Thursday, January 2, 2014

Asasi za kiraia zatangaza wajumbe Bunge la Katiba

Mitandao ya Asasi za kiraia nchini (Azaki), zimechagua wawakilishi 40 ambao majina yao yatapelekwa kwa Rais Jakaya Kikwete, kwa ajili ya uteuzi wa wabunge 20 wa Bunge Maalum la Katiba linalotarajia kufanyika Februari, mwaka huu. 

Asasi za kiraia nchini ambazo zinawakilisha makundi ya kikanda na kisekta, zimepewa nafasi 20 za uwakilishi katika Bunge hilo. 

Katika uchaguzi huo uliomalizika juzi saa 4:00 usiku mjini Dodoma na kusimamiwa na Jukwaa la Katiba nchini, zaidi ya wagombea 100 walijinadi na kupigiwa kura na wawakilishi wa Azaki kutoka mikoa yote 30 nchini.

Wapigakura hao ambao ni wawakilishi ya mitandao ya Azaki wa wilaya 140, mikoa 30 na kisekta 20, waliwachagua wawakilishi hao kwa kufuata kanda na uwakilishi wa kisekta.

Waliochaguliwa kuwakilisha sekta ya Utawala bora na Uwajibikaji na kura walizopata katika mabano ni Alban Marcossy (104) na Renatus Mkinga (78).
Sekta ya Haki za Watoto ni Seif Mahumbi na James Marenya ambao walifungana kwa kupata kura 47 kila mmoja.

Msimamizi wa uchaguzi huo, Deus Kibamba, aliwataja waliochaguliwa katika sekta ya Uchumi na Maendeleo kuwa ni Martina Kabisana (95) na Gerald Ruhere (64).
Kwa upande wa habari ni Mwandishi wa Kampuni ya New Habari 2006 Arodia Peter (108) na wa Kampuni ya Mwananchi Communication, Burhan Yakoub (75).
Kibamba alisema sekta ya wazee waliochaguliwa ni Charles Lwabulala (77) na Dk. Joseph Saqware (56).

Alitaja sekta nyingine kuwa ni Vijana ambayo waliochaguliwa ni Violet Edwin (58) na Jafari Yusuph (45) huku sekta ya Sheria na Haki za Binadamu wakichaguliwa Sarah Malingingwa (71) na Elias Mathibya (67).

Alisema Sekta ya Virusi vya Ukimwi na Ukimwi ni Alex Margery na Elita Chusi, ambao walifungana kwa kura 72 huku Sekta ya Jamii ni Happiness Sengi (66) na Dk. Peter Bujari (43). 

Mazingira na Maliasili waliochaguliwa ni Magreth Katanga (56) na Jecha Jecha (46), wakati Jinsia na Wanawake ni Gemma Akilimali (93) na Grace Mkumbwa (61).
Kwa upande wa kundi la uwakilishi wa kikanda, Kanda ya Kati ni Maliki Marupu (12) na Maendeleo Makoye (7) wakati Kanda ya Kaskazini ni Petro Ahham (9) na Saumu Swai (8). 

Alisema Kanda ya Magharibi waliochaguliwa ni Babyegeya Bitegeko (6) na Bihaga Simon (5) wakati Kanda ya Kusini ni Michael Malucha (5) na Sharifu Kombo (4) huku Kanda ya Pemba waliochaguliwa ni Mussa Kombo Mussa (4) na Fakih Hamad Ally (3). Kwa upande wa Nyanda za Juu Kusini, waliochaguliwa ni Paul Kita na Raphael Mtitu, wote wakiwa na kura saba kila mmoja.

Kibamba alisema kwa upande wa Kanda ya Ziwa waliochaguliwa ni Mariam Mkaka (13) na Nicas Nibengo (9) wakati Kanda ya Unguja ni Hassan Khamis Juma (4) na Hafidhi Hamid Soud (3) huku waliotoka Kanda ya Pwani ni Shaib Lipwata (9) na Sofia Mwakagenza (8).

Kibamba alisema majina hayo yanatarajiwa kuwasilishwa kwa Rais Kikwete kesho kabla ya saa 9:00 alasiri kwa ajili ya uchaguzi wa wabunge 20 watakaoingia katika Bunge Maalum la Katiba.

Akizungumza juzi jioni, Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi huo, Juma Nyumayo, alisema kamati hiyo imepokea malalamiko kutoka Kanda ya Unguja kuwa mmoja wa wawakilishi aliyechaguliwa ni mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa hilo.

Nyumayo alisema aliyekata rufaa wa Kanda ya Kaskazini alidai kuwapo kwa idadi kubwa ya kura kuliko wapiga kura.

“Tumepokea rufaa tatu kwa maandishi. Kanda ya Unguja kuna rufaa moja na Kanda ya Kaskazini rufaa moja, ambazo zote zitafanyiwa kazi,” alisema.
Alisema rufaa ya tatu ilikuwa ni kutoka Kanda ya Ziwa, lakini mrufani baadaye aliamua kujitoa.

Nyumayo alisema malalamiko hayo yatafanyiwa kazi na kisha kurejeshwa majibu kwa wajumbe wa mkutano huo wa uchaguzi. Akizungumza na waandishi wa habari, wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe, alisema kuwa makundi hayo yanatakiwa kuwasilisha kwa Rais orodha ya majina ya watu wasiopungua wanne na wasiozidi tisa na muda wa mwisho ni kesho.

Rais Kikwete Desemba 13, 2013 alitoa tangazo kwa mujibu wa kifungu kidogo cha (2A) cha kifungu cha 22 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 alialika kila kundi kutoka pande zote za Muungano kuwasilisha kwake majina kwa ajili ya kuzingatiwa kwenye uteuzi.

Akifafanua, alisema Bunge Maalum la Katiba lina makundi matatu, ambapo wabunge wote wa Jamhuri ya Muungano, wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na watu 201 kutoka kwenye makundi mbalimbali watakuwa wajumbe.
Wajumbe 20 watatoka kwenye taasisi zisizokuwa za kiserikali, nusu yao wakiwa ni wanawake na moja ya tatu wakitokea Zanzibar.

Pia watakuwapo wajumbe 20 kutoka taasisi zote za dini, wajumbe 42 kutoka vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu. Wajumbe wengine na idadi yao kwenye mabano ni Taasisi za Elimu ya Juu (20), makundi ya watu wenye ulemavu (20), vyama vya wafanyakazi (19), vyama vinavyowawakilisha wafugaji (10), vyama vinavyowawakilisha wavuvi (10) na vyama vya wakulima 20. 

No comments:

Post a Comment