa kwa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba tarehe 13 Januari, 2013: “Mfumo
(wa Muungano) uliopo sasa hauinufaishi Zanzibar na hivyo haukubaliki kwa
Wazanzibari. Koti la Muungano kama lilivyo sasa linabana sana. Wakati umefika
tushone koti jipya kwa mujibu wa mahitaji ya zama hizi.”
Nalo Baraza la Wawakilishi
Zanzibar, katika maoni yake kwa Tume ya tarehe 5 Februari, 2013, limetaka ‘kuwa
na Muungano wa dhati’, yaani “...
Muungano wa kweli, hata kama ni kwa maeneo machache, kwa dhati ya wanasiasa na
Watanzania kwa ujumla.” Kwa mujibu wa Baraza hilo, Muungano ‘wa dhati’ na
‘wa kweli’ ni ule ambao kuna “... Mamlaka
ya Zanzibar huru na Mamlaka ya Tanganyika huru ndani ya Muungano, (na) Mamlaka
ya Muungano iwekwe wazi – maeneo yake, uwezo au nguvu zake, na utendaji wake.
Mambo yote hayo yawekwe wazi na mipaka yake.”
Aidha, Baraza la Wawakilishi
limependekeza kwamba “rasilmali za
Muungano ziwe ni milki ya pande mbili za Muungano; na rasilmali hizo ndio
zitumike katika uendeshaji wa Mamlaka za Muungano. Ugawaji wa rasilmali ufanywe
kwa uwiyano maalum utakaokubaliwa kwa pamoja na pande mbili za Muungano.”
Hata kama baadhi ya wajumbe wa
Baraza la Wawakilishi Zanzibar baadaye waliyakana maneno yao haya walipofika mbele
ya wakubwa wao wa Tanganyika wakati wa vikao vya Bunge Maalum hapa Dodoma, haya
sio maneno ya kupuuza hata kidogo kwa sababu yanathibitisha kwamba hata wale
Watanzania wachache, kama wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, ambao
wamefaidika kwa kupata nafasi za uongozi kwa sababu ya Muungano, hawauoni
Muungano huu kama kielelezo cha umoja, mshikamano na upendo wao. Kuyapuuza
maneno haya ni kujenga misingi imara na hakika ya Muungano huu kuvunjika.
NCHI MOJA AU NCHI MBILI?
Mheshimiwa Spika,
Kuna propaganda na uongo mwingine
juu ya Muungano huu ambayo imeenezwa sana katika kipindi hiki cha nusu karne ya
uhai wake. Propaganda hii inahusu kile kilichozaliwa na Hati ya Makubaliano ya
Muungano, yaani Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Baada ya jina la
Jamhuri hiyo kubadilishwa kuwa Tanzania tarehe 28 Oktoba, 1964, ilizaliwa dhana
kwamba Makubaliano ya Muungano yaliua nchi za Tanganyika na Zanzibar na
kuanzisha ‘nchi moja’ ya Tanzania. Dhana hii imetumika, katika miaka hamsini ya
Muungano huu, kuhalalisha ukiukwaji wa matakwa ya Makubaliano ya Muungano kwa
kutumia dhana nyingine ya ‘kuimarisha Muungano.’ Dhana hizi mbili ndio msingi
wa nyongeza zote za mambo ya Muungano, na ndio sababu kubwa ya kuporomoka kwa
uhuru na mamlaka ya Zanzibar katika kipindi hicho.
Mheshimiwa Spika,
Dhana kwamba Hati ya Makubaliano
ya Muungano iliua nchi mbili na kuzaa nchi moja ya Tanzania ni dhana potofu na
isiyokuwa na msingi wowote katika Hati yenyewe. Kwanza, Hati ya Makubaliano ya
Muungano ilitamka wazi kwamba sheria zilizokuwepo Tanganyika na Zanzibar kabla
ya Muungano zitaendelea kutumika ‘katika nchi zao’ hadi hapo zitakaporekebishwa
ili kutilia nguvu Muungano na Hati za Muungano; au sheria mpya zitakapotungwa
na mamlaka husika au kutolewa kwa amri ya Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa ajili
ya utekelezaji wa Mambo ya Muungano kwa upande wa Zanzibar.
Pili, vifungu mbali mbali vya
Katiba zilizofuatia Makubaliano ya Muungano ziliweka wazi kwamba Tanganyika na
Zanzibar hazikuuawa na Makubaliano ya Muungano. Hivyo basi, hata baada ya
mabadiliko ya jina kwenda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Katiba na sheria
mbali mbali ziliendelea kutumia jina la Tanganyika na Zanzibar. Kwa mfano, Sheria ya Kuongeza Muda wa Kuitisha Bunge la
Katiba, 1965, iliyosainiwa na Rais Nyerere tarehe 24 Machi, 1965, inataja,
katika vifungu vyote vitatu, ‘Sheria za Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.’
Aidha, Sheria ya Kutangaza Katiba ya Muda ya Tanzania ya tarehe 11 Julai,
1965, ilitangaza kwamba ‘Tanzania ni Jamhuri Huru ya Muungano’; kwamba eneo
lake ni “... eneo lote la Tanganyika na
Zanzibar ...” na kwamba chama kimoja cha siasa “... kwa Tanganyika kitakuwa Tanganyika African National Union
(TANU)....” Kwa wakati wote wa uhai wake, Katiba ya Muda haikuwahi kutamka
kuwa Tanzania ni nchi moja. Badala yake, ibara ya 27(1) ya Katiba hiyo
iliyokuwa inahusu sifa za kuchaguliwa kuwa mbunge ilitamka wazi kwamba: “Raia
yeyote wa Tanganyika ambaye amefikisha umri wa miaka ishirini na moja na ni
mwanachama (wa TANU) atakuwa na sifa ya kuchaguliwa kuwa mbunge wa jimbo....”
Kwa upande wake, licha ya kuanza
kutumia jina la Tanzania Bara na Tanzania Visiwani kwa mara ya kwanza, Toleo la
Kwanza la Katiba ya sasa ya Muungano lilitamka kwamba Tanzania ni ‘Jamhuri ya
Muungano.’ Hapa pia hapakuwa na tamko la ‘nchi moja.’
Mheshimiwa Spika,
Maneno ya ibara ya 1 ya Katiba ya
sasa ya Muungano kwamba “Tanzania ni nchi
moja na ni Jamhuri ya Muungano” yaliingia katika kamusi ya kikatiba na
kisiasa ya nchi hii kufuatia ‘kuchafuka kwa hali ya kisiasa ya Zanzibar’ na
kung’olewa madarakani kwa Rais Aboud Jumbe. Kufuatia hali hiyo, Katiba ya
Jamhuri ya Muungano ilifanyiwa marekebisho makubwa ambayo, pamoja na mengine,
yalitangaza kuwa “Tanzania ni nchi moja
na ni Jamhuri ya Muungano.” Kwa sababu ya upinzani mkubwa wa Wazanzibari,
Marekebisho hayo ya Katiba yaliondoa pia maneno ‘Tanzania Visiwani’ na kuweka
‘Tanzania Zanzibar’ badala yake. Maneno ‘Tanzania Bara’ yalibaki kama
yalivyowekwa mwaka 1977.
Kwa maana hiyo, dhana ya Tanzania
kama nchi moja haijatokana na Makubaliano ya Muungano bali ilitokana na siasa
za Muungano, yaani mvutano kati ya viongozi wa Tanganyika wakiwa wamevalia joho
la Jamhuri ya Muungano na viongozi wa Zanzibar waliotaka uhuru zaidi kwa nchi
yao. Pili, dhana hiyo haina umri mkubwa sana kuliko inavyodhaniwa, kwani
iliingia kwenye Katiba mwaka 1984, miaka thelathini iliyopita, na miaka
ishirini baada ya Muungano.
MUUNGANO USIO WA USAWA
Mheshimiwa Spika,
Tangu mwanzo Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar haukuwa Muungano wa usawa. Huu ni Muungano ulioipa
Tanganyika – ikiwa imevalia koti la Jamhuri ya Muungano - mamlaka ya kuingilia
uhuru na mamlaka ya Zanzibar. Hii inathibitishwa na Hati ya Makubaliano ya
Muungano yenyewe. Kwanza, kwa kutamka kwamba katika kipindi cha mpito “Katiba ya Jamhuri ya Muungano itakuwa ni
Katiba ya Tanganyika...”, ni wazi kwamba Mshirika wa Muungano aliyekuwa na
nguvu katika Muungano huu ni Tanganyika.
Pili, kwa kuweka orodha ya mambo
11 ya Muungano, ni wazi kwamba Zanzibar ilinyang’anywa mamlaka juu ya masuala
hayo na mamlaka hayo yalihamishiwa kwa Tanganyika ikiwa imevaa koti la Jamhuri
ya Muungano. Kwa maana hiyo, Zanzibar ilinyang’anywa mamlaka yake juu ya
masuala ya nchi za nje, ulinzi, polisi, mamlaka ya hali ya hatari, uraia,
uhamiaji, biashara ya nje na mikopo na masuala mbali mbali ya kodi. Hati ya Makubaliano
ya Muungano yenyewe inasema wazi kwamba “Bunge
na Serikali (ya Jamhuri ya Muungano) litakuwa na mamlaka kamili kwenye mambo
hayo kwa Jamhuri ya Muungano na, kwa nyongeza, mamlaka kamili kwa ajili ya
mambo mengine yote ya na kwa ajili ya Tanganyika.”
Tatu, kwa kutangaza kwamba rais
wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano atakuwa Mwalimu Nyerere na Makamu wa kwanza wa
Rais atakuwa Sheikh Abeid Karume; na kwa kutangaza kwamba Makamu wa Kwanza wa
Rais atakuwa ndiye msaidizi mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano katika
utekelezaji wa majukumu yake ya kiutendaji kuhusu Zanzibar, ni wazi kwamba Hati
ya Makubaliano ya Muungano ilithibitisha nafasi ya chini (subordinate position) ya Zanzibar katika Muungano.
Nne, kwa kuzifanya alama za
utaifa (national emblems) za Tanganyika
kuwa ndio alama za taifa za Jamhuri ya Muungano, kuna-emphasize superior position ya Tanganyika ndani ya Muungano na subaltern position ya Zanzibar katika
Muungano huu. Ukweli huo huo unahusu masuala ya kuzifanya taasisi na watumishi
wa Serikali ya Tanganyika kuwa ndio taasisi na watumishi wa Jamhuri ya
Muungano.
Tano, hata kwa kuangalia watu
ambao wamewahi kupata fursa ya kuongoza Jamhuri ya Muungano, ni wazi kwamba
Watanganyika ndio wamekuwa mabwana na Wazanzibari wamefanywa watwana katika masuala
ya haki za kiutawala. Hivyo, kwa mfano, katika kipindi cha miaka hamsini ya
Muungano huu, ni Mzanzibari mmoja tu ndiye aliyepata fursa ya kuwa Rais wa
Jamhuri ya Muungano, kwa miaka kumi kati ya miaka hamsini hiyo.
Kwa utaratibu huo huo, tokea
mwaka 1964, Zanzibar haijawahi kutoa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Mkuu wa Jeshi
la Polisi au Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania. Zote hizi ni taasisi za Muungano.
Aidha, Zanzibar imewahi kutoa Waziri Mkuu mmoja tu, tena kwa kipindi cha mwaka
mmoja na nusu, na Jaji Mkuu mmoja tu katika kipindi hicho cha nusu karne ya
Muungano huu. Vile vile, katika
Diplomatic Corps, kwa sasa kuna Wazanzibari wawili tu ambao ni mabalozi wa
Tanzania nchi za nje kati ya mabalozi 32 wanaoiwakilisha Tanzania nchi za nje.
Mheshimiwa Spika,
Hata Bunge lako tukufu lina
rekodi mbaya katika masuala haya. Hivyo, kwa mfano, katika miaka yote ya
Muungano, hakuna Mzanzibari ambaye amewahi kushikilia nafasi ya Spika au Naibu
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano. Aidha, licha ya Kanuni za Bunge lako tukufu
kuruhusu kufanyika kwa vikao vya Kamati zake za Kudumu nje ya Dodoma, yaani Dar
es Salaam na/au Zanzibar; na licha ya Kanuni kuruhusu Mikutano ya Bunge
kufanyika nje ya Dodoma ikiwa ‘itaelekezwa vinginevyo’, hakuna Kamati hata moja
ya Bunge hili tukufu ambayo imewahi kufanya vikao vyake Zanzibar na haijawahi
kutokea Bunge hili likaelekezwa kufanya Mikutano yake nje ya Tanganyika!
KURA YA MAONI JUU YA MUUNGANO
Mheshimiwa Spika,
Baada ya nusu karne ya Muungano
wa aina hii, wananchi wa Tanganyika na, hasa wa, Zanzibar hawako tayari
kuendelea na utaratibu huu wa kinyonyaji na kikandamizaji. Wananchi wanataka
mabadiliko ya msingi ya muundo wa Muungano na uendeshaji wake. Wananchi
wanataka kusikilizwa juu ya Muungano. Wananchi wanataka kufanya maamuzi kuhusu
kama wanataka kuendelea na Muungano na, kama jibu ni ndiyo, muundo wa Muungano
huo.
Wakati wa mjadala wa Sura ya
Kwanza na ya Sita ya Rasimu ya Katiba katika Bunge Maalum, Kamati nyingi
zilishindwa kufanya maamuzi kwa sababu ya kukosa uungwaji mkono wa theluthi
mbili ya wajumbe wote wa Kamati kutoka Tanganyika na idadi hiyo hiyo ya wajumbe
kutoka Zanzibar. Kama hali ni hiyo katika Bunge Maalum licha ya Bunge hilo
kujazwa wajumbe wengi wa CCM kutoka kundi la 201, hali ni mbaya zaidi nje ya
Bunge Maalum na nje ya Bunge lako tukufu. Nje ya mabunge haya, watu wengi, hasa
Wazanzibari ambao ndio wamekuwa waathirika wakubwa wa Muungano huu katika nusu
karne ya maisha yake, wananchi wengi hawataki tayari kuendelea na Muungano huu.
Mheshimiwa Spika,
Katika mazingira haya, namna
muafaka ya kutoka katika constitutional impasse
inayokuja mbele yetu, ni kuwauliza wananchi wa Tanganyika na Zanzibar – kwa
kutumia kura ya maoni - kama bado wanataka kuendelea na Muungano huu. Na kama
jibu lao litakuwa ni ndiyo, basi wananchi waamue, katika kura hiyo, ni muundo
gani wa Muungano wanautaka. Miaka hamsini ya watawala kuamua masuala haya
muhimu peke yao inatosha. Huu ni wakati muafaka kwa wananchi kufanya maamuzi
haya makubwa kwa maisha yao na kwa nchi zao mbili. Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni inawataka wabunge wa Bunge lako tukufu wawe kwenye upande sahihi wa
historia, yaani upande wa wananchi katika jambo hili.
HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
Katika kuhitimisha maoni haya,
napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza viongozi wakuu wa vyama
vyetu vitatu vinavyounda Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa kufanya maamuzi ya
kuendeleza ushirikiano ulioanzia ndani ya Bunge Maalum, kwenye Bunge lako
tukufu. Wananchi wetu wanataka mabadiliko ya msingi ya utawala wa nchi zetu mbili
na usimamizi wa rasilmali zake. Kama ilivyokuwa kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi
(UKAWA) ndani ya Bunge Maalum, ndivyo wananchi wanavyotutazamia kuendesha
shughuli zetu ndani ya Bunge hili tukufu. Historia itatuhukumu vikali endapo
tutashindwa kukamata fursa hii ya kihistoria katika nchi zetu mbili.
Baada ya maelezo haya marefu,
naomba kukushukuru na wewe binafsi na naomba kuwasilisha.
---------------------------------------------------------------
Tundu Antiphas Mughwai Lissu
MSEMAJI & WAZIRI KIVULI, OFISI
YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO)
KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI
Lisu,
ReplyDeleteHii nondo aliyotoa inahitaji kuhifadhiwa kwa makini kama serikali inavyodai kutunza hati ya muungano. Well said Lisu, hakuna chenga hapo, and you stand on the truth and the history will recall this.
Great