Friday, April 25, 2014

Warioba:Matusi hayataleta Katiba

Wakati  matusi, dhihaka na kejeli dhidi ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba,  yakipamba moto ndani ya Bunge Maalum la Katiba, amewataka wajumbe hao kuacha malumbano na kuishambulia Tume na badala yake watafute maridhiano vinginevyo katiba mpya haitapatikana.

Warioba pia alionyesha kusikitishwa na kile kinachoendelea katika Bunge hilo kwa baadhi ya wajumbe wake kurushiana maneno wao kwa wao, huku wakitumia lugha ambazo hazina matumaini kwa ajili ya kufanikisha upatikanaji wa katiba mpya.

Alisema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuzindua ripoti maalumu iliyotolewa na Taasisi ya Utafiti ya Twaweza kuhusu Katiba, jana jijini Dar es Salaam.

Kutoakana na hilo, aliwataka wajumbe kujirekebisha kwa kujadili kwa kina rasimu ya katiba, ambayo ina maoni ya wananchi, kwani ndicho kilichowapeleka katika Bunge hilo.

“Tume ilipata maoni kutoka kwa wananchi wanaozungumzia utawala bora, wanataka kuwapo kwa miiko ya uongozi. Lazima uwazi, ukweli na uwajibikaji uthaminiwe. Wajirekebishe, wafanye kile ambacho wananchi wamewapeleka,” alisema Jaji Warioba.

Mbali na hilo, pia Warioba alieleza kuingiwa na wasiwasi wa kupatikana katiba mpya kutokana na namna ambavyo majadiliano yanaendelea bungeni kwa baadhi ya wajumbe kurushiana maneno ya kejeli ambayo hayalengi kufanikisha kazi hiyo kubwa ya taifa.

“Lugha wanayotumia hainipi matumaini ya kufanikiwa katika kazi waliyopelekwa hapo. Naomba wasiijadili tume, bali wajadili mambo ya msingi yaliyomo kwenye rasimu hiyo ambayo ni maoni ya wananchi. Yaliyomo kwenye rasimu siyo mali ya Tume, ni maoni ya wananchi.” 

Aliwashauri wajumbe hao kufikia maridhiano kwa kuwa katiba haiwezi kupatikana bila ya kuwapo kwa muafaka baina yao.

Alisema Tume hiyo iliundwa na watu kutoka makundi na itikadi tofauti, lakini walifanikisha kazi ya kuzunguka sehemu mbalimbali nchini kukusanya maoni kutoka kwa wananchi na kuyaweka kwenye rasimu hiyo bila malumbano yoyote baina yao jambo ambalo linaonekana kuwapa shida wajumbe wa Bunge hilo.

“Ni lazima pawepo na maridhiano na makubaliano baina yao, lakini kwa hali hii ninayoiona ikiendelea, sijui kama watafanikiwa katika kazi hiyo,” alisema Jaji Warioba
Aliongeza: “Sisi tulikuwa na makundi mbalimbali, lakini hatukuwa na siasa katika kazi ya kukusanya maoni. Tulikuwa pamoja hadi kufanikisha kazi, Tume ilikuwa ya wananchi.”

Jaji Warioba alitoa kauli hiyo kufuatia mashambulizi makubwa yanayoendelea kutolewa dhidi yake na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba aliyokuwa anaiongoza, kutoka kwa baadhi ya wanasiasa, wakiwamo wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, kwamba yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba ni maoni ya Tume na siyo ya Watanzania.

Kwa upande wake, mjumbe wa Bunge la Katiba, ambaye pia ni Mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangalla, alisema kujitoa kwa baadhi ya wajumbe kutoendelea na vikao, siyo sababu ya kuvunjika kwa Bunge hilo bali litavunjika lenyewe hapo baadaye iwapo safu inayotakiwa kikanuni itapungua.

Kwa mujibu wa Dk. Kigwangalla, katiba haiwezi kupatikana bila kuwapo kwa maridhiano baina ya makundi yanayohusika na hivyo kumtaka Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, kuunda Kamati ya Maridhiano ili kufikia mwafaka wa mchakato huo, kwani kanuni zinaruhusu. 

“Kama hakutakuwapo maridhiano baina ya wajumbe, basi turudi kwenye katiba ya zamani. Kinachoniuma zaidi ni kwamba, kwa nini kuendelea kujadili suala moja tu huku kukiwa na masuala ya msingi kwa ajili ya wananchi ambayo yapo kwenye rasimu?” alihoji Kigwangalla.

Aliongeza: “Kama tunataka kuendelea kujadili kuhusu muundo wa serikali, basi paundwe na mabunge ya Tanganyika, Muungano na Zanzibar kwa ajili ya kujadili mambo yake.”

Mjumbe wa Bunge hilo, Julius Mtatiro alisema iwapo wajumbe wanataka kujadili muundo wa serikali mbili, basi iundwe tume nyingine kwa ajili ya kujadili aina hiyo ya serikali.

Pia alisema iwapo baadhi ya wajumbe watang’ang’ania serikali mbili, kitakachotokea ni kwamba, wananchi watakuwa na katiba ile ile iliyopo na hivyo kukosa yale waliyoyataka kuingizwa kwenye ile mpya kwa ajili ya mustakabali wao.

No comments:

Post a Comment