MWANASHERIA wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amesema anachukizwa na mgambo kuchangisha fedha za michango mbalimbali bila ya kujali kuwa wanazidisha umaskini kwa wananchi.
Aidha, alisema kuwa serikali imekuwa ikitoa mabilioni ya fedha kila mwaka kwa ajili ya maendeleo ya kila wilaya lakini fedha hizo haziwafikii wanachi na badala yake wamekuwa wakiwachangisha michango ili kuficha ukweli.
“Sisi wabunge kila mwaka tumekuwa tukipewa kitabu kilichoandikwa mgawo wa fedha wa kila mbunge na jimbo lake na matumizi ya fedha hizo lakini nashangaa kuona kwamba hamkijui wala mbunge wenu hajawahi kuwasomea, kwa kweli nashangaa. Mimi jimboni kwangu sitaki mchezo kabisa, hakuna mgambo wala michango,’’ alisema Lissu.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, aliyasema hayo katika Kijiji cha Lwande, Kata ya Kiomoni alipokuwa katika ziara ya siku moja mkoani Tanga, ambapo pamoja na mambo mengine alimnadi mgombea udiwani wa Kata ya Kiomoni kupitia chama hicho, Mwanaisha Omary, katika uchaguzi wa udiwani unaotarajiwa kufanyia Febuari 9.
Alisema katika uongozi wa CCM, hakuna mwananchi yuko salama bila kuibiwa, hivyo wasifanye makosa kutompigia kura za ushindi ugombea huyo kwani watachagua kiongozi ambaye ataweza kusimamia fedha za miradi katika kata hiyo.
Naye Katibu wa CHADEMA Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa, alisema uchaguzi si kitu cha mzaha hivyo wananchi wasifanye makosa, wanatakiwa kuchagua kiongozi bora ambaye atawaletea maendeleo kwenye kata yao.
Katibu huyo alizungumzia pia masikitiko yake kwa kitendo cha mgombea udiwani kupitia chama hicho Kata ya Mtae, Jimbo la Mlalo, Wilayani Lushoto, Ally Jaha, kujitoa saa mbili kabla ya kurudisha fomu na kusema kuwa CHADEMA haitafumbia macho suala hilo.
Golugwa alisema inaonekana kuna rushwa imetembea, hivyo atamwandikia barua Mkuu wa Takukuru wilayani Lushoto aweze kufuatilia, kwani wamo viongozi wa CCM na serikali wa wilaya aliodai wanahusika na mchezo huo.
“Ndugu waandishi mimi naomba habari hii iwafikie ili wajue hatujalinyamazia. Upelelezi wetu umebaini kuwa rushwa imetembea, wahusika ni watu wa CCM wilaya pamoja na mkoa, hivyo Mkuu wa Takukuru wilaya tumeshampatia barua ili afuatilie,” alisema Golugwa.
No comments:
Post a Comment