Thursday, January 16, 2014

Halima Mdee amtaka Prof. Tibaijuka ajiuzulu

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ametakiwa kujiuzulu kutokana na kuonyesha kupwaya katika nafasi yake na kushindwa kutatua mgogoro wa ardhi wa shamba la Kapunga, wilayani Mbarali, mkoani Mbeya.
Wiki iliyopita Profesa Tibaijuka alidaiwa kuzomewa baada ya kuingia ndani ya gari la mkuu wa wilaya na kufanya mazungumzo na mwekezaji aliyekuwepo katika mgogoro na wananchi wanaogombania eneo la kijiji chao, kisha aliposhuka akabadili msimamo wa awali wa kutetea haki na stahili za wanakijiji hao na kugeuka kuanza kumtetea mwekezaji hapo hapo.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Waziri Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Halima Mdee, alisema kushindwa kutatuliwa kwa mgogoro huo uliodumu kwa miaka mingi sasa ni mwendelezo wa kushindwa kwa serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kusimamia suala nyeti la ardhi na kudhihirisha kuwa Profesa Tibaijuka amepwaya katika nafasi yake, hivyo hana budi kujiondoa.
Mdee alisema kuzomewa kwa waziri huyo ni wazi kuwa mgogoro huo bado unafukuta na unaonekana kuigharimu serikali ya CCM, pia imemjengea taswira mbaya ya kisiasa Profesa Tibaijuka.
Alisema Watanzania kutokana na migogoro ya ardhi ilipofikia anahitaji mtu makini kwenye wizara hiyo ambaye anaweza kusema na kutenda bila kuonekana akifanya vitendo vya gizani kama ilivyotokea hivi karibuni huko Kapunga.
“Tunataka Waziri Tibaijuka awaambie Watanzania, mawaziri wanaoshindwa kama yeye chini ya serikali isiyowajibika kutatua matatizo ya wananchi wanataka yatokee maafa makubwa kiasi gani ili wajue kuwa migogoro ya ardhi inaweza kulitumbukiza taifa kwenye sintofahamu?,” alihoji.
Mdee alimtaka Profesa Tibaijuka kuacha kuanzisha jambo jipya katika mgogoro huo ambapo itakuwa ni kinyume cha kauli ya serikali hiyo hiyo iliyowahi kutolewa bungeni juu ya kushughulikia suala hilo.
Alisema kuwa serikali kupitia kwa Waziri Christopher Chiza iliwahi kutoa ‘commitment’ bungeni tangu mwaka 2009 na 2011 kuwa ili kumaliza mgogoro wa ardhi katika shamba la Kapunga, inamalizia taratibu za kurekebisha hati ili mwekezaji abakie na eneo linalomstahili pekee.
“Pia wanakijiji warudishiwe eneo lao la kijiji. Hiki ndicho ambacho wanakijiji wale wanasubiri Profesa Tibaijuka atekeleze. Kinyume cha hapo anadhihirisha kuwa serikali ilidanganya Bunge na wananchi,” alisisitiza.
Alisema kuwa wananchi hao wanajua serikali ilishatoa ahadi ya kuwarudishia eneo lao, hivyo wanataka Profesa. Tibaijuka atekeleze kauli ya serikali badala ya kuanza mchakato mpya kama vile suala hilo limeanza hivi karibuni.
“Si siri kwamba suala la migogoro ya ardhi limefika mahali pabaya. Watu wanauana… kwa silaha za kisasa na jadi,” alisema.
Alisema kuwa iwapo waliopo madarakani, hususan katika wizara husika wangeguswa na damu ya Watanzania ambayo imeanza kumwagika kwa sababu ya ardhi, wasingeendelea kufanya ‘vituko’ kama alivyofanya Profesa Tibaijuka kwa kushindwa kutekeleza msimamo wa serikali uliotolewa mbele ya wawakilishi wa wananchi.
Alisema kuwa serikali kupitia wizara husika iwaeleze Watanzania wanataka watu wangapi wafe ili washtuke na kumaliza migogoro katika maeneo mbalimbali ikiwamo Kiteteo, Kapunga, Mvomero, Mtibwa, Malinyi na Kilombero.
Alisema kuwa kutokana na serikali kupuuza na kutochukua hatua za haraka, matokeo yake yameanza kuonekana ikiwemo waziri huyo kuzomewa na wananchi waliokerwa na kitendo chake cha kubadilisha msimamo wake  na kumruhusu  mwekezaji  kuendelea kumiliki eneo  la ardhi katika shamba  hilo.
Alisema kuwa kutokana na nafasi aliyonayo Profesa Tibaijuka na kuujua ukweli ulivyo katika chimbuko la mgogoro huo ambapo serikali yenyewe kupitia NAFCO iliuza ardhi kwa mwekezaji (hekta 7,370) na  kusajili na kupata hati moja   kwa eneo lote  zikiwamo hekta 1,870 za kijiji.
“Tulitarajia baada ya kuwa ameujua ukweli ulivyo angesimamia haki ionekane ikitendeka kupitia kauli ya serikali bungeni kwamba mwekezaji  akabidhi hati yake serikalini ifanyiwe marekebisho, wanakijiji wapate stahili yao,” alisema.
Alisema kutokana na utaratibu ule ule wa utendaji kazi wa kizembe, wenye viashiria vya rushwa, waziri hakuonekana kujali kauli hiyo, akapuuza hata ile aliyoitoa mwenyewe mapema kwenye kikao na wananchi, kabla hajapanda kwenye gari la mwekezaji akiwemo mkuu wa wilaya.
“Haya yaliyotokea Kapunga ni sehemu ya matukio mengi yanayoihusisha serikali kuuza ardhi kwa wawekezaji, wananchi wakiwa ndani ya ardhi hiyo! Tofauti na watu wa Kapunga, ambao waliamua kufanya kitendo cha kijasiri  cha kumzomea waziri wakafikisha ujumbe wao,” alisema.

No comments:

Post a Comment