Saturday, February 1, 2014

Chadema wapambana na polisi Musoma

Polisi mjini Musoma wametumia mabomu ya machozi kudhibiti ghasia zilizoibuka, baada ya wafuasi wa Chadema kupambana na mbunge wa zamani wa Musoma Mjini, Vedastus Mathayo.

Walifanya fujo juzi jioni baada ya mjumbe huyo wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kudaiwa kuingilia safari ya Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Willbroad Slaa ya kwenda kwenye msiba wa Sheikh wa Mkoa wa Mara Athumani Mageyee.

Kiongozi huyo alikwenda kuhani msiba wa Sheikh huyo aliyefariki wiki hii.
Hata hivyo, kabla ya kufika msibani, Mathayo alijitokeza kuelekea nyumbani kwa Sheikh huyo na kuwalazimisha wafuasi wa Chadema waliokuwa wameusindikiza msafara wa Dk. Slaa, kupanga mawe barabarani kumtaka asubiri.

Wakizungumza kwa jazba wakiwa wanapanga mawe hayo, walisema mbunge huyo wa zamani ni mwenyeji wa Musoma lakini tangu msiba utokee hajawahi kuhani lakini alipoona viongozi wa Chadema wanakwenda naye akajitokeza.

“Tunashangaa huyu Mathayo kuja kwenye msiba baada ya kuona viongozi wa Chadema wanakwenda wakati yeye ni mwenyeji na hajawahi kukanyaga, sisi tunaamini hakuwa na lengo zuri na ndiyo tukamzuia,” alisema Jacob Mwita.

Ghasia hizo zilisababia polisi kulifika eneo la vurumai na kuwatawanya kwa kupiga mabomu ya machozi, hali hiyo ilidumu kwa muda wa nusu saa na kusababisha baadhi ya wafuasi wa Chadema kuwashambulia polisi.

Kufuatia hali hiyo, Mbunge wa sasa wa Jimbo hilo, Vincent Nyerere , alilazimika kuingilia kati kuwatuliza wafuasi wa Chadema waliokuwa wanaendelea kupambana na polisi.

Kwa upande wao, wanafamilia wa marehemu walisikika wakizungumza kwa jazba kutokana na kutoridhishwa na kitendo cha mbunge huyo wa zamani wa CCM.
Wakiongeza kwa hasira walisema kuwa inawezekana Mathayo alienda msibani baada ya kusikia Dk. Slaa amekwenda kuhani.

“Mathayo amekuja kufanya nini leo wakati tangu msiba utokee hajawahi kufika hapa eti leo kaona watu wametoka mbali wanakuja kutuhani naye ndiyo anakuja kama siyo fujo ni nini wakati sisi tuna majonzi,” alisikika akisema mmoja wa wanafamilia.

Aidha Dk. Slaa katika hotuba yake na wananchi wa Musoma, aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), itamke wazi kuhusu kiasi cha fedha ambacho kimetengwa kwa ajili ya kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura.

Pia aliitaka ieleze ratiba ya kuanza kuboresha daftari hilo ili wananchi waweze kuelewa

“Hatutaki kuuziwa mbuzi kwenye gunia tunataka iwaambie Watanzania ni kiasi gani cha fedha kimetengwa, lini zoezi litaanza na katika kanda zipi kwa sababu kabla ya hapo tuliambiwa ilikuwa imepewa fedha kidogo za kuboresha daftari hilo.”

No comments:

Post a Comment