Thursday, January 16, 2014

Vyama vya siasa vyataka mwafaka wa Katiba Mpya

Vyama vya siasa vimekubaliana kutafuta mwafaka wa agenda za Katiba Mpya kabla ya kuanza kwa Bunge la Katiba.
Kutokana na makubaliano hayo, vimekubaliana kuwasilisha mapendekezo yao kwenye Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), ili kuratibiwa kabla ya kuanza kwa Bunge hilo.
Vyama hivyo vimetakiwa kuwasilisha maoni ili yachambuliwe na kutolewa maoni ya pamoja yatakayotumika kwenye Bunge Maalumu la Katiba.
Baadhi ya vyama vimeonyesha wazi kutofautiana na Rasimu ya Katiba iliyotolewa hivi karibuni na Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Chama tawala, CCM kinatofautiana na vingine juu ya mfumo wa Muungano kikitaka Serikali mbili wakati vingine vikikubaliana na maoni ya Tume ya Serikali tatu.
Bunge la Katiba limepangwa kuanza Februari, mwaka huu na litakuwa na wajumbe 640, huku 42 wakitokea katika vyama hivyo vya siasa, kila chama kikitoa wajumbe wawili.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa majadiliano ya viongozi wa vyama hivyo, Mwenyekiti wa TCD, James Mbatia alisema: “Tumekubaliana kuwa mpaka Januari 31, mwaka huu kila chama kiwe kimewasilisha maoni yake kuhusu rasimu ya Katiba.
“Kuanzia Februari 8 hadi 14, mwaka huu Kamati ya mashauriano itayapitia maoni yote ya vyama ili kama kuna tofauti ziweze kujadiliwa. Tunataka tuwe na mawazo yanayofanana ndani ya Bunge la Katiba kwa sababu Katiba Mpya ni muhimu kuliko itikadi za vyama vyetu, nchi kwanza vyama baadaye.”
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula na Katibu Mkuu wake, Abdulrahman Kinana ambao walikuwapo katika mkutano huo, walikataa kutolea ufafanuzi msimamo wa chama hicho kuhusu mapendekezo yaliyomo katika rasimu hiyo.
“Kila kitu amezungumza msemaji wetu Mbatia, sasa mimi mnataka niseme nini siwezi kuzungumza tofauti na makubaliano ya kikao chetu cha leo (jana),” alisema Mangula.
Katika ufafanuzi wake, Mbatia alisema kama vyama hivyo vitaingia katika Bunge hilo na kuanza kupingana ni wazi kuwa vitawachanganya wananchi: “Kuna vyama vinataka Serikali mbili vingine tatu na vingine moja, nadhani tutakubaliana na hata ikishindikana basi tuwe na aina ya uwasilishaji ambayo haitaleta mvutano bungeni.”
Mbatia pia aligusia suala la maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapigakura… “Tumeiomba Serikali kuipatia fedha Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ili iweze kuliboresha daftari hilo, tunataka liwe limefanyiwa maboresho katika upigaji wa kura ya maoni Mei mwaka huu.”
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema lengo la kukutana ni kutaka kuweka msimamo wa pamoja kwa maslahi ya taifa.

Viongozi wengine wa vyama walioshiriki mkutano huo ni Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba na Naibu Katibu Mkuu wake, Julius Mtatiro, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Tundu Lissu.

No comments:

Post a Comment