Saturday, January 25, 2014

CHADEMA yaweka msimamo mzito

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetangaza msimamo mzito kwamba endapo vijana milioni tano wasipoandikishwa kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kitasusia kura za maoni ya Katiba.
Msimamo huo ambao mara ya kwanza ulitangazwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, ulitangazwa rasmi tena jana na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Willibrod Slaa.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara  uliofanyika katika uwanja wa michezo wa Shule ya Msingi Matarawe mjini Songea jana, Dk. Slaa alisema CHADEMA imekuwa ikipigia kelele suala hilo kwa muda mrefu, lakini Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imepuuza kwa madai kuwa haina pesa za kuandikisha wapiga kura hao.
Aliitaka serikali kuhakikisha inawaandikisha watu wote 5,300,000 ambao hawakuandikishwa kwenye daftari hilo baada ya kupoteza shahada zao kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo baadhi yao kuziuza wakati wa uchaguzi mkuu, kubadilishana na mbolea na baadhi ya vijana wengi waliofikisha umri wa miaka 18 kutoandikishwa katika daftari hilo.
“Nasema kuwa kama serikali haitakuwa tayari kukubali ushauri huo, basi itambue kwamba tutasusia kupiga kura ya maoni ya Katiba na tutazunguka nchi nzima kuwahamasisha wananchi kususia zoezi hilo kwani suala la katiba si la chama chochote cha siasa bali ni mali ya wananchi, sasa ni kwa nini liendeshwe kisiasa siasa?” alihoji Dk. Slaa.
CCM waingiwa hofu
Katika hatua nyingine, baadhi ya viongozi wa CCM na watendaji wa serikali wameingiwa  hofu na hatua ya CHADEMA kuanzisha operesheni hiyo inayojulikana kama M4C Pamoja Daima.
Wakizungumza na Tanzania Daima jana kwa sharti la kutotaka kutajwa majina, viongozi hao walisema kuwa CCM ina wakati mgumu wa kuhakikisha wananchi wanaendelea kukiamini chama hicho.
Alisema kuwa hatua ya CHADEMA kuamua kutumia chopa na kuzunguka maeneo mbalimbali ya nchi, itaendelea kubadilisha upepo wa kisiasa uliojengwa na uongozi wa CCM miezi michache iliyopita.
Kiongozi huyo alisema kuwa CHADEMA inapofanya mikutano yake inawafanya wananchi kuwa na uelewa wa masuala mbalimbali yanayojitokeza nchini na kama itaendesha harakati za kupinga mchakato wa Katiba mpya kama inavyotishia, inaweza kukwamisha kila kitu.
“Hivi sasa kuna suala la Bunge la Katiba ninaamini kuna changamoto itakayojitokeza katika hoja hiyo maana chama hicho kitatoa elimu itakayotumiwa na wananchi kuhoji juu ya suala hilo,” alisema.
Alisema kuwa mara zote chama hicho kinapofanya operesheni zake kinachangia wananchi kuwa na uelewa na kuhoji masuala mbalimbali kwa undani tofauti na CCM inapofanya mikutano yake.
“Wananchi wamekabiliwa na mambo mengi na wanakosa sehemu ya kuyawasilisha hivyo kitendo cha CHADEMA kuzunguka na chopa zao kuna mambo yatakayowafanya wananchi wabadilike na kuzidi kuichukia serikali, hasa likiwemo suala la kupanda kwa gharama za umeme ambalo linamsumbua kila mwananchi,” alisema.
Kiongozi huyo alisema kuwa iwapo CHADEMA itafanya mikutano katika Jimbo la Kalenga lililokuwa linashikiliwa na CCM, kuna uwezekano wa jimbo hilo kuchukuliwa na chama hicho.
“Kuna kazi huko tuendapo …tuwe tayari kuzomewa na kushambuliwa kwa maneno hasa pale inapotokea hakuna utekelezaji wa masuala ya msingi yanayopaswa kufanywa na serikali,” alisema.
Juzi CHADEMA ilianza operesheni mpya inayoongozwa na viongozi wake waandamizi, akiwamo Mwenyekiti, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, katika mikoa yote ya Tanzania Bara, kwa kutumia helikopta tatu.
Wengine wanaoshiriki operesheni hiyo iliyobatizwa jina la ‘Pamoja Daima’, ni wabunge, wakurugenzi wa makao makuu, wajumbe wa Kamati Kuu (CC), viongozi wa kanda, mikoa, wilaya na majimbo yote ya chama.
Mbowe alisema kuwa operesheni hiyo inafanyika katika mikoa, wilaya pamoja na majimbo yote ya uchaguzi ya Tanzania Bara, isipokuwa mikoa ya Lindi na Mtwara.

1 comment: