Saturday, January 25, 2014

Dk. Slaa aiweka pabaya Serikali

ZIARA ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Silaa na timu yake, imeutikisa mji wa Songea na vitongoji vyake mkoani Ruvuma, baada ya kupata mapokezi makubwa.
Umati wa watu bila kujali mvua, walijitokeza kwenye mapokezi hayo na kisha kuhudhuria mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Dk. Slaa, huku wakinyeshewa mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali iliyodumu kwa takriban saa mbili.
Akiwahutubia mamia ya wananchi ambao walikuja kumsikiliza katika uwanja wa michezo wa Shule ya Msingi Matarawe, uliopo katika manispaa hiyo, Dk. Slaa ambaye viatu vyake vilionekana kujaa maji baada ya kunyeshewa mvua hiyo, alisema lengo la ziara hiyo ni kuwafikishia wananchi ajenda mbili, ambazo ni uandikishwaji majina katika daftari la kudumu la wapiga kura pamoja na ulinzi wa rasilimali za taifa.
Aliitaka serikali kuhakikisha inawaandikisha watu wote 5,300,000 ambao hawakuandikishwa kwenye daftari hilo baada ya kupoteza shahada zao kutokana na sababu mbalimbali, zikwemo baadhi yao kuziuza wakati wa Uchaguzi Mkuu, kubadilishana na mbolea na baadhi ya vijana waliofikisha umri wa miaka 18 kutoandikishwa katika daftari hilo.
“Nasema kuwa kama serikali haitakuwa tayari kukubali ushauri huo basi itambue kwamba tutasusia kupiga kura ya maoni na tutazunguka nchi nzima kuwahamasisha wananchi kususia zoezi hilo, kwani suala la katiba si la chama chochote cha siasa, bali ni mali ya wananchi, sasa ni kwa nini liendeshwe kisiasa siasa?” alihoji Dk. Slaa.
Akizungumzia kwa upande wa rasilimali za taifa alisema wananchi wanatakiwa kuwa wamiliki wakubwa wa ardhi yao na endapo kuna wawekezaji wanataka maeneo hayo ni vema wakafuata masharti na mahitaji ya wananchi badala ya kuwafanya Watanzania kuwa watumwa kwenye nchi yao.
Naye Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, alisema CHADEMA kamwe haitaweza kukaa kimya wakati rasilimali za nchi zinatoroshwa na baadhi ya viongozi huku Watanzania wakiishi katika maisha magumu.
Msigwa ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Wizara ya Maliasili na Utalii, alisema kuwa umaskini mkubwa unaowakabili Watanzania kwa kiasi kikubwa unachangiwa na viongozi waliopo madarakani na si laana kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama wanavyodai wengine.
Aidha, aliishushia lawama Idara ya Usalama wa Taifa kwa kushindwa kulinda rasilimali za nchi na badala yake wamekuwa wakiziacha zikitoroshwa na kuelekeza nguvu katika kukilinda chama tawala wakati wanyama, magogo na pembe za ndovu vinasafirishwa kwenda kuuzwa nje ya nchi wakati taifa likiendelea kuwa maskini.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CHADEMA, Edson Mbogoro, alisema kwamba Kijiji cha Nyororo kitakuwa historia kwa Watanzania kama sehemu ya hija, kwa ajili ya kumkumbuka mwana harakati za ukombozi,  aliyekuwa mwandishi wa habari marehemu Daudi Mwangosi, aliyeuawa na polisi wakati wa mkutano wa chama hicho.

No comments:

Post a Comment