Tuesday, February 4, 2014

Mkakati mpya CHADEMA

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetangaza mkakati mpya wa kupiga kambi katika mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara kikidai wananchi wake wametelekezwa kwa makusudi na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mkakati huo utawashirikisha wabunge na makada wa chama hicho ili kuwaunganisha na kuwaamsha wananchi wa mikoa hiyo, kikidai kuwa wamesahaulika kimaendeleo.
Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, aliyasema hayo katika mikutano ya hitimisho ya ziara ya Operesheni M4C Pamoja Daima, ambayo ilifanyika mkoani Pwani, juzi.
Akiwahutubia wananchi wa mji wa Kibiti, Mbowe alionyesha kushangazwa na wananchi hao kuendelea kubaki maskini kwa miaka yote licha ya kuwa na rasilimali nyingi ikiwemo bahari ya Hindi.
Alisema CHADEMA haikutilia mkazo wa kisiasa katika mikoa hiyo kwa makusudi na badala yake iliwaachia wenzao wa Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kilitangulia kuweka nguvu na kuaminika katika mikoa hiyo.
Alisema baadhi ya mikoa hiyo imebaki nyuma sana katika sekta ya elimu, jambo ambalo alidai limefanywa makusudi na Serikali ya CCM kwa lengo la kuendelea kuwatumia wananchi kukipa ridhaa chama hicho kutawala miaka yote.
“Sasa nasema haki ya Mungu tunakuja kuweka kambi mara tu baada ya Bunge la Katiba kumalizika. Tutakuja na wabunge wetu wote, tutaweka kambi mkoa kwa mkoa, wilaya kwa wilaya, kata kwa kata, kijiji kwa kijiji mpaka kieleweke.
“Mmetumika sana kuibeba CCM kwa kupandikiziwa ukabila na udini, sasa ifike mwisho,” alisema.
Mbowe aliongeza kuwa Serikali ya CCM kwa makusudi imewafungia wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara kupata elimu kupitia mikutano ya kisiasa kwa mwaka mmoja sasa ikihofia wataamshwa kuhusu rasilimali zao wanazodai ziwanufaishe.
“Leo ni mwaka mmoja na siku kadhaa tangu Serikali ya CCM ilipofunga mikutano ya kisiasa kwa mikoa ya Lindi na Mtwara Januari 30, mwaka jana.
“Sisi tunaamini kwamba wananchi wa mikoa hii wamenyimwa fursa ya kupata elimu mbalimbali, ikiwemo ya rasilimali yao iliyowekwa na Mungu ndani ya ardhi yao,” aliongeza.
Alisema wananchi wengi wa mikoa hiyo wamejengewa hofu na woga na CCM jambo ambalo limewafanya wachukie wananchi wa mikoa mingine kwa kuwabagua kwa ukabila na udini.
“Mmenyimwa elimu bora kwa makusudi, na hii ndiyo imewafanya muwachukie makabila mengine wakiwemo Wachaga kwa sababu tu wameendelea kielimu, wanaume mmejengewa woga, mnatakiwa mjifunze kutoka kwao badala ya kuwachukia,” alionya.
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA (Zanzibar), Said Mohamed Issa, akihutubia mjini Kibaha juzi, aliwatahadharisha wananchi wa mikoa ya ukanda huo kutoendelea kutumiwa na CCM kupitia udini, dhana ambayo imewagawa kwa miaka yote tangu uhuru.
Akitoa mfano kwa wananchi wa mikoa hiyo walipoisaliti CUF wakati ina nguvu pande zote za Tanzania Bara na Visiwani wakikubali kupandikizwa chuki kuwa chama hiki ni cha Wapemba na Waislamu.
“Tuulizeni sisi Zanzibar, serikali yote inaongozwa na Waislamu kuanzia rais, makamu wake wawili, baraza la mawaziri na wawakilishi, lakini mpaka leo ninapohutubia hapa, wapo masheikh wako ndani kwa zaidi ya miaka miwili sasa, wamefungwa na hao Waislamu wenzao,” alisema.

No comments:

Post a Comment