Thursday, February 13, 2014

CHADEMA yambana JK

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeitaka serikali ya Rais Jakaya Kikwete kutoa majibu ya maswali yaliyoulizwa na mwandishi wa gazeti la Daily Mail la nchini Uingereza kwa vielelezo, badala ya kulalamika kuwa tuhuma hizo zina lengo la kuichafua nchi.
Wakati CHADEMA ikiwa na msimamo huo Umoja wa Wabunge wa Kuhifadhi Mazingira ya Ulinzi wa Tembo na Faru, umetaka uchunguzi ufanywe dhidi ya watu wanaodaiwa kuwa karibu na mamlaka za serikali huku wanatuhumiwa kujihusisha na ujangili ili kubaini ukweli.
Msimamo wa CHADEMA ulitolewa jana jijini Dar es Saalaam na Waziri Kivuli wa Maliasili na Utalii, Mchungaji Peter Msigwa wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Msigwa alisema baada ya gazeti la Daily Mail  la nchini Uingereza kuripoti ugumu wa kukabiliana na ujangili nchini kutokana na wahusika kuwa karibu na mamlaka ya serikali, Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalaundu, alisema tuhuma hizo zimelenga kuichafua Tanzania.
“Waziri Nyalandu anasahau kuwa Tanzania imeshajichafua katika Jumuiya za Kimataifa baada ya kushindwa kulinda rasilimali zake kutokana na matendo ya ujangili yanayoshika kasi kila siku.
“Nyalandu atuambie amechukua hatua gani kuwalinda wanyama hao wakiwa hai zaidi ya kukamata pembe za ndovu na faru waliokufa?.. je, hakuona taarifa iliyorushwa na kituo cha ITV cha Uingereza namna wachunguzi wao walivyo rekodi namna pembe hizo zinavyopatikana na watu wanaohusika?” alihoji Mchungaji Msigwa.
Alisema pamoja na serikali kuona jambo hilo ni dogo, lakini wanasahau kuwa Jumuiya ya Kimataifa ipo makini katika kulinda viumbe hai vilivyo katika hatari ya kupotea.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge wa Kuwalinda Tembo na Faru,  Dk. Athuman  Mfutakamba, ambaye aliongea muda mfupi baada ya Msigwa kukutana na waandishi wa habari, alisema licha ya kutaka uchunguzi lakini pia wanalaani upotoshaji uliofanywa na gazeti hilo kwa lengo la kuichafua Tanzania.
Kauli hiyo ilitokana na swali kutoka kwa mwandishi wa gazeti hili aliyetaka kujua kama umoja wao una lengo la kutaka uchunguzi ufanyike juu ya tuhuma hizo na kwanini wasiiachie Ikulu ijisemee juu ya watu wanaodaiwa kuwa karibu na Rais Kikwete kujihusisha na ujangili.
Akijibu swali hilo alisema wao kama walinda mazingira na watetezi wa faru na tembo, wangependa uchunguzi ufanyike na wahusika wajulikane badala ya tuhuma za upande mmoja kufanyiwa kazi na kusambazwa kwa jamii.
“Tumeshtushwa na gazeti moja la kihafidhina la Uingereza lililochapishwa Februari nane na tisa likimshutumu Rais Kikwete kwamba ameshindwa kutimiza wajibu wake wa kuwalinda tembo na faru,” alisema Dk. Mfutakamba.
Miongoni mwa tuhuma zilizotolewa na gazeti la Daily Mail ambazo Mchungaji Msigwa anataka zijibiwe kwa vielelezo badala ya kauli ni juu ya watu walio karibu na Rais Kikwete wanaohusika katika biashara haramu ya meno ya tembo, lakini hawachukuliwi hatua.
Tuhuma nyingine ni kuwa ndege iliyomleta Rais wa China mwaka jana iliondoka na shehena ya pembe za ndovu ambayo ilipakiwa na maofisa waliokuwa kwenye ndege hiyo.
Tuhuma nyingine za gazeti hilo ambalo lilimnukuu Msigwa ni kwamba CCM na serikali yake ni wanufaika  wa mradi wa ujangili kwa lengo la kutafuta fedha ya uchaguzi ujao na kwamba ujangili umeongezeka zaidi katika kipindi cha utawala wa Rais Kikwete.
JK atoa kauli nzito
Katika hatua nyingine, Rais Jakaya Kikwete amesema kuwa hataruhusu shehena za pembe za ndovu zilizokamatwa katika matukio mbalimbali ya kupambana na ujangili, kuuzwa  kwani bora shehena hiyo ichomwe moto.
Pia alisema anakwenda nchini London, Uingereza kuwaomba wasaidie kuvunja mtandao wa masoko makubwa ya biashara ya meno ya tembo na  faru yaliyoshamiri katika nchi za mataifa makubwa.
Rais Kikwete alisema hayo juzi usiku katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa  Mwalimu Julius Nyerere akiwa safarini kuelekea nchini London, Uingereza kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya kukomesha biashara ya meno ya tembo na faru na mauaji yake.
Rais pia alitaja masoko makubwa ya meno ya tembo kuwa ni pamoja na Thailand, Vietnam na China na kuongeza kwamba endapo masoko hayo yatafungwa, basi Tanzania na nchi nyingine mauaji ya wanyama hao hayatakuwepo.
Akizungumzia kuhusu kutoruhusu uuzaji wa shehena ya meno ya tembo  iliyokamatwa kwenye operesheni mbalimbali nchini, Rais Kikwete alisema hataruhusu kuyauza na kama hayatakuwa na kazi nyingine ya kufanya ni bora yachomwe moto.
“Kamwe sitatoa  kibali cha kuuza pembe za ndovu na faru ili kusaidia kudhibiti ujangili ambao chanzo chake kikubwa ni kuwepo kwa soko kubwa  la bidhaa hiyo duniani,” alisema Rais Kikwete.
Hata hivyo alisema kuwa katika kipindi cha miaka ya nyuma Tanzania ilipiga hatua ya kupambana na ujangili lakini mafanikio hayo yaliharibiwa baada
ya kurudi tena  kwa biashara ya meno ya tembo katika mataifa makubwa ya nje.
Alisema katika kipindi cha miaka ya 1970 hadi 1980 mara baada ya nchi kupata uhuru mwaka 1961, kulikuwa na tembo zaidi ya 350,000 lakini waliuawa wote na kubakia 50,000.
Aliendelea kueleza kuwa katika kipindi cha mwaka 1989, serikali  iliingiza jeshi katika Operesheni Uhai na kuweka mikakati mbalimbali ya kupambana na ujangili ndipo mafanikio yalianza kuonekana.
Akizungumzia kwa upande wa faru, alisema mwaka 1989 walibaki wawili katika Hifadhi ya Serengeti ambao walikuwa jike, na baadaye aliingia faru dume  kutoka Ruaha, kuanza kuzaliana hadi wakafikia 32 na kuweka historia.
Rais Kikwete pia alizindua mabango yanayohamasisha kuacha mauaji ya tembo na faru yatakayoenezwa sehemu mbalimbali ya nchini ambayo yapo chini ya usimamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii.
Awali akizungumza kabla ya kuzinduliwa kwa mabango hayo, Naibu  Waziri wa  Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa, alisema lengo la mabango hayo ni kutaka kuwahamasisha wananchi kushiriki katika harakati za kupambana na ujangili.

No comments:

Post a Comment