Friday, February 7, 2014

Bunge la Katiba laiva

RAIS Jakaya Kikwete leo anatarajia kutangaza majina ya wajumbe kutoka makundi mbalimbali walioteuliwa kuingia kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
Majina hayo yanatangazwa leo baada ya Rais Kikwete kuyatema majina 3,573 ya watu waliomba kuingia kwenye Bunge hilo linalotarajiwa kuanza Februari 18 mjini Dodoma.
Miongoni mwa waliotoswa ni pamoja na watu maarufu, wenye uzoefu na sifa ya kuingia katika Bunge hilo, lakini ameteua majina 201 kwa mujibu wa Katiba kuingia kwenye Bunge hilo.
Akizungumza kwenye mkutano maalumu wa Baraza la Vyama vya Siasa, Rais Kikwete alisema jumla ya watu walioomba kuingia kwenye Bunge hilo ni 3,774 kutoka makundi mbalimbali.
Aliyataja makundi yaliyoomba kuwa ni pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali ambayo yaliwasilisha majina 1,647, lakini walioteuliwa ni 20 tu.
Makundi mengine na idadi waliyoomba kwenye mabano ni taasisi za dini (329), walioteuliwa 20, vyama vya siasa (198), waliopata nafasi ni 42, taasisi za elimu (130), walioteuliwa 20, vyama vya walemavu (140), walioteuliwa ni 20 na Baraza la Wafanyakazi (102), walioteuliwa ni 19 tu.
Mbele ya viongozi mbalimbali wa kisiasa na kidini, Rais Kikwete aliyataja makundi mengine yaliyoomba na nafasi walizopata kuwa ni wafugaji (47), wamepata nafasi 10, wavuvi (57), walioteuliwa ni 10, wakulima (157), walioteuliwa ni 10 na makundi yenye mlengo unaofanana waliomba nafasi 720, lakini walioteuliwa ni 20 tu.
“Watu 3,573 hawatakuwemo kwenye Bunge la Katiba, si kwamba hawafai, wamo maprofesa waliowasilisha CV zao ni nzuri, vimemo vilikuwa vingi lakini sina pakuwapeleka kwa sababu nafasi ni chache,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alisema kuwa leo anatarajia kutangaza rasmi majina ya wabunge hao kwani kazi iliyobaki ni kufanya uhakiki ili kuepuka kutoa wajumbe wengi kutoka mkoa mmoja na kuibua malalamiko.
Alisema kuwa baada ya kutangaza majina hayo, anafahamu wapo watakaokuja na malalamiko hasa yatakayotoka kwa wanasiasa lakini aliwaasa wasikwamishe mchakato wa Katiba Mpya kwa faida zao binafsi.
Kwa upande wa wajumbe watakaoteuliwa, Rais Kikwete aliwataka watambue kuwa wana dhamana kwa Watanzania na taifa kwa ujumla, hivyo anatarajia Katiba itakayoundwa itadumu kwa zaidi ya miaka 50.
“Katiba itakayoundwa iimarishe Muungano, amani, utulivu, mazingira mazuri ya kisiasa na uchumi. Wajumbe wawasilishe kile kilichomo kwenye rasimu ya pili ya Katiba na watangulize masilahi ya taifa,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete aliwasisitiza viongozi wa vyama vya siasa kwamba wana umuhimu mkubwa katika kuunda Katiba mpya, kwani Bunge hili limo mikononi  mwao.
“Mkielewana ninyi, wale wajumbe 201 hawana matatizo, lakini ninyi msipoelewana hata wale nao mtawachanganya, vyama vijenge na kusaidia kupatikana kwa Katiba Mpya itakayotusaidia katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na ule wa Serikali za Mitaa,” alisema Rais Kikwete.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, kauli ya wanasiasa na vitendo ndivyo vitakavyojenga au kubomoa ama kukwamisha kupatikana kwa Katiba Mpya.
Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM taifa, alisema Katiba itakayoundwa si ya CCM, CHADEMA, CUF wala chama chochote cha siasa na kama wabunge wakilitambua hilo, Bunge la Katiba litakuwa jepesi.
“Lakini tukitengeneza Katiba ya kile kinachotaka chama changu au cha mtu fulani, basi hapo tutakuwa na matatizo. Tuongozwe na hoja zitakazotolewa na wajumbe na si kwa ajili ya mtu au chama fulani.
“Na itakapopatikana Katiba mpya, sitarajii kama kuna mwanasiasa atakayeibuka na kuendeleza hoja ya Katiba na kama atakuwepo, mwanasiasa wa aina hiyo atakuwa amepauka kisiasa, awaache Watanzania wana mambo mengi ya kufanya,” alisema.
Akizungumzia kizungumkuti cha serikali tatu na serikali mbili, Rais Kikwete aliweka bayana kuwa wapo wengi wanaoona ugumu wa rasimu ya pili ya Katiba iko katika aina ya muundo wa Muungano.
Alisema hata chama chake cha CCM waliona kuna ugumu kwenye serikali tatu, lakini baada ya kupitia rasimu ya pili walibaini kuna mambo makubwa mengi ambayo suluhu yake si serikali mbili au tatu.
“Rasimu hii imezungumzia sifa ya kuwa rais.  Kuna mambo mengi ndani ya rasimu hiyo ya pili ambayo yasipoangaliwa kuna watu wameshawekeza kwenye suala la urais, hivyo wasipoiangalia rasimu hiyo kwa makini, wanaweza kuja kujuta huko mbele ya safari.
“Kwa mfano, rasimu inasema, huwezi kuwa rais mpaka uwe mbunge na mbunge aliyekaa kwa vipindi vitatu, anapoteza sifa ya kuwa mbunge na kuwa rais. Mtu wa aina hiyo kama ameshawekeza kwenye urais, atakuwa amepoteza fedha zake bure kwa sababu hana sifa tena. Hivyo jipeni muda kuangalia kila kipengele kwa makini,” alisema Rais Kikwete.
Kuhusu sheria inayompa mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa, Rais Kikwete alisema kazi ya msajili huyo kwa sasa sheria inamruhusu kufuta chama chochote cha siasa kinachokwenda kinyume cha Katiba kiasi cha kuonekana mbabe.
Alisema kuna haja ya kuangalia sheria hiyo ili kuweka unyumbufu mpana katika kulea vyama vya siasa nchini.
Rais Kikwete aliwataka wajumbe wa Bunge la Katiba kutambua kuwa wakishindwa, wajue tumeshindwa sote na nchi itakuwa imekwama na kuwataka viongozi wa vyama kutokwamisha mchakato wa Katiba mpya.
Akizungumzia ratiba ya Bunge la Katiba, Rais Kikwete alisema leo anatarajia kutangaza majina 201 ya wajumbe walioteuliwa kuingia kwenye Bunge hilo.
Alisema Februari 14 serikali itatangaza kwenye Gazeti la Serikali kama sheria inavyotaka na Bunge hilo linatarajiwa kuanza Februari 18, mwaka huu mjini Dodoma.
Alisema Bunge hilo litaketi kwa siku 70, lakini kama kuna hoja nzito zinazohitaji kuongezewa siku, serikali itaongeza siku 20 ili zifike siku 90.
Viongozi wa vyama vya siasa
Mwenyekiti wa taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema kuwa ni muhimu Rais Kikwete akafahamu kuwa migongano inasababishwa na viongozi wa chama chake.
Alisema kuwa Katiba ni maridhiano hivyo lazima wajumbe wa bunge hilo watafute muafaka ili kuweza kukubaliana.
“Vyama vina nafasi, ninamuomba Rais Kikwete ajaribu kuupeleka ujumbe huo kwa viongozi wa CCM kwa kuwa wamekuwa wakibeza baadhi ya vipengele vya rasimu ya Katiba na kusema kuwa si sera ya chama chao,” alisema.
Naye Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, alisema kuwa kauli ya Rais Kikwete imeacha ujumbe mzito na viongozi wa vyama vyote wanapaswa kutafakari kwa makini juu ya Bunge hilo.
Alisema ni ukweli usiopingika kuwa kila chama kina msimamo wake kuelekea Bunge la Katiba, hivyo ni vema wakaangalia na kuweka masilahi ya taifa ili kupata muafaka wa Katiba Mpya.
Naye Mwenyekiti wa taifa wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema taifa hili ni la Watanzania wote, hivyo ni muhimu kuweka mbele masilahi ya taifa ili  kupata Katiba iliyo na muafaka kwa kila upande.
“Kama tutatanguliza utaifa kwanza na kuwa tayari kusikiliza hoja za wengine, ingawa hapo ndipo penye tatizo kubwa na kuondoa unafiki, tutapata Katiba mpya nzuri na yenye manufaa,” alisema.

No comments:

Post a Comment