Thursday, January 23, 2014

CHADEMA yaja na ajenda 9

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeamua kuwasha moto nchi nzima kwa wiki mbili mfululizo kuanzia leo, ukiwa ni mkakati wa kujiimarisha na kujadiliana na wananchi kuhusu masuala nyeti ya kitaifa.
Katika kutekeleza azima hiyo, chama hicho kimejigawa katika makundi makuu matatu, na vikosi vidogo sita, yatakayowashirikisha viongozi wakuu wa chama, wabunge, wenyeviti wa mikoa, wilaya, majimbo na kanda za chama.
Operesheni hiyo imepewa jina la ‘M4C Pamoja Daima’ ikiwa na lengo la kuwafikisha viongozi hao katika mikoa yote ya Tanzania Bara, kupeleka ujumbe kwa umma kupitia ajenda tisa (9) zilizopendekezwa na Kamati Kuu katika kikao chake kilichofanyika mwanzoni mwa mwezi huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za makao makuu ya chama hicho, Kinondoni, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema ni operesheni maalumu yenye lengo la kuimarisha chama na kuwapa wananchi fursa ya kujadili masuala muhimu yanayogubika taifa mwanzoni mwa mwaka 2014.
Ajenda hizo ni mchakato wa katiba mpya katika hatua ya Bunge la Katiba na kura ya maoni; daftari la kudumu la wapiga kura; uchaguzi wa madiwani katika kata 27; ujenzi wa chama ngazi za chini; uchaguzi ndani ya chama; uchaguzi serikali za mitaa na kuandaa umma kwa uchaguzi mkuu 2015.
Vile vile, viongozi hao watajadili kero zinazowakabili wananchi; na watafika katika Jimbo la Kalenga kuhani msiba, na kuwapa pole wananchi kwa kufiwa na mbunge wao, William Mgimwa aliyekuwa pia Waziri wa Fedha.
Mbowe alisema operesheni hiyo imegawanyika katika makundi makuu matatu. Makundi hayo yatagawanyika katika vikosi sita; vitatu vya angani kwa kutumia helikopta na vitatu vya ardhini kwa kutumia magari.
Mbowe alisema chama hicho kimegubikwa na matukio makubwa ya kisiasa ukiwamo uchaguzi wa ndani na ule wa serikali za mitaa, na kwamba wanahitaji kujipanga ipasavyo kuweza kukabiliana na hali hiyo.
“Hatufanyi kampeni bali huu ni mwendelezo wa maandalizi ya uchaguzi mbalimbali. Kama mnakumbuka tulianza kujiandaa na uchaguzi wa 2015 pale tulipomaliza uchaguzi mkuu uliopita, na sasa tunachofanya ni kuongeza nguvu na umakini zaidi katika muda huu,” alisema Mbowe.
Misafara ya helikopta na magari katika operesheni hiyo itaanzia katika mikoa ya Tanga, Mwanza na Ruvuma. Katika kila eneo, viongozi hao watapita katika kata zote zinazotarajiwa kufanya uchaguzi wa marudio kwa ajili ya madiwani ili kuwaongezea nguvu wagombea wa CHADEMA.
Vile vile, watapita katika maeneo yote yaliyoathiriwa na mikakati kadhaa ya utekelezaji wa maagizo ya serikali kama Operesheni Kimbunga na Operesheni Tokomeza Ujangili.
Baadhi ya makada wa CHADEMA waliozungumzia operesheni hiyo, walisema inalenga kuelekeza nguvu ya chama katika masuala ya msingi na kuimarisha umoja miongoni mwa wanachama.
Kwa msisitizo wa pekee, Mbowe alionya serikali isifanye mzaha na daftari la kudumu la wapiga kura, akisema mzaha wowote wa aina hiyo ni kuchezea amani ya nchi.
Alisema CHADEMA imeshajua mbinu za serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kukwamisha mchakato wa katiba mpya, na kutoandikisha wapiga kura katika daftari la kudumu, na kwamba kama CCM wanadhani watazuia katiba mpya kupatikana kistaarabu, CHADEMA itatumia njia mbadala kuhakikisha wananchi wanapata katiba wanayotaka.
“Hakuna kurudi nyuma kwenye suala la katiba mpya. Wakichezacheza na mchakato wa katiba mpya, tutaitafuta kwa utaratibu mwingine,” alisisitiza.
Alisema watatumia ziara hii kuelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kujiandikisha katika daftari hilo, na kuitaka serikali itumie muda huu kuandikisha wananchi wote wenye sifa ambao hawajajiandikisha kupiga kura kwa sababu mbalimbali.
Miongoni mwa kazi watakayoifanya katika ziara hizo ni kuelimisha wananchi na kuwahamasisha kuchukua hatua iwapo serikali itagoma kuboresha daftari hilo.
Hadi sasa inakisiwa kuwa wananchi wapatao milioni nne, hasa vijana, hawajaandikishwa katika daftari la kupiga kura kwa visingizio kadhaa vya Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Kisingizio kikubwa kinachotolewa ni ukosefu wa fedha za kufanyia kazi hiyo.
Mbowe alisema watahamasisha Watanzania wasishiriki mchakato wa kura ya maoni iwapo serikali itagoma kuboresha daftari hilo, lakini haina maana ya kususa, bali kutafuta njia mbadala ili kunusuru taifa lisiingie katika machafuko.
Alisema kama Serikali ya CCM inataka amani iendelee kuwepo wasifanye mzaha katika suala la katiba kwani si la CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi bali ni mustakabali wa Watanzania.
Mbowe alisema kuwa sheria inaelekeza daftari la kudumu la wapiga kura kufanyiwa maboresho kati ya uchaguzi na uchaguzi ili kuwapa nafasi watu waliohama maeneo yao, waliopoteza vitambulisho na waliotimiza sifa ya kujiandikisha.
Alisema kuwa kuendelea kuwaacha nje watu hao ni kuwanyima haki yao ya kikatiba ya kupiga kura.
“Kama katiba haitapita kwa sababu ya kushindwa kuboreshwa kwa daftari la kudumu, wasidhani tutarudi katika katiba ya zamani. Hiyo ni ndoto ya CCM.
“Nawaambia waache, na kama serikali inataka amani wasifanye mzaha katika suala la katiba,” alisema.

No comments:

Post a Comment