Thursday, January 23, 2014

Mnyika atetea upanuzi wa barabara

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amenukuliwa kimakosa kwamba haoni umuhimu wa kupanua barabara kutoka Kibaha hadi Dar es Salaam wakati maeneo mengine ya nchi hayana barabara zinazopitika kwa kirahisi.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Mnyika alisema kuwa kwa nyakati mbalimbali kati ya mwaka 2004 na 2013 amezungumzia haja ya upanuzi wa barabara ya Morogoro kutoka jimboni Ubungo kupitia Kibaha hadi Chalinze na mgogoro uliodumu muda mrefu kuhusu upana wa barabara hiyo.
“Ningependa kutoa ufafanuzi kwamba nyakati zote nimeunga mkono upanuzi wa barabara hiyo, ikiwemo ujenzi wa barabara hiyo kuwa njia sita (tatu kwenda na tatu kurudi).
“Hata hivyo, mara nyingi nimekosoa masuala manne kuhusu upanuzi na mgogoro kuhusu upana wa barabara ya Morogoro,” alisema.
Mosi, serikali kutoa ahadi bila utekelezaji kwa miaka mingi. Pili, badala ya serikali kuja na wazo la kujenga njia zaidi ya sita, ianze kwanza kutekeleza ahadi ya njia hizo sita; kwa kuanza na ujenzi katika umbali wa mita 60 zilizopo.
Tatu, Mnyika alisema serikali kupotosha kwa miaka mingi kuhusu upana wa barabara hiyo.
“Nne ni kwamba kwa nyakati zote nimesisitiza kwamba iwapo serikali inataka kutwaa maeneo ya nyongeza kwa ajili ya ujenzi nje ya nafasi ambayo tayari inawezesha ujenzi wa barabara hiyo, basi ihakikishe inalipa kwanza fidia kwa wananchi kabla ya kubomoa nyumba za wananchi na kuwasababishia umaskini,” alisema.
Alisema kuwa suala hilo nalo alilisisitiza katika mkutano wake na wananchi Januari 19 mwaka huu katika eneo la Luguruni.
“Katika muktadha huo, namshauri Rais Jakaya Kikwete kukaa na mawaziri wake kuwaelekeza kuipitia, kuiheshimu na kuwezesha utekelezaji wa maamuzi ya mahakama pamoja na kuharakisha ujenzi wa barabara huku ikilinda haki za msingi za wananchi wa majimbo ya Ubungo, Kisarawe, Kibaha Mjini na Chalinze walioshi pembezoni mwa barabara hiyo, wenye haki zilizotambuliwa tangu wakati wa Operesheni Vijiji,” alisema.

No comments:

Post a Comment