WAKATI mashabiki na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakihoji uamuzi wa Kamati Kuu ya chama hicho kumvua nafasi zote za uongozi Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, amewasilisha utetezi wake.
Zitto licha ya kuvuliwa vyeo vyote, pia alipewa siku 14 za kujieleza kwanini asifukuzwe uanachama kwa tuhuma za kukihujumu, kukisaliti chama chake na viongozi wenzake.
Taarifa za uhakika zilizolifikia Tanzania Daima Jumatano jana, zilieleza kuwa Zitto aliwasilisha barua hiyo ya utetezi makao makuu ya CHADEMA Mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam mchana na dereva wake aliyefahamika kwa jina moja la Patrick.
Mbali ya Zitto, wengine waliopewa barua ya kujieleza ni aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitilla Mkumbo na Samson Mwigamba, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha.
Tanzania Daima Jumatano, imedokezwa kuwa uchambuzi uliofanywa na wanasheria wa Zitto kupitia makosa 11 aliyotuhumiwa, wamebaini 10 yanajirudia.
Inaelezwa kuwa kosa kuu lililoainishwa na wanasheria hao ni kwenda kinyume na maadili ya chama, kitendo kilichotamkwa kuwa ni uhaini.
Kaimu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Victor Kimesera, alipoulizwa juu ya Zitto kuwasilisha barua ya utetezi, alisema hana taarifa za jambo hilo kwakuwa aliwahi kuondoka ofisini kabla ya saa sita mchana.
“Kama barua imefika itakuwa imeelekezwa kwa Katibu Mkuu na hakuna mtu mwingine wa kuifungua mpaka niione kwa kuwa mimi ndiyo ninakaimu nafasi hiyo kwa sasa, lakini ngoja niwasiliane na ofisini nitakupa jibu,” alisema Kimesera.
Hata hivyo, alipotafutwa baadae Kimesera hakuweza kutoa jibu, na hata simu yake ilipopigwa kwa ajili ya ufafanuzi haikupokewa.
Tanzania Daima Jumatano, iliwasiliana na Zitto kujua suala hilo la kuwasilisha utetezi wake, lakini hakuwa tayari kulizungumzia.
Novemba 22, mwaka huu, Zitto, Dk. Mkumbo na Mwigamba walivuliwa nyadhifa zao na walitakiwa kujibu makosa 11 yaliyoainishwa na Kamati Kuu ya CHADEMA kwa ajili ya kutetea uanachama wao.
Uamuzi huo ulileta msuguano mkubwa ndani ya chama hicho ambapo baadhi ya wanachama walipinga hatua hiyo wakidai itakiumiza chama.
Kutokana na uamuzi huo, viongozi wa CHADEMA Mkoa wa Kigoma waliandika barua makao makuu wakitaka ziara ya Katibu Mkuu, Dk. Willibrod Slaa katika mkoa huo iahirishwe kwa madai kuwa usalama si mzuri.
Hata hivyo, CHADEMA iliamua kuendelea na ziara hiyo ambapo Dk. Slaa yupo mkoani humo akifanya mikutano na shughuli za kuimarisha chama hicho.
Dk. Slaa aunguruma kwa Zitto
Wakati Zitto akiwasilisha barua yake ya utetezi, Katibu Mkuu, Dk. Slaa, amekifananisha chama chake na daktari asiyeweza kuacha saratani kuenea ndani ya mwili na kumuua mgonjwa.
Akihutubia wananchi wa Kijiji cha Nyarubanda, Jimbo la Kigoma Kaskazini, wilayani Kigoma jana, ikiwa ni siku yake ya sita tangu aanze ziara ya kuimarisha na kukagua uhai wa chama, Dk. Slaa alisema wanachama na wananchi wanapaswa kutembea kifua mbele wanapoona ipo taasisi katika nchi hii inaweza kusimamia misingi ya uwajibikaji.
Aliwataka wanachama kusimama na chama chao kinaposimamia uwajibikaji huku akibainisha kuwa baadhi ya viongozi waliojiuzulu hivi karibuni wamempigia simu wakiomba kurejea kwenye chama hicho kwa sababu ‘manufaa’ waliyokuwa wakiyatafuta kwa kujiuzulu, wameyapata.
Akijibu maswali ya baadhi ya wananchi waliohudhuria mkutano huo, Dk. Slaa alifafanua kuwa makada wa chama hicho waliovuliwa nafasi za uongozi ndani ya chama hicho hivi karibuni, hawajafukuzwa uanachama na ubunge kama inavyopotoshwa, bali hatua zilizochukuliwa dhidi yao ilikuwa muhimu kwa ajili ya kuepusha athari zaidi kwa chama.
“Daktari makini akibaini ugonjwa wa kansa kwa mgonjwa wake atahakikisha anachukua hatua za haraka…mathalani kansa ikiwa hapa chini mguuni, hatua za haraka ni kukata eneo husika haraka kabla kansa hiyo haijasambaa mwili mzima. Wananchi wangu najua kuna maneno mengi sana vijiweni na mitaani, lakini watu makini mnajua kuwa chama chenu hakiwezi kumuonea mtu.
“Waliovuliwa nafasi za uongozi wala si Zitto peke yake, yupo Dk. Kitila Mkumbo na Samsoni Mwigamba aliyekuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha. Hatua zilizochukuliwa ilikuwa ni muhimu kama ilivyo kwa daktari kumnusuru mgonjwa kansa. Hatua za kuwavua nafasi zao za uongozi ndani ya chama ilikuwa ni kuepusha athari zaidi huku wakipewa nafasi ya kujitetea,” alisema.
Akijibu swali la mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Felix, kuhusu uamuzi wa Kamati Kuu ya kuwavua uongozi akina Zitto na wenzake, Dk. Slaa alisema makada hao wamepewa siku 14 za kujitetea dhidi ya tuhuma za kimaadili zinazowakabili za kuvunja katiba ya chama hicho, na kwamba suala hilo halijafikia mwisho.
“Sasa kuna watu wanalalamika tu bila kujua hasa nini kimetokea, hawajui hata tuhuma zinazowakabili. Nashukuru wewe umeuliza kutaka kujua. Wengine wameshafikia hitimisho kwamba mbunge wenu kaondolewa. Kuweni wavumilivu, vikao vya chama chenu vitalifikisha suala hili mwisho. Hakuna mtu yeyote anaweza kuonewa kwa sababu tunaendesha mambo yetu kwa kufuata katiba.
“CHADEMA haijawahi kutetereka kila inapochukua maamuzi yake. Kwa sababu hatufanyi hila wala kupindisha pindisha mambo. Mtakumbuka tulipowawajibisha madiwani watano kule Arusha…pamoja na kwamba tunapambana kweli kuongeza madiwani nchi nzima, lakini wale walipoonesha utovu wa kimaadili, hatukumung’unya maneno. Tulichukua hatua.
“Nashukuru kuna watu wanasema hawaumizi kichwa kwa sababu ya watu au mtu. Kama wewe ulijiunga CHADEMA kwa sababu ya Slaa au Mbowe, utakuwa haujui umuhimu wako ndani ya taasisi hii. Kitu kikubwa ndani ya chama ni katiba, kikubwa ni kanuni, maadili ya chama si mtu, si Mbowe wala Slaa,” alisema.
Mvua yakatisha mkutano
Wakati Dk. Slaa akiendelea kuhutubia akiwa amefikia hatua ya kujibu maswali na hoja mbalimbali za wananchi, mvua iliyotanguliwa na ukungu na mawingu mazito, ilianza kunyesha kijijini hapo ambapo wananchi walilazimika kujifunika kwa miamvuli na wengine kujificha upenuni mwa nyumba zilizokuwa pembeni mwa eneo la mkutano.
Jitihada za Dk. Slaa kuitikia matakwa ya wananchi waliomsihi aendelee kuhutubia na wako tayari kumsikiliza, hazikufua dafu baada ya mvua kuzidi kuwa kubwa, hali iliyomlazimu kufunga mkutano huo na kuanza safari ya kuelekea mkutano wa pili eneo la Kidahwe, lakini pia mkutano huo ulishindikana kutokana na mvua hiyo kuendelea kunyesha.
Leo Dk. Slaa, ataendelea na ziara yake ambapo atafanya mkutano wa hadhara pamoja na mikutano ya ndani Wilaya ya Kigoma Mjini, ikiwa ni siku ya 7 tangu aingie mkoani Kigoma akitokea Mkoa wa Shinyanga alikoanzia ziara yake Desemba 4, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment