Wednesday, January 1, 2014

Mwenyekiti Chadema ang’aka: Hatuwataki Wanachama Popo!

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kata ya Sungaji, Musa Kombo, amesema, Kata yake haiwataki Wanachama Popo ambao Usiku wanajenga Mashina ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Mchana wanavaa Magwanda wakijifanya Chadema.
 
Kombo alisema, Kama yalivyo maamuzi ya Kamati Kuu ya Chadema, wao pia wanayatii yaliyoamuliwa na vikao hivyo, kwa hiyo watakuwa wa mwisho kuwa na Mbereko ya kuwabeba wanachama Popo katika chama chao, ikiwemo Kata yao.
 
Kauli ya Kombo inafuatia kuwepo kwa fununu za Mwanachama, Reuben Sembuche, aliyekuwa Chadema na kutupa Kadi ya Chama hicho kwa madai ya kukiacha, lakini hivi karibuni alionekana katika moja ya Mikutano ya Chadema Wilaya Kata hiyo akihutubu mkotanoni.
 
Kombo alisema, “Zipo Taratibu za Chama ambazo mtu akikengeuka kwenye Chama anapotaka kurejea lazima azifuate ili ajadiliwe na hatimae arejeshwe! Lakini Kata inashangaa kuona mtu huyo huyo yupo jukwani amerudi kinyemela na Uongozi wa Kata hauna habar”.
 
Kombo aliuasa Uongozi wa Wilaya Mvomero, kuwa Makini sana na Watu ambao kwa siku za hivi karibuni wamekuwa si watiifu ndani ya Chama, na badala yake wamekuwa wakitumika vibaya na Upande wa pili ili kukidhoofisha Chadema kwa Tamaa ya Fedha na Madaraka.
 
Aidha Ijumaa Desemba 29, Mwaka huu, Chadema Kata ya Sungaji ilikuwa na Kikao kujadili na kutathimini Mustakabali wa Mafanikio na Mapungufu ya Mikutano ya Chama chao iliyofanywa na Wilaya katika Kata ya Sungaji Vijiji vya Mbogo na Kigugu, ambapo Mapungufu ya ukiukwaji wa Ratiba ya Mikutano, lilikuwa mojawapo.
 
Gazeti hili lilimtafuta Katibu Mwenezi na Kaimu Katibu wa Wilaya, Mohamed Mrisho, na kumwandikia Ujumbe Mfupi (SMS) kujua iwapo yupo Mwanachama Popo aliyerejea kinyemela lakini hakutoa ushirikiano, hata hivyo Mwenyekiti wa Wilaya, Saimanga Kashikashi naye hakujibu Ujumbe Mfupi alioandikiwa hadi tunakwenda mitamboni.

No comments:

Post a Comment