Thursday, January 23, 2014

Lissu: Tusijadili suala la Zitto

MWANASHERIA Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu, amewataka Watanzania, hususan wanachama wa chama hicho kutopoteza muda kujadili suala la baadhi ya wanachama waliopatikana na makosa ya usaliti na utovu wa maadili ndani ya chama hicho, kisha kuchukuliwa hatua bali wajikite kukiimarisha chama hicho kila mahali na kujadili masuala yanayowahusu wananchi.
Lissu ambaye aliambatana na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa CHADEMA (BAVICHA), John Heche, alisema kuwa taifa linakabiliwa na masuala mengi ambayo yanahitaji umakini wa kila mwanachama wa chama hicho akitolea mfano wa kujadili maudhui ya Rasimu ya Pili ya Katiba Mpya, ili taifa lipate katiba mpya na bora.
Mwanasheria huyo pia aliwaambia wananchi wa maeneo hayo kwamba kutokana na uongozi mbovu, rasilimali za Tanzania zimeendelea kutafunwa na watu wachache kwa kupitia sera za ubinafsishaji ambazo zimetumiwa na watawala kama mianya ya kujigawia mali kwa mgongo wa uwekezaji, huku wazawa wengi wakiwa hawana la kufanya.
Alitumia mikutano hiyo kusoma taarifa za kila mwaka wa bajeti za serikali ambazo zinaonesha mgawo wa fedha wa kila eneo kwa sekta hususan zinazohusu huduma za jamii, akisema wananchi wengi hawajui kwa sababu viongozi wao hawataki wajue.
Kwa upande wake, John Heche aliwaambia wananchi kwamba bila kuupiga vita na kuutokomeza ufisadi ambao unaendelea kulitafuna taifa akidai unalelewa na Serikali ya CCM, wananchi hawatapata matumaini na maendeleo wanayoyahitaji.
Alisema kuwa hata ujangili unaoendelea kwa kasi kubwa kiasi cha kutia shakani uwepo wa tembo katika mbunga za wanyama ni matokeo ya ufisadi ambao CHADEMA kimekuwa kikihamasisha umma kuupiga vita kwa nguvu zote kwa sababu utaliangamiza taifa.
Alisema kuwa pamoja na Tanzania kuwa moja ya mataifa machache yaliyobarikiwa kila aina ya utajiri wa rasilimali, wananchi wake wanazidi kuwa maskini huku viongozi wao wakitembea nje ya nchi kuomba vitu vidogo kama vyandarua, wakati taifa lina uwezo wa kuhudumia watu wake kwa vitu kama hivyo endapo kungelikuwa na viongozi bora wanaojali watu wao.
“Ninyi wananchi mnajua kwamba viongozi wa Serikali ya CCM wanakwenda karibu kila siku Ulaya kutembeza bakuli la kuomba misaada, lakini misaada wanayoomba si ile ambayo inaweza kutusaidia kama taifa kuondokana na matatizo yetu ya umaskini, ujinga, maradhi na sasa ufisadi, wanakwenda Ulaya kuomba vyandarua wakiwa wanarudi wanapishana angani na Wazungu wamebeba dhahabu, almasi na vitu vingine vya thamani kutoka Tanzania,” alisema Heche.

No comments:

Post a Comment