Saturday, February 22, 2014

Mnyika:Rasimu imepuuza rasilimali

Waziri Kivuli wa Nishati na Madini  na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika amesema rasimu ya pili ya Katiba haijazingatia masuala ya msingi kuhusu haki ya wananchi kumiliki na kunufaika na rasilimali za nchi.

Mnyika alisema hayo kupitia taarifa aliyoitoa kwenye vyombo vya habari na kuongeza kuwa hatua hiyo imekuwa kinyume na mapendekezo aliyoyatoa bungeni na mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba,  juu ya haki za wananchi kuhusu umiliki wa rasilimali.

Mnyika alisema alipendekeza Katiba mpya iweke ibara mahususi ya haki za wananchi kumiliki rasilimali ikiwamo ardhi, madini, gesi, mafuta, maji, misitu na maliasili nyingine.

Kadhalika, alisema wananchi wakipewa haki ya kumiliki na kuwekewa mazingira ya Kikatiba ya kunufaika na rasilimali zao, mianya ya mikataba mibovu, ufisadi na matumizi mabaya ya rasilimali itazibwa.

 “Natambua kwamba katika sura hiyo hiyo ya nne sehemu ya pili inayohusu wajibu na mamlaka za nchi ibara ya 51 ya  ulinzi wa mali za umma,  imetoa wajibu wa raia kulinda rasilimali na maliasili, hivyo, wadau wanapaswa kuendelea kujadili suala hili  kwa  maslahi ya uchumi wa nchi na  wananchi wenyewe.”

No comments:

Post a Comment