Friday, February 7, 2014

CHADEMA yabaini njama Polisi, CCM

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimebaini hujuma zinazodaiwa kufanywa kwa ubia kati ya Jeshi la Polisi na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutaka kuanzisha vurugu kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani unaotarajiwa kufanyika kesho kutwa katika kata 26 nchini.
Chama hicho kimeeleza kuwa hata matukio ya kuvamiwa, kupigwa na kisha kukamatwa kwa wafuasi wa CHADEMA ni matokeo ya hujuma hizo.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa
Oganaizesheni na Usimamizi wa Kanda, Benson Kigaila, wakati akizungumza na waandishi wa habari, kuelezea ushiriki na mkakati wa CHADEMA katika uchaguzi  mdogo wa Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa.
Mbali na kuelezea mkakati wa ushindi katika Jimbo la Kalenga, pia Kigaila alielezea  matukio yanayotokea katika kampeni ya uchaguzi mdogo wa madiwani kwa kata 26 unaoendelea sasa sehemu mbalimbali nchini.
Akizungumzia ushirikiano wa Polisi na CCM katika kuihujumu CHADEMA, Kigaila alisema mkakati huo ulianza wakati wa M4C Operesheni Pamoja Daima, ambapo wakiwa mkoani Mbeya katika Wilaya ya Mbarali, waligundua kambi ya vijana wa CCM wapatao 300 waliopangwa kufanya vurugu kwenye mkutano wa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa, mkoani humo.
“Tulipobaini mbinu zao niliwasiliana na RPC Mbeya, chakushangaza badala ya kushughulika na wahalifu hao, akaamua kumuita mwenyekiti wa CCM wa mkoa huo na kumueleza wasitishe vurugu walizopanga kuzifanya na kama zingefanyika, tuliwaambia tutamkamata mwenyekiti wa mkoa badala ya wafanya vurugu na kweli wakasitisha,” alisema Kigaila.
Alisema kinachosikitisha ni kuona wafuasi wa CHADEMA wakipigwa na kuumizwa, lakini polisi inawakamata watu walioumizwa badala ya kuwatafuta waliosababisha maumivu hayo.
“Waliofanya fujo CCM, walioumizwa CHADEMA, waliokamatwa CHADEMA, inakuwaje hali hii na haya mambo ya CCM kwanini yanaibuka kila panapokuwa na uchaguzi?” alihoji Kigaila.
Alisema tayari malalamiko yao dhidi ya polisi  wameyafikisha kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye ndiye mlezi wa vyama nchini na kumuomba aingilie kati hali hiyo kabla uvumilivu haujawashinda wafuasi wao.
16 wajitokeza Kalenga
Akizungumzia maandalizi ya uchaguzi wa Jimbo la Kalenga lililoachwa wazi na marehemu William Mgimwa, Kigaila alisema kazi ya kuchukua fomu ndani ya chama imeshaanza na hadi jana watu 16 walishachukua fomu kuomba ridhaa ya chama.
Alisema fomu za  CHADEMA zimeanza kutolewa juzi na mwisho ni Februari 9 na hadi jana watu 16 walishachukua fomu.
Aliongeza kuwa fomu zinapatikana katika tovuti ya CHADEMA ya www.chadema.or.tz, pia makao makuu ya chama hicho pamoja na ofisi ya Jimbo la Kalenga.
Kigaila alisema Kamati Kuu ya CHADEMA itakutana Februari 12 kwa ajili ya uteuzi wa mwisho wa mtu atakayepeperusha bendera ya CHADEMA.
Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga  unafanyika kuziba nafasi ya marehemu William Mgimwa aliyefariki dunia Januari Mosi nchini Afrika Kusini alikokuwa akipata matibabu.

No comments:

Post a Comment