Viongozi wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), wamesema hawajaridhishwa na hatua ya jeshi la polisi ya kuzuia mkutano wao wa hadhara uliokuwa ufanyike visiwani Zanzibar jana na kwamba sasa wanaandaa maandamano na mikutano ya nchi nzima.
Wamesema hatua hiyo ya polisi imetokana ni shinikizo la Waziri Mkuu na Makamo wa Pili wa Rais Zanzibar.
Wakizungumza na waandishi wa habari visiwani hapa jana, viongozi hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, walisema ni haki yao ya kisiasa kufanya mkutano wa hadhara sehemu yoyote nchini.
Akiongea kwa niaba ya viongozi wenzake, Profesa Lipumba alisema kuzuiliwa kufanya mkutano huo kumewasha ari na hamasa ya kujipanga vizuri kufanya mikutano katika mikoa yote ya Tanzania.
Profesa Lipumba alisema Aprili 23, mwaka huu wanatarajia kufanya maandamano na mkutano mkubwa wa hadhara katika Viwanja vya demokrasia Kibandamaiti Visiwani na Aprili 24, watafanya mkutano na maandamano kisiwani Pemba.
Alisema lengo la maandamano na mkutano huo ni kudai mawazo ya wananchi walio wengi ambao walitoa mawazo yao katika Tume ya kukusanya maoni ya kutaka serikali tatu yaheshimiwe.
“Tutahakikisha tunakwenda kila mkoa kufanya mkutano wa hadhara na maandamano ya aina yake ambapo kwa kuanzia tutaanza Zanzibar na maandamano na mikutano hiyo itakuwa ya amani na usalama,”alisema Profesa Lipumba.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema zipo propaganda nyingi zinazoenezwa kuwa kuwapo kwa mfumo wa serikali tatu ni kueneza mfumo wa dola ya Kiislamu kitu ambacho siyo kweli.
“Hizo ni fikra hasi hakuna mwanadamu mwenye benki ya fikra…,”alisema. Alifafanua kuwa mfumo wa serikali tatu au mkataba kamwe hautovuruga mawasiliano na udugu baina ya Wazanzibari na Watanganyika.
Aliwataka Wazanzibar kutosita kudai haki zao na kutokubali kuburuzwa kwa kuendelea na mfumo wa serikali mbili na kuwasisitiza kudai haki zao mpaka kieleweke.
Alisema viongozi waliokuwapo madarakani ndiyo wanaoleta uchochezi na ubaguzi miongoni mwa Waunguja na Wapemba hivyo aliwataka wananchi kutokubali kubaguliwa.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema mikutano na maandamano itakayofanyika kila mkoa itakuwa ni mikutano ya umoja wa vyama vya siasa, taasisi za dini na taasisi nyingine na siyo mikutano ya Ukawa.
Alisema hotuba ya ufunguzi wa Bunge la Katiba iliyotolewa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano ndiyo iliyosababisha Bunge la Katiba kuchafuka na yeye ndiye anayepaswa kulaumiwa kwa kuharibu mchakato mzima wa katiba.
Aidha, viongozi hao walisema hati ya Muungano iliyowasilishwa katika Bunge la Katiba ni ya kughushi kwa walichokidai kuwa saini ya mzee Karume iliyosainiwa siyo sahihi.
BIG UP WANAHARAKATI WA UKWELI
ReplyDelete