Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi maarufu kama Mr. Sugu, anakusudia kuwasilisha kwa hati ya dharura muswada binafsi wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 wenye lengo la kurekebisha kifungu cha 25 cha sheria hiyo kinachotumiwa vibaya na mawaziri kufungia/kusitisha uchapishaji wa magazeti.
Alisema kwa kutumia kanuni ya 81 (5) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, anakusudia kuchukua dharura hiyo ili kutimiza masharti ya kanuni hiyo na kwamba kuanzia jana alitarajia kuanza kukusanya saini za wabunge wanaounga mkono hatua hiyo.
“Natarajia kufanya hivyo kwa kuzingatia kwamba muswada kwa utaratibu wa kawaida wa kuifuta sheria nzima utahitaji kuchapwa kwanza kwenye gazeti la Serikali na kwa vyovyote vile Serikali itatumia kisingizio cha kesi iliyofunguliwa na Hali Halisi Publishers (Mwanahalisi) ya mwaka 2009 ambayo imecheleweshwa kusikilizwa kwa miaka minne kuendelea kucheleweshwa kufuta sheria hiyo,” alisema Sugu.
“Ili kukwepa kikwazo hicho nitawasilisha muswada wa dharura wa kufanya marekebisho (siyo kufuta) yenye kumwondolea Waziri mwenye dhamana mamlaka ya kufungia/kusitisha kuchapisha gazeti lolote au magazeti yoyote,” aliongeza.
Alisema serikali haitaweza kutumia kisingizio cha kesi iliyo mahakamani kufanya marekebisho ya sheria hiyo kwa sababu pamoja na kesi kuwapo mahakamani yenyewe tayari imeshasomwa kwa mara ya kwanza Bungeni Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali namba 3 wa mwaka 2013 ambao katika vifungu vya 40 na 41 unakusudia kufanyia marekebisho vifungu vya 36(1) na 37 (1) (b) kwa ajili ya kuongeza faini kwa magazeti kutoka Sh. 150,000 mpaka milioni tano kwa makosa ya kashfa.
No comments:
Post a Comment