Na Bryceson Mathias
SERIKALI imetangaza majina 201 ya wajumbe kutoka makundi mbalimbali nchini walioomba kuteuliwa ili waungane na wabunge wa Bunge la Jamhuri na la Wawakilishi Zanzibar waliopo, kuingia kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
Kabla ya kutangaza majina hayo kwa niaba ya Rais Jakaya Kikwete, Kaimu Katibu Mkuu Kiongozi, Dk. Florence Turuka, alisema kazi ya kuwapata wajumbe wa Bunge hilo ilikuwa ngumu kwani walioomba walikuwa 3,754 na waliotoswa 3,553.
Hadi sasa, Rais Jakaya Kikwete ameshanawa mikono kama Pilato, na sasa analala usingizi mnono, akiwatazama wajumbe aliowatupia Zigo ili wajadili mustakabali wa Kiuchumi, Kisiasa na Kiutamaduni wa nchi hii; Hivyo wakibolonga; Hukumu iko kwao si Rais Kikwete.
Kwa msingi huo huo, Mosi; hatutarajii tuone tena kuna watu wanasinzia na kulala usingizi katika Bunge hili Maalum kama tulivyowaona wabunge fulani wakubwa kwa nyadhifa zao, wakipiga usingizi hadi wakafikia kukoroma.
Pili; lakini muhimu. Hatutaki kuona tena, Usingizi huu wa, ‘Sasa nitawauliza; Wanaoafiki waseme ndiyo. Utasikia wengi wenye Chama chao wakikurupuka usingizini na kujibu Ndiyooooooooooooooooo. wasioafiki wasemasiyo’….Hatutaki! tunataka kama hakuna maafikiano, ‘zipigwe kura za siri’!.
Pamoja na Wabunge wa Bunge la Muungano na Wawakilishi wa Zanzibar, lakini Macho na Masikio ya watanzania nikiwemo mimi, kwa sehemu kubwa sana tunawaangali na kuwategemea wajumbe 201 toka makundi mbalimbali, walioteuliwa ili wawe mawakili wetu watusemee.
Walioteuliwa ni kutoka taasisi zisizokuwa za kiserikali, taasisi za kidini Tanzania Bara, Kundi la vyama vya siasa, taasisi za elimu, watu wenye ulemavu, vyama vya wafanyakazi, vyama vya wafugaji, vyama vya wavuvi, vyama vya wakulima na watu wenye malengo yanayofanana.
Kama kati ya watanzania Mil. 50, wajumbe hao 201 wameoteuliwa; Ni Matarajio yangu watathamini uteuzi huo, na hivyo katika Mjadala huo wa Rasimu ya Pili ya Katiba, watajikiti kuangalia mustabali na uzalendo wa Taifa hili; ili waandike Historia ya muhimu maishani mwao.
Naamini wajumbe hao watatamani kuandika Historia za maisha yao ili waje wakumbukwe na vizazi vya miaka 50 ijayo ambapo vizazi hivyo vitasoma, vitasikia, na kushuhudia Katiba nzuri, wakiwapongeza kuwa walifanya kazi nzuri na kusujudu makaburi yao badala ya kuwalaumu.
Lakini kama wajumbe hao watajadili Usingizi wa Itikadi zao, Dini zao, Maslahi ya Uongozi wa watu fulani binafsi, Ukanda, Ukabila bila kujali Utaifa; Vizazi vijavyo vitawalaumu kwa kutengeneza Katiba Mbovu, na watathubutu kutandika Bakora makaburi yao.
Tunawaonya wajumbe waliochaguliwa, wasiwe watu watakaokwenda na mawazo waliyofundishwa kwa Kitu kidogoau Takrima, ili Katiba hiyo isipatikane kwa Lengo la mwanya wa kusema, Wajumbe wameshindwa kuleta Katiba mpya, hivyo tuirudie ya awali.
Kutopatikana kwa Katiba Mpya, kutasababisha msuguano mkubwa miongoni mwa jamii nchini Tanzania, kwa sababu iliyopo imeonesha mapungufu makubwa ambayo, kwa namna moja au nyingine, imekuwa ikiwanyima haki wananchi na hasa wapiga kura.
Ni rai yangu wajumbe wafahamu kwamba, waiingie mjengoni wakijua kuwa, kama watafanya madudu yasiyotarajiwa kutupatia Katiba Mpya, waelewe wananchi bado tuna Dume na Jike la Karata (Kura ya Maoni), ambapo tutapiga kura ya kuikataa.
Aidha ni onyo letu kwa vyombo vya dola, visithubutu kufanya Uumini na ushiriki wao wa kukiegemea Chama Tawala kiasi cha kusababisha vurugu ambazo tumekuwa tukizishuhudia katika Mabunge yaliyopita.
No comments:
Post a Comment