Saturday, November 2, 2013

Waliolipua bomu CHADEMA wayeyuka

LICHA ya serikali kutamba kuwa itawakamata watuhumiwa wa shambulio la bomu katika mkutano wa CHADEMA eneo la Soweto jijini Arusha, sakata hilo limegeuka kuwa siri ya Jeshi la Polisi kutokana na hali ya sintofahamu inayoendelea kutawala.
Tukio hilo lilitokea Juni 15, mwaka huu, na sasa ni zaidi ya miezi minne tangu kuuawa kwa wafuasi watatu wa CHADEMA, huku wengine wengi wakiachwa majeruhi, lakini hadi leo hakuna taarifa kama kuna mtuhumiwa aliyekamatwa.
Awali, tukio hilo ambalo nusura limuue Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, aliyekuwa akihitimisha mkutano wa kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani, lilipotoshwa kisiasa ili kujenga taswira kwa umma kuwa chama hicho kililipanga chenyewe.
Tangu wakati huo, Jeshi la Polisi na viongozi wa serikali mkoani Arusha wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa, Magesa Mulongo, wamekuwa na kauli za kukinzana kuhusu wahusika wa tukio hilo.
Hivi karibuni, Mulongo alikaririwa akisema kuwa watuhumiwa wametiwa mbaroni na kwamba watatangazwa wakati wowote na vyombo vya dola, lakini Kamanda wa Polisi Mkoa, Liberatus Sabas, alipohojiwa alionekana kumshangaa kiongozi huyo.
Alipotafutwa juzi, msemaji wa jeshi hilo makao makuu, Advera Senso, naye alimtupia mzigo huo Kamanda wa Arusha akisema aulizwe yeye.
Tanzania Daima Jumamosi liliwasiliana na Sabas, lakini akasema atatoa taarifa hiyo muda ukifika bila kufafanua ni lini au kama watuhumiwa wamekamatwa.
Itakumbukwa kuwa siku moja baada ya mlipuko huo, serikali kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi wa Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, ilitoa taarifa bungeni ikilenga kulikingia kifua Jeshi la Polisi na kuibebesha lawama CHADEMA.
Katika tamko hilo, Lukuvi alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa mlipuko huo ulikuwa wa bomu la kurushwa kwa mkono, na kwamba aina ya urushaji wake haitofautiani na mbinu iliyotumika katika shambulio la Mei 5, mwaka huu, katika Kanisa la Olasiti jijini Arusha.
Alisema kuwa zimekuwepo jitihada za makusudi za baadhi ya vyama vya siasa, makundi ya kijamii na watu binafsi kupandikiza chuki kwa raia dhidi ya Jeshi la Polisi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, mlipuko huo ulikuwa wa bomu la kurushwa kwa mkono, na kwamba lilirushwa kutoka upande wa mashariki kuelekea magharibi kulikokuwa na gari aina ya Fuso lililokuwa linatumika kuhutubia.
Alidai kuwa polisi walimuona mlipuaji, lakini katika harakati za kumkamata, wafuasi wa CHADEMA waliwashambulia kwa mawe na hivyo mtuhumiwa akatokomea.
Kwa mbwembwe, Lukuvi alisema serikali itatoa zawadi ya sh milioni 100 kwa wale watakaowezesha kukamatwa kwa watuhumiwa wa milipuko hiyo.
Hata hivyo, taarifa ya Lukuvi iliota mbawa na kuzua mkanganyiko baada ya Mbowe kutangaza kuwa wanao mkanda wa video unaowaonyesha polisi kuwa wahusika wa shambulizi hilo.
Katika mkutano wake na waandishi, Mbowe alisema tukio hilo lilikuwa ni la kupangwa na waligundua risasi za bunduki aina ya SMG na bastola zilitumika mara baada ya mlipuko huo jambo lililozusha hofu.
Alilitaka Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi na kuwakamata watuhumiwa huku akiapa kwamba video hiyo hawataikabidhi kutokana na kutokuwa na imani na jeshi hilo, vinginevyo iundwe tume huru ya uchunguzi ya kimahakama.
Baada ya polisi kushindwa kuwakamata watuhumiwa ambao Waziri Lukuvi alilieleza Bunge kuwa waliwaona, lilimgeukia Mbowe na kuanza kumshinikiza asalimishe video hiyo, kwa vitisho kwamba atachukuliwa hatua asipotii amri.
Katika kutapatapa, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mulongo, alisema kuwa serikali imegundua mtandao wa milipuko ya mabomu yaliyotokea katika Kanisa la Olasiti na Uwanja wa Soweto kwenye mkutano wa CHADEMA.
Alitamba kuwa serikali itachukua hatua stahiki kwa wahusika hao bila kujali cheo, umaarufu au nafasi ya kisiasa.
Mulongo alithibitisha kuwa tayari kuna askari wa upelelezi wa FBI walishakuja Arusha wakishirikiana na wataalamu wa milipuko toka Kenya, jambo ambalo lilikanushwa na Ubalozi wa Marekani nchini.
Mbali ya Mbowe, viongozi wengine mbalimbali waandamizi wa chama hicho, akiwamo Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA) walinusurika katika mlipuko huo wa bomu.

No comments:

Post a Comment