December 7 /
2013.
Chadema Students’ Organization (CHASO) ni umoja wa
wanafunzi wa elimu ya juu wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo iliyo
chini ya Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA) taifa iliyoanzishwa chini ya kanuni
ya Mabaraza ya chama katika kipengele 7.8.2(a) cha katiba ya chadema
Msimamo:
Umoja wa wanafunzi wa vyuo (vikuu) wanachadema / Chadema Students
Organisation(CHASO) IRINGA, unatamka rasmi wazi kwamba tunaunga mkono kwa
asilimia zote maamuzi yaliyotolewa na kamati kuu ya chama Makao makuu ya chama
cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) kuhusiana na kuvuliwa nyadhifa za uongozi
kwa baadhi ya viongozi ndani ya chama.
Tukiwa ni taasisi ya Chama inayoundwa na wanafunzi
wa elimu ya juu Mkoani Iringa, tunakubaliana moja kwa moja na maamuzi ya chama,
pia tunaungana na wenzetu wa CHASO Kanda ya Dar-es-salaam kulaani vikali
vikundi vya kihuni vinavyotumia vibaya jina la CHASO
kutoa matamko yanayopingana na maamuzi ya kamati kuu
ya chama; kwani kama weledi ni wazi kwamba wanaelewa taratibu kamili
zinazopasika kufikia hatima mahususi.
Maamuzi ya kamati kuu ya chama yanaonesha wazi na
dhahiri kwamba Chama cha demokrasia na maendeleo(CHADEMA) ni chama kipevu yaani
kilichokomaa na chenye misimamo yake: kisichoogopa Umaarfu wa Mtu bali ni chama
kinachosimamia na kufuata misingi ya kikanuni na taratibu (katiba)
iliyojiwekea.
Tunawaomba Watanzania kutoamini katika ushabiki wa
kisiasa unaoendelea ama kutokuwa washabiki wa umaarufu wa mtu fulani ama
kikundi fulani cha watu, katika kufikia maamuzi juu ya suala lolote katika
jamii; pia tuwe wafuatiliaji na waelewa kwa kina juu ya mambo yanayohusika ili
tuweze kufikia maamuzi sahihi bila upotofu (kupotoshwa).
Chama cha Demokrasia na Maendeleo kimesimamia dhana
ya uwajibikaji katika ngazi zote bila kuangalia ama kuogopa nyadhifa au nafasi
ya mtu, bali kuhakikisha utaratibu unafuatwa katika kufikia maamuzi bila woga,
pasipo kuathiri matakwa ya kikatiba.
Watanzania wote kwa ujumla: wasomi kama dira ya
jamii huu ni wakati ambao tunatakiwa kutumia uledi na busara katika kuangalia
mambo(uchambuzi) kwa upeo mpevu. Ni rai kwetu kwamba si vema kutoa shutuma
dhidi ya chama bila kufuatilia ama kuelewa taratibu na kanuni (katiba)
zinazopasika katika kufikia maamuzi sahihi. Maamuzi sahihi sio lazima
yamfurahishe kila mtu bali kulinda maslahi ya Chama na Umma kwa ujumla wake.
Watanzania hatupaswi kukurupuka kiushabiki na hurka
binafsi/mihemko ama jazba na gadhabu kwani kwa kufanya hivyo tutawapa nafasi
watu wenye hinda katika gurudumu la mabadiliko tunayoyaelekea hivyo tunapaswa
kuwa makini.
Kimsingi tunatakiwa kuwa watu wenye Mantiki na
upembuzi yakinifu katika kufikia maamuzi kwa kuzingatia uhalisia wa dhana ya
uwajibikaji; hivyo basi, katika kuyaelewa mambo na tufanye tafiti za kina ili
kuweza kufikia maamuzi ya kuamini watu wengine katika usahihi wake, hivyo
kutozipa nafasi hisia za propaganda za mamluki.
Tunawaomba Watanzania wote katika makundi
mbalimbali, kuondokana na dhana ya ushabiki katika mambo ya msingi kwani mpango
wa Chadema ni kuangalia na kulinda maslahi ya Umma
na siyo kujenga jina ama umaarufu wa mtu mmoja
mmoja, pia chama siyo sehemu ya malumbano; hivyo shauku yetu ni kujenga
wanachama Imara na siyo kupata mashabiki kabambe. Chadema itaendelea kuwa
chemchemi ya Ukombozi wa Taifa na ujenzi wa viongozi wenye nidhamu, haki na
uwajibikaji.
Pia tutumie fursa hii kuwaonya watu wanaotumiwa
kusambaza propaganda zenye lengo la kuendeleza marumbano yasiyo na msingi.
Mwitikio wa vyama vya siasa nchini umekuwa ni
watofauti kwa kuwa vinara wa kuleta mkanganyiko baina ya watanzania na uvumi wa
propaganda; swali rahisi la kujiuliza wana maslahi gani juu ya maamuzi ya CHADEMA
ama mtu yeyote ndani ya CHADEMA?, pia tunawataka watanzania waelewe kwamba
malengo ya timu (wachezaji katika timu ni kuhakikisha wanafunga goli ili kupata
ushindi mchezaji anayepiga chenga nyingi na kukimbia na mpira mpaka nje ya
uwanja anakuwa hafai anapaswa kukaa benchi).
Tunawaomba watanzania tushikamane katika kipindi
hiki cha mpito, tukielewa ya kwamba tunapaswa kuwa makini na propaganda
zinazofanywa na makundi ya watu wenye lengo baya la kurudisha nguvu ya harakati
dhidi ya mabadiliko tunayoyakusudia, kwani kila mapinduzi au mageuzi yanakwenda
na usaliti. Chadema kitaenzi mawazo na mchango mzuri wa mtu yeyote mwenye
mapenzi mema na chama kwa maslahi ya Umma.
MUNGU IBARIKI TANZANIA, MUNGU IBARIKI
CHADEMA.
TIMOTHEO J. MKANYIA..............MWENYEKITIKITI
CHASO IRINGA 0713739683
ANDEMBWISYE ISRAEL…………………….KATIBU CHASO IRINGA
0764969838
MICHAEL NOEL…………………KATIBU MWENEZI CHASO IRINGA
0716746442
MWENYEKITI CHASO
No comments:
Post a Comment