Friday, February 14, 2014

KAMATI KUU YA CHADEMA KUKUTANA KWA DHARURA



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

KAMATI KUU YA CHADEMA KUKUTANA KWA DHARURA
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) itakutana kwa ajili ya kikao cha dharura, Februari 14, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Katika kikao hicho, Kamati Kuu itajadili na kufanya uteuzi wa mwisho wa jina la mgombea ubunge wa CHADEMA katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga, mkoani Iringa, unaotarajiwa kufanyika Machi 16, mwaka huu.

Kikao hicho kitafanya uteuzi wa mwisho, baada ya mchakato wa ndani wa kumpata mgombea ubunge wa Jimbo la Kalenga kwa tiketi ya CHADEMA, kuwa umepitia hatua za awali, ambazo ni pamoja na watu wote wenye nia ya kugombea, kuchukua fomu za uteuzi wa ndani tangu Februari 5-10, mwaka huu.

Kama ilivyoelezwa kwa umma kupitia vyombo vya habari, Februari 6, mwaka huu, fomu hizo zilitolewa katika maeneo matatu, Ofisi za Makao Makuu ya Chama, Dar es Salaam, Ofisi za Jimbo la Kalenga na kwenye tovuti ya chama, ambayo ni; www.chadema.or.tz.

Jumla ya watu 16 waliweza kuchukua fomu za kuwania uteuzi huo, ambapo hadi siku ya mwisho, watu 13 waliweza kurejesha fomu zao na kupita kwenye mchakato wa kura za maoni, zilizofanyika Februari 12, mwaka huu.
Imetolewa leo Februari 13, 2014, Dar es Salaam na;
Tumaini Makene
Ofisa Mwandamizi wa Habari- CHADEMA

No comments:

Post a Comment