Saturday, February 1, 2014

Dr. Slaa arusha kombora

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimefichua siri kwamba Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imeanza kuuza baadhi ya viwanda vya umma kwa wake za marais na wabunge wa chama hicho.

Kimesema kuwa kuuzwa kwa viwanda hivyo vilivyokuwa nguzo muhimu ya uchumi wa taifa, ni dhamira mbaya ya serikali kuendeleza unyonyaji wa jasho la Watanzania maskini, na kwamba katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, CHADEMA kupitia nguvu ya umma itakiangusha chama hicho tawala.

Kana kwamba hiyo haitoshi, CHADEMA imeishtaki serikali kwa wananchi kwa madai kuwa imewalipa wazee wastaafu hundi ya sh milioni tatu na kusema hayo ni matusi makubwa kwa Watanzania yasiyovumilika, hivyo lazima wananchi waonyeshe kukasirishwa na vitendo hivyo kwa kuinyima kura CCM 2015.

Shutuma hizo zimetolewa juzi na Katibu Mkuu wa CHADEMA Taifa, Dk. Willibrod Slaa, wakati akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Mukendo mjini Musoma mkoani Mara, ikiwa ni mwendelezo wa mikutano ya Operesheni M4C Pamoja Daima.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na Mbunge wa Viti Maalumu Tarime, Ester Matiko, Mbunge wa Musoma mjini, Vincent Nyerere, viongozi na makada wa CHADEMA ndani na nje ya Mkoa wa Mara, Dk. Slaa alilazimishwa na wananchi kumpandisha jukwaani mbunge Nyerere kwa madai kwamba ndie rais wa Musoma.

Dk. Slaa aliyekuwa akikatishwa mara kwa mara hotuba yake kwa sauti za watu waliokuwa wakimuita Rais wa Watanzania, alimtaja mke wa Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, Mama Anna Mkapa, kwamba ameuziwa kiwanda cha korosho.

Mbali na mke wa Mkapa, Dk. Slaa ambaye alitua kwenye viwanja hivyo vya Mukendo akiwa na chopa akitokea Kata ya Nyasura wilayani Bunda, alimtaja Mbunge wa Singida mjini, Mohammed Dewji (CCM), kwamba amenufaika kwa kuuziwa kiwanda cha nguo cha Mutex cha Musoma.

“Serikali ya CCM sasa imeamua kuwauzia wabunge wa CCM viwanda vyetu vya umma. Hapa Musoma kiwanda cha Mutex ameuziwa Mohammed Dewji na Mama Mkapa naye ameuziwa kiwanda cha korosho.

“Watanzania wanalia na umaskini, wanalia kwa kukosa huduma bora za afya, maji na elimu, wanalia kwa kunyanyaswa na kuteswa, leo hii Serikali ya CCM imeanza kuuza viwanda vya umma kwa kujuana.

“Yupo mtu mwingine alinunua kiwanda baadaye akapelekwa mahakamani, anakana mahakamani hajanunua. Anasema aliyenunua yupo Uarabuni. Ameambiwa na mahakama amlete aliyenunua ameshindwa kumleta.

“Kwa matatizo na mateso wanayofanyiwa wananchi na Serikali yao ya CCM, CHADEMA tunasema mwaka 2015 CCM tutaiangusha asuhuhi tu. CCM haipo tena… na sisi CHADEMA tukishika nchi, tutawafuta machozi Watanzania kwa kuwatumikia vizuri kwa uadilifu wa hali ya juu, naombeni mtuunge mkono,” alisema Dk. Slaa huku akishangiliwa.

Alisema serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi kwa mambo ya anasa ambazo zimemfanya asihudhurie sherehe mbalimbali zikiwemo za Uhuru na nyinginezo ambazo zinatumika kifisadi kufilisi fedha za umma.

Dk. Slaa aliishutumu Ikulu kwa kuwaalika na kuwalipia tiketi za ndege, baadhi ya marais kutoka nchi za nje kuja na kurudi nchini wakati marais hao wamegharimiwa na serikali zao.

“Serikali ya CCM imeshindwa kuboresha huduma za kijamii kwa kisingizio kwamba haina pesa. Lakini inaalika marais kutoka nchi za nje kuja na kurudi Tanzania na inawalipia tiketi za ndege wakati viongozi hao wamegharimiwa na serikali zao. Huu ni ufisadi mkubwa. Watu wanakusanya na kuweka vyao mapema mifukoni,” alisema.

No comments:

Post a Comment