Tuesday, January 21, 2014

CHADEMA wazindua kampeni Sombetini kwa mbwembwe

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimezindua kampeni zake za udiwani kwenye Kata ya Sombetini jijini hapa kwa kulitaka Jeshi la Polisi kutimiza wajibu wao wa kulinda usalama wa raia na kuonya kuwa hawatakuwa tayari kuona wanachama wao wakiumizwa kama ilivyotokeaa kwenye chaguzi zilizopita.

Aidha, kimewataka wanachama na wapenzi wa chama hicho wasiharibu wala kung’oa mabango na benderea za vyama vingine, badala yake hasira zao wazihamishie siku ya kupiga kura kwa kuhakikisha wanahamasisha wananchi wengi wakampigie kura mgombea wa CHADEMA, Ally Bananga, ili aibuke na ushindi wa kishindo.

Kauli hiyo ilitolewa juzi na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, alipokuwa akizindua kampeni hizo kwenye viwanja vya soko la Mbauda, ambapo umati mkubwa wa watu ulijitokeza wakiwemo viongozi na makada mbalimbali wa chama hicho pamoja na aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Alphonce Mawazo.

Alisema siku zote CHADEMA wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kampeni zinazofuata taratibu za sheria, lakini vyama vingine hasa CCM, kimekuwa kikitumia ubabe, ikiwemo kuwapiga wale wanaoonekana kuishabikia CHADEMA na kwamba vyombo vya usalama vimekuwa vikikaa kimya bila kuwachukulia hatua ya kisheria.

“Bananga ukiwa jukwaani ukasikia mmoja wetu amepigwa au kaumizwa funga mkutano, ondokeni wote mlioko mkutanoni mwende mkamtafute huyo aliyempiga mwenzetu mpaka mumpate, ila mtumie busara kuhakikisha mnamfikisha kituo cha polisi,” alisema Lema huku akishangiliwa.

Aliyekuwa diwani wa kata hiyo, Mawazo ambaye alijivua gamba kwa kujitoa CCM na kuvaa gwanda kwa kujiunga na CHADEMA katikati ya mwaka 2012, aliwatoa machozi wananchi waliojitokeza kwenye mkutano huo baada ya kupiga magoti akiomba wamsamehe kwa uamuzi wake huo.

Alisema ingawa uamuzi huo ni sahihi, lakini anajua uliwaumiza baadhi ya wananchi wake waliokuwa wakimtegemea awalipie ada za shule na wale aliokuwa akiwatetea pale walipokuwa wakikandamizwa katika kupatiwa huduma mbalimbali.

Aliwaomba wamchague Bananga aliyedai kuwa ni mtetezi wa wanyonge kama alivyokuwa yeye.

Ilikuwa ni sahihi kuondoka CCM, nilikuwa nachukiwa na kupingwa kutokana na misimamo yangu ya kuwatetea wanyonge,” alisema Mawazo.

Kwa upande wake Bananga aliwaomba wananchi hao wamchague ili ashirikiane nao katika kuhakikisha wanasimamia maendeleo ya kata yao pamoja na kuhakikisha huduma muhimu zinapatikana na fedha za miradi zinazoletwa kwenye kata hiyo zinatumika bila kuchakachuliwa.

No comments:

Post a Comment