Thursday, January 23, 2014

Chadema yawaonya wabunge CCM

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema kuwa chama hicho kitachukua uamuzi mgumu ikiwa wabunge wa CCM watajikita katika kulinda masilahi yao kwenye Bunge Maalumu la Katiba kinyume na maoni ya wananchi.
Alisema hayo jana katika Wilaya ya Nyasa na Mbinga kwenye siku ya kwanza ya Operesheni Pamoja Daima. Katika operesheni hiyo, ambapo aliruka kwa helikopta katika sehemu mbalimbali, alihutubia mikutano katika maeneo ya Mbamba Bay, Mbinga, Peramiho, Namtumbo na Songea Mjini.
Akiongozana na Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, Dk Slaa aliwaonya wabunge wa CCM kutotumia wingi wao bungeni kutetea masilahi ya chama chao. “Kamwe wasithubutu kwani Chadema itachukua uamuzi mgumu ambao kwa sasa si vizuri kuutaja,” alisema Slaa.

Alionya akisema ni lazima wabunge watoe maoni ambayo yana masilahi ya wananchi wote na siyo vyama.

Daftari la wapigakura

Katika hatua nyingine, alisema Chadema itasusia kura ya maoni iwapo daftari la wapiga kura halitaboreshwa kwa ajili ya mchakato wa Katiba.
Alisema kwa sasa chama hicho kinasambaza fomu maalumu nchi nzima kwa ajili ya watu wasio na vitambulisho vya kupiga kura wajiorodheshe.
“Kuna maelfu ya watu waliopoteza vitambulisho vyao vya kupigia kura na wengine wamefikia umri wa kupiga kura lakini Serikali haioni suala hilo kuwa ni muhimu,” alisema.

Alisema uchunguzi wa chama hicho umebaini watu zaidi ya 5,000,000 hawana vitambulisho vya kupigia kura japokuwa tayari wamefikia umri wa kupiga kura.

Ili kuhakikisha Bunge la Katiba linakuwa na manufaa, Dk Slaa aliwataka wananchi kufuatilia mjadala juu ya Katiba Mpya kwa makini ili kuwabaini wabunge wasioitakia nchi hii mema.
Alisema wabunge wa namna hiyo wamepanga kutengeneza Katiba ya viongozi badala ya katiba ya wananchi.

Baadaye katika mkutano uliofanyika katika Uwanja wa Matarawe mjini Songea mvua kubwa ilinyesha, lakini wananchi waliofurika hawakujali kunyeshewa badala yake walionyesha shauku ya kuendelea kumsikiliza Dk Slaa.

Mawaziri Mizigo

Kwa upande wake, Msigwa alisema CCM wana deni la kujieleza mbele ya wananchi kwa sababu walitangaza mawaziri mizigo lakini Rais Jakaya Kikwete bado ameendelea kuwaweka kwenye Baraza la Mawaziri.
“Kinana (Abdulrahman, Katibu Mkuu wa CCM) na Nape (Nnauye, Katibu wa Itikadi na Uenezi) walikuja kwenu na kutaja majina ya mawaziri mizigo, walikuwa wanadanganya, si mnaona wale waliowataja wameteuliwa tena? Chama hicho siyo makini,” alisema Msigwa.
Alidai kuwa kwa sasa CCM imegawanyika na kila kiongozi anatoa kauli yake kulingana na anavyojisikia na wala hazingatii vikao.
Alisema mparaganyiko uliopo ndani ya CCM kwa sasa ndio utakaosaidia Chadema kushinda kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.

‘Washambulia’ Tanga
Naye, Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu akisindikizwa na Mwenyekiti wa Taifa wa Vijana Chadema, John Heche, Katibu wa Vijana, Deo Munisi na Katibu wa chama hicho Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa ‘walishambulia’ baadhi ya wilaya za Mkoa wa Tanga.
Lissu alifanya mikutano katika Wilaya za Lushoto, Korogwe, Muheza na Tanga huku wakimtaka Rais Jakaya Kikwete kuharakisha mchakato wa uboreshaji wa daftari la wapiga kura.
“Rais Kikwete alipokea Rasimu ya Pili ya Katiba, lakini katika mazungumzo yake mbalimbali hakuzungumzia mchakato wa uboreshaji wa daftari la wapiga kura...Serikali iharakishe maboresho, kwani litakapokuja suala la kura ya maoni wengi watashindwa kupiga kura.
“Na kilio cha wananchi kitaonekana itakapotokea wakashindwa kupiga kura,” alisema Lissu, ambaye akiwa Wilaya ya Tanga, alifanya mikutano katika Kijiji cha Lwanda, Kata ya Kiomoni ambako Mwanaisha Omari anawania udiwani wa kata hiyo.

No comments:

Post a Comment