KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk Willibrod Slaa, amemtaka Rais Jakaya Kikwete kumwondoa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP), Eliezer Feleshi, kutokana na kuidhalilisha serikali kwa kufungua kesi za kufikirika.
Dk. Slaa alitoa kauli hiyo juzi kwa nyakati tofauti wakati akihutubia mamia ya wananchi wa Wilaya ya Maswa, mkoani Simiyu katika Uwanja wa Nguzo Nane mjini Nyalikungu na Malampaka katika mikutano ya hadhara ikiwa ni sehemu ya Operesheni M4C Pamoja Daima.
Alisema kesi ambayo imemalizika hivi karibuni ya uchochezi dhidi ya waandishi wa habari watatu na kuwaachia huru baada ya serikali kushindwa kuthibitisha makosa yao, ni udhaifu wa DPP na matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi.
“Nafikiri mmesikia katika vyombo vya habari kuwa mahakama imewaachia huru waandishi wa habari watatu waliofunguliwa kesi ya uchochezi dhidi ya askari kutowatii viongozi wao, cha kushangaza serikali yenye Mwanasheria Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka nchini, lakini inapeleka kesi ambayo haina kichwa wala miguu, sasa wameumbuka mahakamani,” alisema Dk. Slaa huku akishangiliwa na wananchi.
Alisema hakuna dhambi yoyote kuwaeleza ukweli askari polisi na kuhoji kuna dhambi gani kumweleza kuwa mshahara wake ni mdogo au kuwaeleza hawana nyumba nzuri za kuishi hata kambi nyingine hawana vyoo wanajisaidia kwa majirani.
“Wananchi hivi kuna dhambi gani kuwaeleza askari polisi kuwa mishahara yao ni midogo? Hawa askari ukiwatembelea katika makazi yao wanayoishi huko makambini utashangaa hawana nyumba nzuri na wengine hata vyoo hawana hadi vya kutafuta kwa majirani, ukisema hali halisi unaelezwa kuwa ni uchochezi ni jambo la kushangaza,” alisema.
Alisema kuwa ni wazi serikali haikupeleka kesi hiyo mahakamani kwa nia njema, na lengo lilikuwa kuwakomoa wanahabari na kuwanyima wananchi haki yao ya msingi ya kupata habari.
Hivi karibuni Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwaachia huru Mhariri Mtendaji wa New Habari, Absalom Kibanda, Meneja Uendeshaji Biashara wa Kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL), Theophil Makunga na Samson Mwigamba, mwandishi wa makala iliyodaiwa ya uchochezi dhidi ya askari.
No comments:
Post a Comment