Friday, February 7, 2014

Ndesamburo: Nitalirudisha Soko la Kiborloni

MBUNGE wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (Chedema), amewahakikishia wakazi wa Kata ya Kiborloni kuwa atalirejesha soko lao la nguo na viatu vya mitumba lililohamishwa mwaka 2007.
Soko hilo maarufu kwa wakazi wa mikoa ya Kilimanjaro na Arusha lilihamishwa Kata ya Kiborloni na kupelekwa eneo la Memorial Kata ya Karanga na kusababisha usumbufu kwa wafanyabiashara.
Akihutubia mkutano wa hadhara sokoni hapo jana wakati wa kumnadi mgombea udiwani wa kata hiyo, Frank Kagoma, mbunge huyo alisisitiza kuwa litarudi.
Ndesamburo maarufu kama ‘Ndesa pesa’ ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Kilimanjaro, alisema alikuwa na ugomvi na Mkurugenzi aliyestaafu wa Manispaa ya Moshi, Bernadeta Kinabo, kuhusu suala hilo.
“Naapa kwamba Soko la Kiborloni lazima lirudi hapa. Piga ua, mvua inyeshe ama jua liwake lazima soko litarudi na mtaendelea kufanya biashara zenu kama kawaida.”
Aliwataka wananchi wa kata hiyo kumchagua mgombea wa CHADEMA katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Februari 9, akisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimekuwa balaa.
“Ndugu zangu CCM imekuwa balaa, achaneni nayo, inataka kuwarudisha kwenye vumbi wakati sisi tumekuwa tukiwapigania ili mpate barabara za lami.
“Najua mmekwishaamua diwani wenu awe huyu Kagoma, sasa hakikisheni Jumapili mnajitokeza kwa wingi kupiga kura na mzilinde, kisha baadaye tutasherehekea pamoja,” alisema Ndesamburo.
Kwa upande wake Kagoma aliwaomba wananchi kupuuza propaganda chafu za CCM kwamba si Mtanzania, akisema hata wakimfunga sasa atashinda akiwa gerezani.
Uchaguzi katika kata hiyo unafanyika baada ya aliyekuwa Diwani wake, Vincent Rimoi (CHADEMA) kufariki dunia mwaka jana.

No comments:

Post a Comment