Sunday, January 26, 2014

Lissu, Heche washupalia ujangili

MWANASHERIA Mkuu wa CHADEMA, Tundu Lissu, amedai kwamba kitendo cha serikali ya Rais Jakaya Kikwete kutumia majeshi ya ulinzi kufanya operesheni za kiraia kilikuwa ni uvunjifu wa Katiba na ni kosa ambalo Bunge lilitakiwa kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye.
Akizungumza katika mikutano ya hadhara iliyofanyika jana katika maeneo ya Mabogini (Moshi Vijijini), Mererani, Mbuguni na Sombetini-Arusha, Lisu akitumia mfano wa Operesheni Tokomeza Ujangili ambayo askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania walitumika.
“Tanzania ingekuwa na Bunge linalosimamia wananchi wake, rais angepigiwa kura ya kutokuwa na imani naye… ni makosa kutumia wanajeshi kufanya operesheni za kiraia. Wanajeshi wamefundishwa kuua.
“Ni tofauti na askari polisi ambao wamefundishwa kulinda raia na mali zao, ambapo ikiwalazimu sana wanatumia mabomu ya machozi kutuliza ghasia na kupiga risasi ambazo hazitamuua mtu.
“Wanajeshi wanatumika pale ambapo kuna uvamizi wa kutoka nje au kuna uasi wa kiraia kama ilivyo huko Sudan Kusini hivi sasa.
“Ujangili unaofanywa tena na watu wengine wakubwa kutoka ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wanaojulikana kwa majina si uasi wa raia wala hatujaona uvamizi wa kutoka nje, kwanini rais alitumia majeshi kwenye operesheni hiyo ya kiraia? Watanzania wanahoji kwa nini rais ametumia majeshi kutesa na kuua raia?” alihoji Lisu.
Naye Mwenyekiti wa BAVICHA, John  Heche, aliitaka serikali itoe kauli kwa Watanzania kwa nini hadi sasa watu wakubwa walioko serikalini na ndani ya CCM wanaotuhumiwa kwa ujangili hawajakamatwa huku serikali ikiendesha operesheni iliyoumiza na kuua watu wasiokuwa na hatia.
“Waliouawa si majangili, wameuawa wananchi wa kawaida, wakulima na wafugaji wasiokuwa na kosa lolote, kwa nini hadi sasa serikali hii kama kweli inataka kukomesha ujangili na kufuta kabisa mtandao huo unaohatarisha maliasili zetu haijawakamata vigogo waliotajwa bungeni kwa majina yao kwamba wanahusika na kumaliza tembo wetu.
“Hadi leo serikali haijamkamata na kumhoji kiongozi wa CCM aliyetajwa kwa jina ndani ya Bunge kuwa anahusika na ujangili, mwingine kampuni yake imehusika katika kusafirisha meno ya tembo, hivyo ni wale wale, lakini wanatamba barabarani wakiua wananchi maskini,” alisema Heche.

No comments:

Post a Comment