Wednesday, January 1, 2014

Katiba kutumika Uchaguzi 2015

Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya, imeelekeza kipindi cha mpito ambacho pamoja na mambo mengine, kitaandaa mazingira ya Katiba hiyo kutumika kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
“Kufanya maandalizi na kuendesha Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kuzingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 2014 na kufanya maandalizi ya mambo yote muhimu kwa ajili ya utekelezaji bora wa masharti ya kikatiba yaliyomo kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya Mwaka 2014,” inasema sehemu ya rasimu hiyo.
Tume ya Mabadiliko ya Katiba pia imependekeza kipindi cha mpito cha miaka minne kuanzia tarehe ya kuanza kutumika kwa Katiba Mpya ili sheria zilizopo ziweze kubadilishwa.
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba alisema jana kwamba katika kipindi hicho cha mpito utakuwa ni muda wa kutungwa kwa Katiba ya Tanganyika. Warioba alisema pia katika kipindi hicho, utakuwa ni muda wa mgawanyo wa rasilimali baina ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali za nchi washirika.
“Katika kipindi hicho pia utakuwa ni muda wa kufanya maandalizi na kuendesha Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa kuzingatia masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 2014,” alisema.
Warioba alisema katika kipindi hicho, Katiba ya Zanzibar itafanyiwa marekebisho ili kuwiana na masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 2014.

Maoni ya Muungano kutengeneza Katiba ya Tanganyika
Sehemu ya Rasimu ya Katiba ya Muungano, imependekeza kuwa maoni yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, yanaweza kutumika kutengeneza Katiba ya Tanganyika.

No comments:

Post a Comment