MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ina mfumo wa kirafiki katika utawala wenye utitiri wa viongozi unaogharimu taifa mamilioni ya fedha.
Akihutubia mamia ya wakazi wa Chalinze juzi, Mbowe alisema utitiri huo wa viongozi unatokana na watawala kulipa fadhila kwa wapambe wao.
Kwa mujibu wa Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, serikali ya CCM itaendelea kuiingizia deni nchi yetu kwa bajeti ya kugharimia serikali iliyojaa viongozi wasio na kazi wakiwemo wakuu wa wilaya na mikoa.
“Hata upatikanaji wake inategemea siku hiyo rais ameamkaje na familia yake kama nyota imekuangazia basi taarifa ya habari ya saa saba unashangaa unatangazwa mkuu wa wilaya au mkoa fulani…
“Haijalishi una elimu ya utawala, unazifahamu mila na desturi au mazingira, ndiyo maana kila kona ya nchi hii kuna migogoro isiyo na ufumbuzi.
“Serikali ya CHADEMA haitakuwa na rundo la viongozi, badala yake viongozi watachaguliwa na kuwajibishwa moja kwa moja na waliomchagua ikiwemo kuongeza nidhamu ya uwajibikaji na haki za binadamu kutekelezwa kikamilifu, si kumwogopa na kumsujudia mtu,” alisisitiza.
Akizungumzia hali ya kisiasa nchini, Mbowe alisema baada ya ziara ya siku 12 nchi nzima amegundua CCM wamechoka na wananchi wanasubiri kwa hali na mali kuidhalilisha kwa kuiangusha kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
“Nawaonya polisi, uchaguzi wa 2015 ni Manchester na Arsenal, kaeni pembeni tuacheni tuwaonyeshe anguko la mtu mzima… tumejipanga, tunajiamini na tuna uhakiaka 2015 serikali ya CHADEMA itaingia mzigoni,” alisema.
Alisema bila aibu serikali ya CCM imetumia njia mbalimbali kudhoofisha nguvu ya CHADEMA bila kujua kuwa chama hicho hakipo kwa mipango ya watu bali mpango wa Mungu.
“Juzi tulipandikizwa mgogoro eti tusielewane. CHADEMA ni mpango wa Mungu mzee… wanasahau kuwa leo CHADEMA ni kimbilio la wapenda haki, amani na utulivu, maana leo wapo waliotoka, wataendelea kuja kutoka vyama mbalimbali, vikiwemo vikubwa kama CUF, CCM, TLP na vidogo,” alisema.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai alisema Watanzania sasa wanalia nchi nzima wakitaka mageuzi baada ya kuchoshwa na utawala dhalimu wa CCM uliojaa vichocheo vya udini na ukabila bila haya.
Alisema nchi imejaa migogoro na harufu ya damu za watu na hakuna hatua zinazochukuliwa na serikali dhidi ya hali mbaya kama hiyo.
mbona chama chenu hamkisemi kilivo na mfumo wa kibepari . .
ReplyDeleteni kweli ndilo tatizo la ccm kulindana kumezidi ndani ya ccm,kwa msingi huo nchi itabakia hapa hapa ilipo,hongera MHESHIMIWA MBOWE
ReplyDelete