Thursday, January 23, 2014

Chopa tatu kufunika nchi kwa siku 14

Mbunge wa Iringa Mjini Mh Peter Msigwa akiwa mbele ya Moja ya Chopa zitakazokuwa katika Operesheni Pamoja Daima

  Ni operesheni mpya 'Pamoja Daima' ya Chadema
  Inaanza leo, kuwashirikisha viongozi waandamizi
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeanza operesheni mpya inayoongozwa na viongozi wake waandamizi, akiwamo Mwenyekiti, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, katika mikoa yote ya Tanzania Bara, kwa kutumia usafiri wa helikopta tatu.

Wengine wanaoshiriki operesheni hiyo iliyobatizwa jina la “Pamoja Daima”, ni wabunge, wakurugenzi wa makao makuu, wajumbe wa kamati kuu (CC), viongozi wa kanda, mikoa, wilaya na wa majimbo yote ya chama.

Mbowe aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa, operesheni hiyo itafanyika katika mikoa, wilaya pamoja na majimbo yote ya uchaguzi ya Tanzania Bara, isipokuwa mikoa ya Lindi na Mtwara.

Alisema hadi sasa bado hawajapata uhakika wa kuruhusiwa kufanya mikutano ya hadhara kutokana na zuio la serikali katika mikoa hiyo miwili.

Serikali iliamua kuzuia mikutano ya kisiasa katika mikoa hiyo miwili tangu mwaka jana kutokana na kuzuka kwa vurugu zilizotokana na wananchi kupinga usafirishaji wa gesi kwa njia ya bomba kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam.

Hata hivyo, Mbowe alisema bado wanaendelea kuwasiliana na Jeshi la Polisi na kwamba, kama wataruhusiwa hawatasita kufanya operesheni hiyo katika mikoa hiyo.

Alisema ili kuhakikisha wanayafikia maeneo yote wanayoyakusudia katika ziara hiyo, wamejigawa katika makundi sita na kwamba, matatu kati yao, yatatumia usafiri wa helikopta na yaliyobaki usafiri wa majini na nchi kavu.

Mbowe alisema helikopta ya kwanza itatumiwa na viongozi wa chama, ambao watatembelea mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Manyara, Arusha, Singida na Dodoma.
Alisema katika ziara hiyo, viongozi hao watapita kwenye kila kata inayotarajia kufanya uchaguzi mdogo wa udiwani.

Mbowe alisema helikopta ya pili itazuru mikoa ya Mara, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Geita, Tabora, Kigoma, Katavi na Kagera na kwamba, katika maeneo yote itafanywa mikutano ya hadhara.

Alisema helikopta ya tatu itatembelea mikoa ya Ruvuma, Iringa, Mbeya, Morogoro na Rukwa.

Mbowe alisema watatumia fursa hiyo kutembelea Jimbo la Kalenga mkoani Iringa, lililokuwa likiwakilishwa bungeni na Dk. William Mgimwa, ambaye alifariki dunia nchini Afrika Kusini Januari Mosi, mwaka huu.

Alisema wakiwa jimboni humo, watafanya mambo makuu mawili; la kwanza likiwa ni kufanya mkutano wa hadhara.

Jambo la pili alisema litakuwa ni kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu Dk. Mgimwa, ambaye hadi anaaga dunia, alikuwa pia Waziri wa Fedha.

MALENGO YA OPERESHENI
Alisema operesheni hiyo imezingatia mwaka 2014 kuwa na historia ya matukio ya kisiasa nchini, ambayo chama kinahitaji kujipanga kukabiliana nayo.

Aliyataja matukio hayo kuwa ni pamoja na Bunge Maalumu la Katiba linalotarajiwa kuanza rasmi mwanzoni mwa mwezi ujao.

Hivyo, alisema chama kimeona kuwa kuna ulazima wa kuliandaa Taifa kwa ajili ya kulikabili tukio hilo.

Alisema matukio mengine ni uchaguzi wa serikali za mitaa na kura ya maoni, ambayo itapigwa na wananchi kuamua ama kuikubali au kuikataa rasimu ya pili ya katiba mpya.
Kutokana na hilo, Mbowe alisema wanatumaini kuwa daftari la kudumu la wapigakura litatumika katika kuendesha kura ya maoni.

Hivyo, alisema wameona ni lazima waliamshe Taifa kuhusu kujiandikisha katika daftari hilo.

“Katika operesheni yetu tutaliandaa taifa lisishiriki kwenye kura ya maoni kama daftari la wapigakura halitaboreshwa,” alisema Mbowe.

Alisema tangu mwaka 2010, daftari la kudumu la wapigakura halijaboreshwa.
Kutokana na hali hiyo, alisema itakuwa ni ndoto za serikali kufikiria kwamba Watanzania watarudi kuitumia katiba ya mwaka 1977 inayotumika hivi sasa baada ya kuwa tayari wamekwishaikataa.

“Nchi haitakalika. Tutaidai katiba mpya kwa taratibu nyingine. Hatutarudi kwenye katiba ya zamani,” alisema Mbowe.

Mbowe alisema matukio mengine ya kisiasa yanayotarajiwa kujiri mwaka huu, ni uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 27 nchini.

Alisema kati ya kata hizo, Chadema imesimamisha wagombea kwenye kata 26 baada ya mgombea wao katika Kata ya Mtae, mkoani Tanga kushindwa kurejesha fomu za kuomba kuwania kiti hicho katika mazingira ya kutatanisha.

Mbowe alisema katika mwaka huu pia kunatarajia kufanyika uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Kalenga kuziba nafasi iliyoachwa wazi kufuatia kifo cha Dk. Mgimwa.
Alisema pia katika mwaka huu watakuwa na uchaguzi wa ndani ya chama, hivyo wameona ulazima wa kuwaandaa wana-Chadema kushiriki uchaguzi huo.

Alisema pia Watanzania watakuwa na uchaguzi mkuu mwakani, hivyo wameamua kuutumia mwaka huu kukazia maandalizi kwa ajili ya ushiriki wao katika uchaguzi huo.
Mbowe alisema watatumia fursa hiyo kuibua kashfa na mambo yote yanayowakera wananchi katika maeneo yao.

Kwa mujibu wa Mbowe, operesheni hiyo ambayo itakuwa ya wiki mbili, itaendeshwa kwa njia ya mikutano ya hadhara na ya ndani.

No comments:

Post a Comment