MBUNGE wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (48) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Iringa kwa tuhuma za kujeruhi katika kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani Kata ya Nduli.
Mbele ya Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Godfrey Isaya, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Elizabeth Swai, alisema Mchungaji Msigwa alitenda kosa hilo Februari 5, 2014 katika Kijiji cha Nduli, mjini Iringa.
Katika kesi hiyo namba 28 ya mwaka 2014 mbunge huyo anadaiwa kumjeruhi Salum Kahita kinyume cha kifungu kidogo namba 225 cha sheria ya kanuni za adhabu.
Msigwa anayetetewa na Wakili Lwezaula Kaijage alikana kosa hilo na hakimu aliahirisha kesi hadi Machi 10 itakapotajwa tena kwa kuwa upelelezi wake haujakamilika.
Pamoja na mbunge huyo, Jeshi la Polisi limewapandisha kizimbani Meshack Chonanga (22) na Paulo Mapunda wote wanakijiji cha Nduli mjini Iringa wakituhumiwa kumjeruhi Alex Mpiluka wakati wa kampeni hizo.
Hata hivyo watuhumiwa wote walipata dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili walioweka dhamana ya ahadi ya sh milioni mbili kila mmoja.
Wakati huohuo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, imemwachia kwa dhamana Mbunge wa Maswa Mashariki, Sylvester Kasulumbayi (CHADEMA).
Dhamana ya mbunge huyo ilishindikana juzi kutokana na zuio la hati ya kiapo kutoka kwa Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Shukrani Madulu.
Kasulumbayi na wenzake 12 akiwemo Diwani wa Buselesele, Christian Kagoma wanakabiliwa na tuhuma za kuwacharanga mapanga wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani wilayani Kahama.
Awali akisoma uamuzi mdogo mahakamani hapo, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya, Gadiel Mariki, alitupilia mbali cheti cha kiapo kwa madai ya kuwa na upungufu wa kisheria, hivyo kukosa uzito wa kuzuia dhamana kwa watuhumiwa hao.
Hakimu Mariki alisema cheti cha kiapo hakikuonyesha taarifa ya majeruhi watatu ambao hali zao ni mbaya, kimetolewa na nani, pia nafasi ya mkurugenzi wa kiapo haikuwa na sahihi wala kuonyesha kiapo cha dini gani.
Baada ya kutupa kiapo hicho, alisema dhamana ipo wazi kwa watuhumiwa wote 13 na kwamba kila mshitakiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili huku mmoja akiwa na hati ya vielelezo vya mali isiyohamishika yenye thamani isiyopungua sh milioni 10.
Licha ya watuhumiwa wote kupewa dhamana, ni mbunge huyo peke yake aliyeweza kutimiza masharti ya dhamana huku watuhumiwa wenzake wakiendelea kusota rumande kwa kushindwa kutimiza masharti hayo.
No comments:
Post a Comment