Sunday, February 2, 2014

Mafuriko ya CHADEMA yaibomoa CCM

HARAKATI za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) za kujiimarisha, jana zilizidi kupata nguvu mpya baada ya vigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani kujiunga nacho.
Makada watatu wa CCM  akiwemo aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Kibaha Mjini mwaka 2010, Dk. Rose Nkonyi, wamejiunga na CHADEMA.
Makada hao walijiunga na CHADEMA jana na kukabidhiwa kadi na Mwenyekiti wa chama hicho ngazi ya taifa, Freeman Mbowe, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Mailimoja, ikiwa ni ziara ya Operesheni Movement  For Change (M4C) Pamoja Daima.
Waliojiunga na CHADEMA mbali na Dk. Nkonyi ni Joseph Chakale, aliyekuwa mjumbe wa  Kamati ya Utekelezaji CCM ngazi ya wilaya na Hafidh Mudhihiri aliyekuwa Katibu wa Vijana wa Tawi la Mailimoja.
Wakizungumza katika mkutano huo makada hao walisema wameamua kuihama CCM baada ya kubaini chama hicho hakina dhamira ya kuwaletea Watanzania maendeleo.
Waliongeza kuwa CCM hivi sasa imelemewa na tuhuma nyingi za ufisadi pamoja na  kutumia vibaya rasilimali za wananchi.
Walisema licha ya tuhuma hizo kukilemea chama hicho, viongozi wake wameshindwa kuchukua hatua zinazostahili, jambo linalochangia ugumu wa maisha kwa wananchi.
Mara baada ya kuzungumza, makada hao walikabidhiwa kadi za CHADEMA na Mbowe aliyewataka waendeleze harakati ili kuleta mabadiliko na ukombozi kwa Watanzania.
Mbowe aliwataka wananchi kuacha kumbeza mwanachama yeyote wa chama cha siasa anayejiunga na chama akipendacho, kwakuwa kila mmoja huwa ana sababu za msingi za kujiunga na chama kingine.
Mbowe pia aliwataka wananchi kuiunga mkono CHADEMA katika harakati za maandalizi ya Katiba Mpya na kusisitiza kuwa wanaunga mkono maoni ya rasimu ya Katiba mpya.
Slaa: CCM wameganda
Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, akiwa mkoani Mwanza alisema viongozi wa serikali ya CCM wana mawazo mgando ndiyo maana umaskini unazidi kushamiri.
Alisema kutokana na mawazo hayo mgando kila kukicha wamekuwa wakipandisha gharama za bidhaa mbalimbali ikiwemo umeme.
Alibainisha kuwa haoni sababu kwa serikali kupandisha bei za umeme wakati nchi ina rasilimali nyingi ambazo kama zingetumika ipasavyo fedha nyingi zingepatikana.
“Umeme si jambo la anasa kwa binadamu, kwetu linaonekana ni anasa…..nishati hii ilitakiwa kutolewa kwa gharama nafuu, viongozi wa CCM wana mawazo mgando” alisema.
Alisema mawazo mgando ya viongozi ndiyo yamekuwa yakirudisha nyuma jitihada za maendeleo ya wananchi huku wananchi wakibaki kuwa watazamaji wa rasilimali zao badala ya wanufaikaji.
Dk. Slaa alisema serikali imeshindwa kuendeleza vipaji vya vijana licha ya kuwatumia  kujipatia kura kila zinapofika nyakati za uchaguzi.
Alisema kuwa CHADEMA itaendelea kuhakikisha daftari la wapiga kura linaboreshwa, huku akiwataka Watanzania wakatae kuandikishwa na mabalozi wa nyumba kumi ambao ni wa CCM.
Alisema kazi hiyo ni lazima ifanywe na watendaji wa serikali kwa mujibu wa sheria za nchi na si mabalozi hao ambao ni makada wa CCM.
“Mkiwaruhusu mabalozi wawaandikishe  mjue ni lazima udanganyifu utakuwepo kwa kiwango kikubwa, hapa mtakosa haki ya kupiga kura,” alisema.
Alisema CCM wanataka kuitumia fursa hiyo kuwanyima watu haki ya kuwachagua viongozi wanaowapenda, hasa katika kipindi hiki ambacho upinzani una nguvu.
Aliwataka Watanzania wajitokeze kwa wingi katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu ili wachague viongozi wanaowataka.
Dk. Slaa pia amewataka wananchi wawe makini katika maamuzi yao ili viongozi watakaowachagua wawasaidie kuliendeleza gurudumu la maendeleo yao.
Alisema mwaka 2015 nchi inahitaji kupatikana kwa viongozi bora, wawajibikaji zaidi, tofauti na hawa wa CCM wanaoendekeza matumbo yao na jamaa walio karibu nao.
Aliwataka viongozi wa CHADEMA kuhakikisha wanakuwa wabunifu katika harakati za mapambano ya uchaguzi wa mwaka 2015.
Kuhusu madini yanayopatikana hapa, jambo hilo bado limeonekana ni balaa au hasara kwa Watanzania ambao hawanufaiki kama walivyo wageni.
Amesema kuwa kama serikali ingekuwa makini, ingekuwa na viwanda vya kuchakata madini ambavyo vingetoa ajira kwa vijana na kukuza pato la taifa.
“Fedha zote zinapelekwa nje ya nchi, tukiingia madarakani tutatumia vizuri madini kwa manufaa ya watu wote,” alisema.
Alisema CHADEMA wanajua mahitaji ya wananchi na vijana ambao wana tatizo kubwa la ajira.
Alibainisha kuwa CHADEMA inataka kuona vijana wanapata fursa za ajira zitakazowasaidia kuondoa umaskini walionao.
Serikali ifufue viwanda vya nguo ili kuleta nafuu kwa wakulima ambao wanalima pamba na malighafi mbalimbali.
Alibainisha kuwa uwepo wa viwanda hivyo vitasaidia pamba inayozalishwaji nchini kupata soko la uhakika.
Aliwataka wabunge wa Bunge la Katiba wakiingia kwenye Bunge hilo watumie busara na hekima katika majadiliano ili Tanzania iwe na Katiba bora na imara.
“Hatuhitaji katiba yenye viraka viraka au milengo ya kisiasa, walete Katiba yenye kujali matakwa ya wananchi waliowapa fursa ya kuingia bungeni,” alisema.

No comments:

Post a Comment