Wednesday, February 5, 2014

CCM wawapiga CHADEMA

KIKOSI cha ulinzi cha Chama Cha Mapinduzi (CCM), wilayani Njombe, mkoani Iringa kimewashushia kipigo wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kumvunja taya mwanachama, Ally Kalonga.
Licha ya kushusha kipigo hicho, Mkuu wa Polisi wilayani Njombe, Lucy Mwakafirwa, amelaumiwa kuwakumbatia watuhumiwa makada wa CCM, huku akiwasweka ndani wanachama wa CHADEMA.
Akizungumza na Tanzania Daima jana kwa njia ya simu kutoka eneo la tukio, mwananchi ambaye hakupenda jina lake litajwe, alisema kikosi cha CCM cha ‘Green Guards’ kilitoa kipigo kwa wafuasi wa CHADEMA baada ya kubaini mpango wao wa kutaka kugawa fedha kwa wapiga kura utabainika.
CCM na CHADEMA wako katika kampeni za udiwani wa Kata ya Njombe Mjini unaotarajiwa kufanyika Februari 9,  sambamba na kata nyingine 27 nchini kote.
“Siku ya leo (jana) tulikuwa na mikutano ya kampeni za udiwani wa Kata ya Njombe Mjini, mikutano ilifanyika salama huku vyama vyote vikimaliza salama,” alisema.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo, baada ya kukamilika kwa kampeni hizo viongozi wa CCM wilayani hapo wakiongozwa na mbunge wa chama hicho (jina linahifadhiwa), walielekea katika Kijiji cha Matalawe.
Mwananchi huyo alisema baada ya kufika Matalawe, walikusanya baadhi ya wananchi na kuwaweka katika chumba kimoja na kuanza kugawa fedha.
“Baadhi ya Wana CHADEMA waliokuwepo pale, hawakupendezwa na jambo hilo, hivyo waliamua kupiga simu kwa viongozi wao kuwajulisha mchezo huo mchafu na viongozi hao walichukua gari kuja eneo hilo,” alisema.
Alisema kabla ya kufika walikutana na  kundi la vijana wa CCM waliokuwa wametanda barabarani.
Alisema vijana hao wa CCM waliwaamuru Wana CHADEMA hao wasimame, kisha walichomoa funguo za gari lao lililokuwa likiendeshwa na Ally Muhagama.
“Green Guards walisimamisha gari  la vijana wa CHADEMA, wakamnyang’anya funguo dereva, wakamshusha chini na kuanza kumpiga. Wakati wakiendelea kumpiga, ghafla alitokea mtu mmoja aliyevaa kiraia na kujitambulisha kuwa askari na kuomba wamuachie mtu huyo.
“Kutokana na kauli hiyo mbunge aliyekuwa na vijana wa CCM alimuomba raia huyo  atoe kitambulisho lakini hakuwa nacho, ndipo naye alipogeuziwa kibao na kuanza kupigwa na baadaye walifungiwa kwenye ofisi ya CCM ya eneo hilo,” alisema mtoa habari wetu.
Alisema vijana wa CHADEMA waliojificha baada ya kuona wenzao wakipata kipigo hicho walijaribu kukimbia lakini Green Guards waliwakamata na kuwapa kipigo huku mmoja wao akivunjwa taya na hali yake si nzuri.
“Hata hivyo wananchi walilazimika kupiga simu polisi ambapo walifika na kuwaamuru Wana CCM hao na mbunge wao wawatoe na kuelekea kituo cha polisi,” alisema.
Kwa mujibu wa mtoa habari wetu, wakiwa polisi, mbunge huyo na viongozi wa wilaya walifika kituoni na kwenda moja kwa moja katika ofisi ya OCD Mwakafirwa.
Mwananchi huyo alisema baada ya dakika chache ilitolewa amri ya kuwasweka ndani wanachama hao wa CHADEMA walioumizwa, huku baadhi yao wakiendelea kuvuja damu.
Gazeti hili lililazimika kumtafuta Mwakafirwa ambaye hakukubali wala kukataa kuwepo kwa vurugu hizo huku akimtaka mwandishi wa habari hizi kuwasiliana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Kamishna Msaidizi (ACP) Ramadhan Mungi, kwa taarifa zaidi.
Kwa upande wake Kamanda Mungi alisema hajapata taarifa kamili na kwamba anafuatilia kujua ukweli na undani wa tukio hilo.

No comments:

Post a Comment