Sunday, January 26, 2014

CHADEMA yavilipua CCM, CUF Zanzibar

WAKATI Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) ikitimiza miaka mitatu, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema mfumo wa serikali hiyo Zanzibar umeshindwa kudhibiti ufisadi na kuua dhana ya demokrasia ya vyama vingi.
Hayo yalisemwa jana na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Zanzibar, Hamad Mussa Yussuf, alipohutubia mkutano wa kampeni za uchagzu mdogo wa Kiembesamaki zilizofanyika uwanja wa Kiembesamaki na kumnadi mgombea wa chama hicho, Hasim Juma Issa.
Hamad alisema tangu kupatikana kwa SUK, dhima ya upinzani imepotea na kukithiri kwa  vitendo vya ubadhirifu na ufisadi, huku Baraza la Wawakilishi likishindwa kuisimamia serikali katika utekelezaji wa ripoti za uchunguzi zinazoikaba serikali.
“Baraza la Wawakilishi Zanzibar limekosa meno, halifanyi kazi kama Bunge la Muungano ili kuisimamia SMZ, kinahitajika chama mbadala kuingia kwenye Baraza la Wawakilishi  haraka kabla mambo hayajaenda mrama,” alisema Hamad.
Alizitaja ripoti za ubadhirifu wa fedha za umma katika Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco), Baraza la Manispaa ya Mji wa Zanzibar (ZMC) mbali na ripoti za uchunguzi wa uuzaji wa majengo ya serikali yaliouzwa kwa bei ya kutupwa kinyume cha sheria.
Naibu katibu mkuu huyo alisema vyama vya CCM na CUF vimepoteza imani kwa wananchi na sasa ni wakati sahihi kwa Zanzibar kupatikana chama kingine kitakachopigania masilahi ya wananchi na kuibana serikali.
Vyama vya CCM na CUF kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ndivyo vinavyounda serikali ya umoja wa kitaifa Zanzibar kutokana na kupata viti vya uwakilishi na kura za urais kwa asilimia 10.
Kwa upande wake mgombea wa uwakilishi Hasim Juma Issa, alisema iwapo atachaguliwa atajenga hospitali itakayohudumia wananchi, usambazaji wa maji safi na salama na kujenga barabara kwa kiwango cha lami.
Alisema wabunge na wawakilishi wa CUF wameshindwa kutumia ruzuku ya maendeleo ya jimbo na idadi kubwa ya wawakilishi na wabunge wamelazimika kufanya kazi kwenye mikoba kwa kushindwa kujenga ofisi huku wakilipwa sh milioni 25 na sh milioni 10 wanazolipwa wawakilishi.

No comments:

Post a Comment