Saturday, February 22, 2014

Lissu, Lipumba, Werema jino kwa jino bungeni

Malumbano, vijembe na mvutano vimeanza kuibuka mapema katika Bunge la Katiba jana, baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kumaliza kutoa elimu na ufafanuzi kwa wajumbe kuhusu Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83, huku Tundu Lissu, akidai kuwa Jaji Werema amefanya upotoshaji mkubwa.

Lissu ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema na Mbunge wa Singida Mashariki, alidai kuwa Jaji Werema alifanya upotoshaji huo wakati akitoa ufafanuzi kuhusu sheria hiyo kwa wajumbe wa Bunge la Maaluma la Katiba jana.

Akiwa wa kwanza kuuliza swali baada ya Jaji Werema kumaliza kutoa darasa la somo la sheria hiyo kwa wajumbe na ufafanuzi mbalimbali, Lissu alisema, “Napenda kurekebisha upotoshaji uliofanywa na mjumbe.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, kifungu 25 (1) kinasema, ‘Bunge Maalum litakuwa na mamlaka ya kujadili na kupitisha masharti ya katiba inayopendekezwa, kutunga masharti ya mpito na masharti yatokanayo kama Bunge Maalum litakavyoona inafaa.

“Nguvu za wajumbe wa Bunge la Maalum ipo kwenye hicho kifungu cha 25 na kifungu cha 9 kinahusu kazi za Tume…mamlaka ya Bunge hili yako kwenye kifungu cha 25,” alisema na kuongeza, “Tafadhali tusipotoshane hapa.”

Baada ya hapo, alifuata Zitto Kabwe, aliyehoji kuwa katika sheria hiyo hakuna maeneo hayo ya ukomo ambayo yanahusisha Bunge Maalum la Katiba lakini Jaji Werema amesisitiza sana katika eneo hili.

Pia alitaka kujua baadhi ya makundi ya watu, taasisi na vyama ambavyo vimetengeneza rasimu mbadala za katiba na mamlaka ya wajumbe kuhusu rasimu hizo yapoje kupoea rasimu mbadala.

Kwa upande wake, Mwalimu Ezekiel Oluochi, akitokea kundi la vyama vya wafanyakazi alisema hakuna uhusiano wowote kati ya kifungu cha 9 na kifungu cha 25 cha sheria hiyo.

Naye Hamad Rashid, Mbunge wa Wawi (CUF), alihoji mamlaka ya Bunge hilo iwapo katika rasimu hiyo itaonekana Tume haikufanyakazi yake.

Mjumbe Hamza Hassan Juma, alitaka wajumbe wenzake kujikita zaidi katika sheria hiyo iliyowaleta hapo, na ndio maana waliomba wapewe muda wa kutosha wa kuipitia.

Christopher Ole Sendeka, alisema Bunge hilo halina uwezo wa kujadili masuala ya Jamhuri na ikiwa tofauti na hivyo, uhalali wa Bunge hilo upo wapi.

Profesa Ibrahim Lipumba, akizungumzia suala la mamlaka na madaraka ya Bunge hilo alilazimika kunukuu maneno ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, kuwa si suala la kawaida kwa Bunge hilo kunyang’anya madaraka ya wananchi, isipokuwa kuboresha maoni yao.

Baadaye alifuatia Ismail Aden Rage, ambaye awali alijinadi kuwa ni Rais wa Klabu ya Mpira ya Simba, alionekana wazi kumshambulia Profesa Lipumba kwa nukuu alizodai kuwa zimeandikwa kwenye gazeti la Mawio.

Lakini hata hivyo, Musa Haji Kombo alipopata nafasi ya kuuliza swali alimtetea Profesa Lipumba pale aliposema wasomi hutumia nukuu mbalimbali kujenga hoja ili kufikia uelewa na uamuzi mzuri wa hoja zinazobishaniwa.

Bila kumtaja kwa jina alisema, alichofanya Profesa Lipumba ni sahihi kabisa kufanywa na wataalam wengi na sio kama ambavyo wanafanya marais wa vilabu michezo katika uongozi wa timu zao na ndio maana hazina maendeleo.

Mapema akinukuu kifungu cha 9 (2) (a) hadi (i) kinachozungumzia misingi mikuu ya kitaifa na maadili, Jaji Werema, alisema wajumbe hawana mamlaka ya kujadili mambo hayo.

“Sheria imeweka mambo ya kufanya kwa wajumbe kwenye Rasimu ya Katiba hii yale yote mnayoyapenda lakini kuna mipaka…mna mamlaka lakini kuna mipaka, fanyeni mnachotaka, lakini hamuwezi kujadili kuhusu misingi mikuu ya kitaifa na maadili ya jamii kama ilivyo katika kifungu 9,” alisema.

Kwa mujibu wa kifungu hicho, mambo ambayo wajumbe hawaruhusiwi kuyabadili ni kuhusu kuwapo kwa Jamhuri ya Muungano, uwapo wa Serikali, Bunge na Mahakama, mfumo wa kiutawala wa kijamhuri na uwapo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Misingi mingine ambayo hawawezi kubadili ni umoja wa kitaifa, amani na utulivu, uchaguzi wa kidemokrasia wa mara kwa mara katika vipindi maalum kwa kuzingatia haki ya watu wote wenye sifa ya kupiga kura, ukuzaji na uhifadhi wa haki za binadamu, utu, usawa mbele ya sheria na mwenendo wa sheria na uwepo wa Jamhuri ya Muungano isiyofungamana na dini yo yote na inayoheshimu uhuru wa kuabudu.

Akijibu maswali na maoni ya wajumbe, Jaji Werema, alisema, Lissu alisema mamlaka ya Tume ya Warioba hayawezi kutumika katika Bunge hili.

Jaji Werema alitoa mfano wa jongoo ambaye ana miguu mingi, lakini yote inafanya kazi kwa ushirikiano na kumwezesha jongoo kutembea.

“Unaposoma sheria unapaswa kujua unasoma sheria kama  kitabu, kwa njia ambayo inaleta maana, lakini ukisoma sheria kama mstari mmoja wa Bibilia na kutoka nao utapotoka,” alisema.

Alisema misingi mikuu ya taifa imetajwa kwenye kifungu cha 9 (2) na imetumika kwa Tume ya Jaji Warioba na inatumika pia kwa Bunge hilo.

“Mimi nina viapo vinne na sijapotosha hata mara moja,” alisema bila kuvitaja.

Alisema kwenye kutafsiri sheria maneno yaliyomo pembeni kwa sheria (marginal notes), hayasaidii kitu chochote kama ambavyo Lissu alitumia maneno hayo kutoa maelezo yake bungeni. “Kama hali ndiyo hiyo, walimu wa sheria ongezeni bidii,” alisema.

Kuhusu ajenda ya Bunge Maalum, alisema ni Rasimu ya Katiba na siyo rasimu nyingine yoyote ambayo imetengenezwa pembeni, lakini hata hivyo, alisema kama mmoja anaweza kuipata basi asiipige teke, itamsaidia.

Kuhusu hoja iliyotolewa na Profesa Lipumba, alisema, Jaji Warioba hakukosea, ila inategemea mmoja anasoma kama mwanasiasa, mtaalum au mwanasheria.

Alisema maswali mengi ya wananchi ni kwamba wanataka au kuona sio sahihi kwa Bunge kufanya ukarabati wa rasimu hii, kwani wana nguvu ya kuifanyia mabadiliko rasimu hii.

Lakini ukweli ni kwamba bunge hilo halina mamlaka ya kuondoa misingi muhimu ya Katiba, ni kweli ipo katika kifungu cha 9.

Katika hatua nyingine, Jaji Werema aliwaomba wajumbe wavumiliane. “Naomba sana jamani tuvumiliane, wale wote tuliogombana zamani mimi nasema hadharani sasa nimeacha, tukubaliane kufanya kazi,” alisema.

Bunge limeahirishwa hadi Jumatatu, watakapoanza kujadili kanuni ambazo ziliwasilishwa jana bungeni na ofisa wa Bunge, Oscar Mtenda.

No comments:

Post a Comment