Sunday, January 19, 2014

Mnyika: Serikali, TANESCO zinafilisiana

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amesema kuwa serikali na TANESCO kwa pamoja zinafilisiana, na hali hiyo inasababishwa na udhaifu katika Wizara ya Nishati na Madini.
Mnyika alitoa kauli hiyo jana wakati akitoa maoni yake kuhusu madeni yanayoikabili TANESCO na mkakati wa kutaka kuendesha operesheni kata umeme kwa wadaiwa sugu.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mnyika alitaja sababu nyingine kuwa ni ufisadi katika sekta ya nishati wenye athari kwa uchumi wa nchi na maisha ya wananchi.
Alisema kuwa suala la TANESCO kubeba mzigo wa madeni sugu ya serikali na taasisi zake pamoja na kampuni binafsi sio geni kwani ameshalisema bungeni tangu mwaka 2011, 2012 na 2013.
“Badala ya Mkurugenzi Mramba kusema watachukua hatua, nilitarajia aeleze hatua ambazo tayari wameshaanza kuchukua, hiyo ni aibu kuona sasa ndio wanazungumzuia kuwapa notisi wadaiwa wakati tatizo linafahamika muda mrefu, hata kabla ya Mramba kuteuliwa kuwa mkurugenzi akiwa kaimu mkurugenzi,” alisema.
Mnyika alimlaumu Mramba na TANESCO kwa kuficha majina ya wizara za serikali na taasisi zake ambazo ni wadaiwa sugu pamoja na watu binafsi wanaohusika.
“Kwani ni muhimu watajwe hadharani wote ambao ni wadaiwa sugu wa muda mrefu ambao wamekumbushwa na barua wakapuuza, lakini pia suala la wadaiwa sugu ambao ni mamlaka za juu ya kiserikali haliwezi kushughulikiwa na TANESCO pekee,” alisema.
Mnyika alimtaka Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kutoa majibu kwa umma kwa kuzingatia kwamba suala la wadaiwa wenye madeni sugu nilishamhoji bungeni Mei 22, 2013 na badala ya kujibu akatoa maelezo yasiyokuwa ya kweli bungeni Mei 25, 2013.
“Katika hotuba yangu bungeni nilitaja majina na viwango vya mabilioni ambavyo wizara na taasisi za serikali zinadaiwa,” alisema.
Alizitaja wizara na taasisi hizo kwa wakati huo kuwa ni Wizara ya Maji, Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi Tanzania, Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO) na taasisi nyingine.
“Muda mrefu umepita toka nitake Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO wachukue hatua, lakini mpaka sasa badala ya kueleza hatua zilizofikiwa, TANESCO inatoa taarifa kwamba ndiyo wanataka kuchukua hatua, huku ikiendelea kuficha majina ya taasisi za serikali zinazodaiwa zaidi ya sh bilioni 129.
“Hili ni kati ya mambo ambayo kabla ya kuruhusu kupanda kwa bei ya umeme, Ewura na wizara walipaswa kwanza kukusanya fedha hizo,” alisema.
Mnyika ambaye ni Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, aliponda ahadi ya hivi karibuni iliyotolewa na TANESCO kufanya marekebisho makubwa ya kiutendaji, na badala yake ilichotakiwa kufanya ni matendo badala ya maneno kwa kuwa kauli kama hizo zimekuwa zikitolewa bila utekelezaji.
Alisema marekebisho ya utendaji wa TANESCO sio wa kutolewa kauli na Mkurugenzi wa Shirika hilo Felchesmi Mramba pekee kwa kuwa linahusu masuala mapana ya muundo, mfumo na uongozi mzima wa shirika hilo, hivyo zipo hatua ambazo zinapaswa kuchukuliwa na mamlaka nyingine ikiwemo Wizara ya Nishati na Madini na Ofisi ya Rais.
Mnyika alisema kwa sasa ni wajibu wa Waziri Muhongo kueleza sababu za kutotekeleza ahadi yake aliyoitoa mwaka 2012 na kuirudia tena mwaka uliofuata ya kufanya mabadiliko ya muundo na utendaji katika shirika hilo kwa kipindi kifupi, lakini hadi sasa hajatekeleza.
“Ikumbukwe kwamba Waziri Muhongo aliwahi kueleza kwamba ameunda kikosi kazi kuangalia upya miundo na utendaji wa mashirika yaliyo chini yake, hususani TANESCO na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), hata hivyo ripoti za kamati hizo zimefanywa kuwa siri,” alisema.
Akizungumzia hali ya umeme iliyoonyesha kuridhisha, Mnyika alipinga na kusema kuwa kauli hiyo ya Mramba inaficha ukweli wa udhaifu uliopo katika utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme.
“Anaposema hali ya umeme imepanda kutoka 851 hadi 898, lakini ukweli kwamba tukiwa bado tunategemea mitambo ya mafuta kama chanzo kikuu cha umeme, umeendelea kuwa asilimia 45 hali inayofanya kuongeza kwa kiwango kikubwa gharama za umeme na mzigo kwa TANESCO, nchi na wananchi,” alisema.
Mnyika alitoa ushauri akisema kuwa wakati ambapo nchi ikisubiri ongezeko la matumizi ya gesi kuwa zaidi ya asilimia 42 ya sasa, TANESCO ilipaswa kufanya ukarabati wa dharura wa vyanzo vya maji ambavyo kwa sasa vinazalisha asilimia 13 ambayo ni chini ya uwezo halisi.
Naye Abdallah Hussein wa Kariakoo, alisema ili TANESCO iweze kufanya kazi kwa ufanisi, serikali lazima ifanyie kazi maoni ya Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe, ya kufikiria kuwepo kwa shirika mbadala ambalo litatoa ushindani kwa TANESCO ili iweze kutekeleza shughuli zake.
Katunzi Oswald wa Mbagala Rangi Tatu alitoa maoni yake kwa kusema TANESCO kwa sasa ni shirika la matajiri, hivyo amewataka maskini kutumia umeme wa jua ‘solar’ na kuwaacha matajiri waendelee na shirika hilo.
“Cha ajabu juzi nilitoa 20,000/- kununua umeme, nimepata uniti 8 pekee, ni heri wote tuhamie kwenye solar, na kuiacha TANESCO ife kama TTCL ilivyo sasa ili wafanyakazi wake wawe na heshima kwa wananchi,” alisema Oswald.
Naye Ayubu Jumanne wa Temeke, Mtongani, alisema kama wanataka kuliokoa shirika hilo ni lazima watumishi wa ngazi ya juu wote waondolewe na kuomba kazi upya akiwamo mkurugenzi.

No comments:

Post a Comment