Thursday, January 23, 2014

Mnyika amvaa Magufuli

Mbunge wa Jimbo la Ubungo (Chadema), John Mnyika amemtaka Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli na Wakala wa Barabara (Tanroads) waelekeze nguvu katika kusimamia ujenzi wa mradi wa mabasi yaendayo kwa haraka (BRT) kutoka Ubungo hadi Chalinze.

Amemtaka Waziri Magufuli pia kuipitia, kuiheshimu na kuwezesha utekelezaji wa maamuzi ya mahakama juu ya hukumu ya kesi ya wananchi wa maeneo hayo ambao wanapinga kuondolewa kupisha ujenzi wa barabara hiyo.

Katika taarifa yake aliyoiwasilisha kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana, Mnyika alisema kutokana na serikali bado haijapanga bajeti ya fedha za kujenga barabara hiyo ni vyema ikatumia mbinu mbadala za kupanua barabara za pembezoni ili kupunguza tatizo la foleni.

“Badala ya serikali kuja na wazo la kujenga njia zaidi ya sita, ianze kwanza ujenzi wa umbali wa mita 60 zilizopo, sioni haja ya serikali kujenga kwa sasa mpaka eneo la upana wa mita 241 wakati kuna barabara nyingine muhimu za pembezoni mwa barabara ya Morogoro ambazo zikiharakishwa kujengwa zinaweza kupunguza foleni kama vile Goba-Mbezi-Msigani-Malambamawili-Kinyerezi na nyinginezo ambazo ujenzi wake unasuasua,” alisema Mnyika.

Pia aliitaka Serikali kuhakikisha inawalipa fidia wakazi wa maeneo hayo kabla ya kuwabomolea maeneo yao.

“Nimekuwa nikisisitiza kwamba iwapo serikali inataka kutwaa maeneo ya nyongeza kwa ajili ya ujenzi nje ya nafasi ambayo tayari inawezesha ujenzi wa barabara hiyo, basi ihakikishe inalipa kwanza fidia kwa wananchi kabla ya kubomoa nyumba za wananchi na kuwasababishia umaskini. Kutokana na Mkandarasi (Starbag) na Wakala (Dart) hawatekelezi ipasavyo masharti ya mikataba,” alisema Mnyika.

No comments:

Post a Comment