Wednesday, December 11, 2013

Mbowe: Muulizeni Zitto nilikomtoa

MWENYETI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe, amewataka wanachama wa chama hicho wamuulize Mbunge Kigoma Kaskazini Zitto Kabwe wapi alikomtoa hadi kufikia ngazi na hadhi aliyonayo sasa katika medani ya siasa nchini.
Mbowe alitoa kauli hiyo jana katika kongamano la miaka 52 ya Uhuru wa Tanzania Bara, lililoandaliwa na Umoja wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu (Chaso) kwa kushirikiana na Baraza la Vijana la Chama hicho (BAVICHA)
Katika kongamano hilo lililofanyika katika Hoteli ya Land Mark, Mbowe ambaye alianza kwa kutaja historia yake kama mwasisi kijana wa CHADEMA na mwenyekiti wa kwanza, alisema mwaka 2003 akiwa katika harakati za kukijenga chama, alipita katika vyuo mbalimbali ili kupata vijana wasomi wajiunge na CHADEMA na ndipo alipompata Zitto, akiwa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
“Nikiwa katika harakati zangu za kukijenga chama, nilipita Chuo Kikuu cha Dar es Salaam …nilibahatika kuwapata kina John Mrema, Halima Mdee, Zitto Kabwe, John Mnyika wakiwa viongozi ambao walipenda siasa ya mabadiliko, nami nikaondoka nao bila ya kusita,” alisema.
Alisema nia ya kuwachukua vijana hao ni kujenga chama kama taasisi ili kisonge mbele tofauti na ilivyo sasa na siyo kujenga jina la mtu kama watu wanavyotaka iwe au wanavyodhani.
Mbowe alisema akiwa na vijana hao pamoja na viongozi wengine, walifanya kazi kama timu ili kuhakikisha wanakiingiza chama hicho Ikulu, akiamini kuwa asingeliweza peke yake kukipeleka mbele chama hicho.
Aliwataja viongozi aliowachukua kutoka katika vyama vingine vya siasa kuwa ni pamoja na Mkurugezi wa Fedha wa chama hicho, Antony Komu, Tundu Lissu, Mabere Marando ambao walitoka NCCR – Mageuzi.
Wengine ni Godbless Lema, Saidi Arfi na Mchungaji Peter Msigwa ambao walikuwa TLP na Ezekia Wenje aliyetoka Chama cha Mapinduzi (CCM), akiwa mwenyekiti wa tawi moja la chama hicho huku Mwanza.
Alisema safari ya kukijenga chama sio lelemama kwani ni sawa na treni inayotoka Dar es Salaam kuelekekea Kigoma huku akiamini wote watafiki, lakini imekuwa tofauti kwani wapo walioshuka njiani.
“Safari yetu ya Kigoma toka Dar es Salaam ilikuwa ndefu sana … wapo walioshuka katika kituo cha kwanza tu Pugu, wengine Morogogo na vituo vingine vilivyofuata na kupata vilevile lakini tutafika tu,” alisema.
Akitoa historia fupi ya maisha yake katika siasa, Mbowe alisema aliingia akiwa kijana mdogo muasisi ambaye alipata nafasi ya kukiongoza chama kama mwenyekiti wa kwanza wa vijana, baadaye kupata nafasi mbalimbali ikiwamo uenyekiti.
Alisema aliingia katika chama hicho na kuchanguliwa kuwa kiongozi, lengo likiwa kufanya mabadiliko kwa vitendo na si kwenda kupata faida kama watu wengine wanavyofikiria.
“Lakini nilifanya kazi yangu ya kuijenga CHADEMA hatua kwa hatua kwa maana nyingine nimefanya kazi ya chama kwa miaka 23 sasa bila kulipwa mshahara wowote kwa sababu mimi ni mfanyabiashara,” alisema.
Alisema chama akitatoa maamuzi ya kumwonea mtu yeyote bali kitamhukumu mtu kutokana na makosa yake.
Dk. Slaa aitikisa Kigoma
Wakati Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa akiwasili mjini Kigoma kwa ziara ya kukagua na kuimarisha uhai wa chama, hali ya ulinzi katika mikutano imeimarishwa kwa ajili ya kudhibiti vurugu zinazopenyezwa na watu wanaotumia jina la Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe.
Dk. Slaa alipata mapokezi mazito akiwa na msafara wa magari zaidi ya 22, pikipiki 150, magari manne ya polisi na ulinzi umeimarishwa mara dufu.
Kabla ya kuwasili mjini Kigoma, Dk. Slaa alifanya mkutano katika eneo la Janda na Mnanila, katika Jimbo la Manyovu, Wilaya ya Buhingwe, ikiwa ni siku yake ya tano tangu aingie mkoa wa Kigoma, akitokea Shinyanga.
Dk. Slaa alihoji matunda ya uhuru ‘kumilikiwa’ na kikundi kidogo cha watu wanaotumia dhamana za uongozi kufanya ufisadi unaoangamiza matumaini ya Watanzania.
Alisema kuwa wakati nchi ikifikisha miaka 52 tangu kupata uhuru Desemba 9, 1961, Watanzania wengi hawana kitu cha kusherehekea kwa sababu malengo ya mapambano ya kumwondoa mkoloni yamefifishwa na watu walioko kwenye dhamana ya uongozi, kiasi kwamba hata maadui waliotangazwa wakati wa uhuru badala ya kupungua, wameongezeka.
“Ndugu zangu hata ninyi hapa mmekubali kuwa miaka 52 baada ya uhuru maadui wameongezeka na bila woga mmesema ufisadi ni adui aliyeongezeka. Hivyo katika wale maadui watatu wa taifa waliotangazwa na Mwalimu Julius Nyerere kuwa tunapaswa kupambana nao na kuwatokomeza, yaani ujinga, maradhi na umaskini, ameongezeka adui ufisadi.
“Yaani hatujamalizana na ujinga, hatujamalizana na umaskini, hatujamalizana na maradhi, viongozi wetu kutokana na ulafi na ubinafsi wao, wametuongezea adui ufisadi.
“Huyu sasa amekuwa ndiye msingi wa maadui wote, adui umaskini anasaidiwa kuendelea kwa sababu ya ufisadi, adui ujinga anasaidiwa kuishi kwa sababu ya ufisadi, halikadhalika adui maradhi,” alisema Dk. Slaa kijijini Janda.
Dk. Slaa aliyewasili jimbo la Manyovu akitokea jimbo la Kasulu mjini, alisema kuwa miaka 52 baada ya uhuru Watanzania waliokuwa na matumaini ya kujitawala, hawana uhakika wa kusherehekea kwa sababu madhira wanayokabiliana nayo sasa mengine hata wakoloni hawakufanya kwa raia.
“Wananchi wenzangu wa Mnanila, wazee wetu hawakupambana kumwondoa mkoloni Mwingereza kwa sababu ya rangi yake, ilikuwa ni kwa sababu waliona wazi kabisa kuwa alikuwa ameshindwa kuondoa umaskini, ameshindwa kuondoa ujinga, ameshindwa kuondoa maradhi.
“Ndiyo maana tunasema tunahitaji kuunga mkono vuguvugu la mabadiliko ya kumwondoa mkoloni mweusi ambaye ni CCM.
“Hatuwaondoi CCM kwa sababu ya rangi, kabila, dini wala chochote kile cha namna hiyo. Ni kwa sababu miaka 52 baada ya uhuru tunaona kabisa wameshindwa kutuongoza, wamevuruga hata misingi iliyowekwa na waasisi wa taifa wakiongozwa na Mwalimu Nyerere. Wamevuruga hata tunu tulizojengewa kwa muda mrefu,” alisema Dk. Slaa.
Hali ya ulinzi
Wakati mikutano ya Dk. Slaa ikiendelea na kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na chama hicho, leo ataingia jimbo la Uvinza, hali ya ulinzi imeonekana kuimarishwa ambapo gazeti hili jana lilishuhudia idadi kubwa ya askari polisi takriban 50, katika eneo la Mnanila, wakisimamia ulinzi na usalama.
Gazeti hili limedokezwa kuwa hali hiyo inatokana na chama hicho kubaini na kutoa taarifa hadharani, huku pia kukiwa kuna mikakati inayopangwa.

No comments:

Post a Comment