MWENYEKITI wa taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amemkaribisha Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye kujiunga na chama chake ili kuendeleza mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa.
Mbowe alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati wa sherehe za ufunguzi wa jengo jipya la ibada zilizofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheli Usharika wa Lole Mwika na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na kanisa ambapo Sumaye alikuwa mgeni rasmi.
Alisema hoja ya rushwa inayozungumzwa na Sumaye ambayo CHADEMA imekuwa mstari wa mbele kuipiga vita ina msingi, hivyo viongozi wengine wanapaswa kumuunga mkono na kuliomba kanisa lizidi kuwaombea viongozi wa aina hiyo ili wazidi kupaza sauti zao bila hofu.
“Ndugu zangu hoja ya rushwa iliyozungumzwa mahali hapa na Sumaye ni hoja ya msingi sana, haki katika taifa hili ni bidhaa adimu na wale wanaotetea haki katika taifa hili wengine wanailipa kwa gharama ya maisha yao,” alisema.
Alisisitiza kuwa ni vyema viongozi wakawa na mipaka ya vyama vyao vya siasa na kuwa na lengo moja la kusimamia hatma ya taifa kwa kupigania haki bila uwoga ili kuepusha mateso kwa wananchi.
“Viongozi wote kama tukaamua kusimamia hii hoja bila ya kuona huyu yuko chama gani, yule yuko chama gani, tukafanya hili suala la rushwa ni la taifa, basi tunaweza kupiga hatua, na kama hatutasahau mipaka ya vyama vyetu hakika nchi hii bado wananchi wa kawaida wataendelea kuteseka sana,” alisema.
Mbowe aliomba kanisa lisaidie katika suala hilo ili kuepusha taifa kupasuka kutokana na viongozi kuweka itikadi mbele na kusahau kuwa siasa ni masuala yanayopita.
Alisema hivi sasa vyama vya siasa vimetafsiriwa kama vyombo vya kugombanisha watu, huku baadhi ya viongozi kwa makusudi wakisahau kuwa vyama vya siasa ni vyombo vya uchaguzi vinavyotumika kupata viongozi.
“Tunauana kwa mabomu, tunauana kwa risasi, tunafungana kwa ajili ya siasa, siasa ni kazi ya kupita, kama Mungu amemuandika mtu kuwa na uongozi atapata uongozi bila ya kujali yuko chama gani, kwa hiyo niombe kanisa lifanye suala la uchaguzi kuwa ajenda ya kudumu ya kanisa,” alisema.
Akizungumzia mwaka mpya 2014, Mbowe alisema ni mwaka wa kutisha kwa watu ambao wapo katika siasa adhimu (active politics) wanaoona namna siasa zinavyobadilika na kuwa ni mambo ya kutishia uhai wa watu.
“Huu ni mwaka wa majaribu makubwa na tunaliomba kanisa lisikae mbali, kanisa lina wajibu mkubwa wa kutusaidia wanasiasa maana tunapokuwa ndani ya nyumba za ibada kama hizi kwa kiwango fulani tunaheshimiana,” alisema.
No comments:
Post a Comment