Thursday, January 23, 2014

Mnyika: JK hawezi kufunga mjadala wa gesi

KATIKA mkutano wa Ndala, Nzega mkoani Tabora wananchi walitoa sauti za kulalamikia ongezeko la bei ya umeme huku wakilaani madhara ya Operesheni Tokomeza Ujangili, ambapo pia walitaka kujua kuhusu matumizi ya rasilimali za taifa na kauli za viongozi kufunga mijadala juu ya suala la gesi.
Akijibu swali hilo, John Mnyika ambaye ni Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, alisema:
“Kikwete hawezi kufunga mjadala wa rasilimali za nchi, ikiwemo rasilimali mkakati na nyeti ya gesi. Mjadala kuhusu wananchi kunufaika na rasilimali uhamie kwa wananchi wenyewe, si kufungwa na viongozi wa serikali. CHADEMA sasa kupitia operesheni hii kwa mara nyingine tena inaleta kwenu mjadala huu ili sote tuhoji namna rasilimali za taifa zinavyosimamiwa na kutumika.
“Kwa mara nyingine tena Rais Kikwete anageuka kuwa mtetezi wa wageni dhidi ya wazawa. Alifanya hivyo hivyo wakati alipokuwa Waziri wa Nishati na Maji kwa kusaini mikataba mibovu na kuitetea akiwa Waziri wa Mambo ya Nje,” alisema Mnyika.
Akikazia hoja ya madai yake kuhusu Rais Kikwete kuhusika katika mikataba mibovu, Mnyika aliwaambia wananchi wa Nzega wakumbuke jinsi wakazi wa Lusu jirani na uliokuwa mgodi wa dhahabu wa Nzega Golden Pride Mine Ltd, walivyohamishwa kwa mitutu ya bunduki miaka ya 1990.
Mnyika aliongeza kusema kuwa hata wakati huo zilitolewa kauli kama za hivi sasa kuhusu gesi lakini hadi leo wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya migodi na Watanzania wengine kwa ujumla hawaoni manufaa ya wazi kuhusu rasilimali zao.
“Waziri Muhongo ni muongo, hataki kusema lakini sisi tunamwambia kuna ufisadi mkubwa katika suala la gesi. Nipende tu kuwaambia Watanzania wa Nzega na mahali pengine ambao wanashauku kuona rasilimali hizi zinatumika kwa manufaa ya taifa zima, kwamba nitakwenda kumbana Muhongo bungeni juu ya jambo hili.
“Pamoja na kusimamia mambo mengine na sisi tungeomba sana muendelee kuijadili hii rasimu ya pili kabla ya bunge maalumu, nawataka wananchi wote mhakikishe masuala mengine ya muhimu ambayo tume haijayazingatia, muendelee kuyasukuma katika mijadala yenu hasa kuhusu haki ya kumiliki rasilimali inaingizwa kwenye katiba mpya.
“Nawaombeni tupige kura ya wazi hapa hapa…wangapi wanapinga msimamo wa CCM ambao unapingana na maoni ya Watanzania kuhusu katiba mpya…asanteni sana naona watu wote hapa mnasema mnapinga msimamo huo wa CCM. Kwa kura hizi za wananchi namtaka mbunge wenu aheshimu hizi kura za wazi za wananchi na aungane na msimamo huu katika bunge la katiba,” alisema Mnyika.

No comments:

Post a Comment