- M4C Pamoja Daima yatikisa
- Mbowe anusurika ajalini
HARAKATI za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kujiimarisha kupitia operesheni mbalimbali wanazozifanya ikiwemo ya M4C Pamoja Daima zimeanza kuwatia hofu ya kung’oka madarakani wabunge na viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Makada hao wa CCM wakiwamo wabunge wa majimbo mbalimbali wameanza kufanya ziara kwenye majimbo yao ili kujinusuru na vumbi lililoachwa na CHADEMA huku wakikumbuka ziara kama hizo ndizo zilizosababisha chama chao kupata pigo kubwa katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika mwaka 2010.
Katika uchaguzi huo CHADEMA iliyokuwa na wabunge watano wa majimbo na sita wa viti maalumu ilifanikiwa kupata wabunge 23 wa majimbo na wengine wa viti maalumu pamoja na idadi kubwa ya madiwani.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa hofu hiyo imewafanya makada hao kuwataka viongozi wakuu wa CCM kuandaa ziara kwenye maeneo yaliyopitiwa na CHADEMA ili wasipate maumivu kwenye chaguzi za serikali za mitaa zitakazofanyika Oktoba mwaka huu na Uchaguzi Mkuu utakaofanyika mwakani.
Operesheni ya M4C Pamoja Daima inayofanywa na timu tatu za viongozi na makada wa CHADEMA zilizogawanyika kwenye maeneo mbalimbali zikitumia usafiri wa helikopta na magari zimeanza kulalamikiwa kwa kubeba gharama kubwa.
Wengi wa wanaojenga hoja ya gharama kubwa ni makada wa CCM wanaojificha, wanaohofia mustakabali wa chama chao, ambacho tangu uingie mfumo wa vyama vingi hakijapata upinzani mkali kama ilivyo hivi sasa.
CCM kwa muda mrefu imekuwa ikizoea kuona vyama vya upinzani vikianza harakati za kujiimarisha unapokaribia uchaguzi, tofauti na hivi sasa ambapo CHADEMA kimeonekana kuzika utamaduni huo.
Baadhi ya makada wa CCM wanadai gharama ya kukodisha helikopta moja kwa saa si chini ya sh milioni 2.5, hivyo kwa siku CHADEMA inatumia sh milioni 4.5 mpaka sita kwa helikopta moja.
Hoja inayojengwa na makada hao ni kuwa, gharama hizo zisitumike kwenye operesheni hiyo bali zipelekwe kuimarisha ofisi za wilaya, kata na matawi ambazo zitaimarisha zaidi CHADEMA.
Hata hivyo viongozi wa CHADEMA wameweka wazi kuwa CCM wanahofia kuimarisha CHADEMA, si gharama zinazotumiwa na chama hicho katika shughuli zake.
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa, kwa nyakati tofauti wamejinasibu kuwa operesheni hizo ndizo zitakazoiondoa CCM madarakani.
Viongozi hao walibainisha kuwa demokrasia ina gharama kubwa na chama chochote kinachozikwepa hakitafanikiwa kupambana na CCM.
Wakati hofu ikitawala kwa makada wa CCM, CHADEMA imeendelea na harakati zake ambapo jana Mbowe, Slaa na timu zao walikuwa maeneo tofauti.
Endelea.....
Endelea.....
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, amenusurika kifo baada ya gari alilokuwa akisafiria kutoka jijini Mwanza kwenda wilayani Ngara, Kagera kupata ajali.
Ajali hiyo ilitokea jana saa 6 mchana, umbali wa kilometa mbili kutoka Kata ya Katoro, Geita na inadaiwa kuwa gari alilokuwa akitumia limeharibika sehemu ya mbele.
Taarifa za uhakika kutoka eneo la tukio zimeeleza kwamba chanzo cha ajali hiyo iliyosababishwa na mwendesha pikipiki yenye namba za usajili T 212 BFR aliyefahamika kwa jina la Sayi Kahindi (32) mkulima, mwenyeji wa Kijiji cha Inyala kuingia ghafla barabarani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wakati ajali hiyo ikitokea alikuwa akielekea wilayani Ngara kwa ajili ya mikutano ya Operesheni M4C Pamoja Daima, iliyoanza hivi karibuni nchi nzima.
Inadaiwa kwamba, Mbowe katika safari hiyo alikuwa akitumia gari la Mbunge wa Ilemela, Highness Kiwia (CHADEMA) lenye namba za usajili T 217 CPB.
Baada ya ajali hiyo Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, Kilimanjaro alipata gari jingine lenye namba za usajili T 888 CGT Pajero, mali ya mkazi wa Katoro, aliyejulikana kwa jina la Mbanju, ambalo lilimpeleka Ngara anakoendelea na mikutano ya kukijenga chama wakati dereva na gari lililopata ajali vikipelekwa kituo cha polisi.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumapili, Mbowe alikiri kupata ajali hiyo lakini alisema yupo salama na alikuwa karibu kufika Ngara ambako alitarajiwa kuhutubia mkutano wa hadhara.
“Niko salama, nakaribia kufika Ngara kwenye mkutano ambapo nitaungana na msafara wa chopa unaotokea Kigoma ukiwa na Makamu wa Zanzibar, Lema na Mnyika,” alisema.
Naye Mkuu wa Usalama Barabarani mkoani Geita, John Mfinanga na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Geita, Kamanda Bwire, walithibitisha kuwepo kwa ajali hiyo huku wakiainisha kuwa wanaendelea na uchunguzi wa chanzo cha ajali hiyo.
“Nimezungumza na mwenyekiti mwenyewe, Mbowe, ameniambia ni kweli alipata ajali umbali wa kilometa mbili hivi kutoka mji wa Katoro akielekea Chato.
“Gari alilokuwa akisafiria limeharibika vibaya maeneo ya mbele. Pikipiki nayo imeharibika sana… wakati nawasiliana naye alikuwa ameshaondoka eneo la tukio akielekea Bihalamuro kwenda Ngara,” alisema Mbunge wa Nyamagana, Ezekiah Wenje.
Leo Mbowe anatarajiwa kutua Geita kwa helikopta ili kuhutubia mikutano ya hadhara katika mwendelezo wa shughuli za kukijenga chama chake.
Lissu awavaa Lowassa, Chenge
Mwanasheria Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu na Katibu Mkuu wa BAVICHA, Deogratius Munishi, wamewataka makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaokabiliwa na tuhuma za ufisadi, Edward Lowassa na Andrew Chenge, kuacha kutumia kigezo cha udini kutaka kuungwa mkono kwenye harakati zao za kukimbilia Ikulu.
Lissu na Munishi walitoa kauli hizo wakati wakimnadi mgombea udiwani wa Kata ya Sombetini, Ally Bananga, kwenye viwanja vya Ngusero.
Lissu alisema kuwa baada ya makada wa CCM kuona hawana sifa za uongozi kutokana na kuwa si waadilifu wala wasafi kulingana na tuhuma za ufisadi zinazowaandama, wameamua kukimbilia makanisani, wakiwashawishi viongozi wa dini wawaunge mkono kwa kigezo kuwa ni Wakristo wenzao.
“Kuna makada wengine wa CCM nao wanazunguka huko misikitini wakisema hii ni zamu yetu sisi Waislamu, hivyo anashawishi wamchague kwa kigezo cha Uislamu tu. Hawa watu wanasahau dini si kigezo wala sifa ya uongozi, tuwakataeni, sijui wanalipeleka wapi hili taifa, zaidi wanatutafutia machafuko, hawatufai wote hawa,” alisema Lissu.
Akizungumzia muswada wa mabadiliko ya Katiba, Lissu alisema kuwa katiba inasema kuwa nchi ni moja lakini kwa sasa kuna Maamiri Jeshi wawili, ambao mmoja ni Mwenyekiti wa CCM, Kikwete na mwingine ni Makamu wake, Dk. Ali Mohamed Shein, jambo alilosema kuwa ni hatari sana hasa ikitokea wakitofautiana na kupishana kauli ilhali wote wana majeshi.
Kwa upande wake Katibu wa BAVICHA, Munishi, alisema kuwa dawa za kulevya zimeathiri kwa kiasi kikubwa wananchi hivyo vita yake inapaswa kuwa ya dhahiri na ya dhati ili kuepusha madhara zaidi, hasa kwa vijana ambao ndio waathirika wakubwa.
“Asilimia 35 ya wananchi wa Tanzania ni vijana ambao wengi wao kwa sasa wanaangamizwa na dawa za kulevya, lakini inasikitisha Rais wetu Kikwete alitutangazia kuwa anayo majina ya wauza dawa lakini hayataji, kayakumbatia tu Ikulu, kama huu si usanii ni nini? Sasa tunamtaka atueleze hao wauza dawa za kulevya ni kina nani, tofauti na hapo naye ni mshirika wao, ndiyo maana hawataji,” alisema Munishi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa BAVICHA, John Heche, alisema kuwa endapo serikali haitafanyia maboresho daftari la kudumu la wapiga kura kabla zoezi la kukusanya maoni ya katiba halijafanyika, watarusha helikopta 10 kila kanda ya chama hicho itakuwa na yake ili kuhamasisha wananchi wasijitokeze kutoa maoni.
Alisema kuwa haiwezekani serikali kucheza na haki za wananchi wake kiasi hicho, kwani mara ya mwisho daftari hilo kuboreshwa ni mwaka 2010, jambo alilosema kuwa linawanyima haki Watanzania waliotimiza umri wa kupiga kura kama Katiba ya nchi inavyotaka.
Pia aliwataka wananchi hao kumchagua mgombea aliyesimamishwa na CHADEMA, Bananga, awe diwani wao ili washirikiane kupigania na kusimamia maendeleo ya kata yao, ambayo imekaa zaidi ya mwaka mmoja bila kuwa na diwani.
“Kama mnaridhika na umeme wa mgawo mchague mgombea wa CCM, kama mnaridhishwa na elimu inayotolewa kwa watoto na wadogo zenu kwenye shule za serikali chagueni mgombea wa CCM. Kama mnaridhishwa na mgawanyo wa rasilimali ya utalii, madini na gesi mchagueni mgombea wa CCM, lakini kama mnataka mchapa kazi, mpigania haki za wanyonge, mpinga ufisadi na rushwa, mchagueni Bananga kwa maendeleo ya kata yenu,” alisema Heche huku wananchi hao wakipaza sauti kuwa wanamtaka Bananga.
No comments:
Post a Comment