Wednesday, November 6, 2013

Selasini ahoji mikataba NHC

SERIKALI imehojiwa kama haioni utaratibu Bodi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuzuia uendelezaji wa miradi ya shirika hilo inayoingia mkataba na wawekezaji wa ndani kupitia PPP na kudai ni lazima ipitiwe upya ili kuruhusu NHC kupewa hisa za ziada kabla ya mradi kukamilika, kinyume cha mikataba ya awali ni kukatisha tamaa wawekezaji wa ndani na kuzuia jitihada za serikali kuhamasisha miradi ya PPP.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni mjini hapa na Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (CHADEMA), ambapo pia alitaka kujua kama serikali haioni kwamba shauri la mwekezaji kuingia gharama zote kama upembuzi yakinifu, usanifu wa majengo na gharama za ubomoaji wa majengo ya zamani likiende mahakamani linaweza kuigharimu serikali fedha nyingi za walipa kodi kama fidia kwa usumbufu waliousababishiwa wawekezaji.
Katika swali la nyongeza, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), alitaka kujua kama serikali iko tayari kutembelea eneo la Ubungo kutatua mgogoro uliopo baina ya wananchi wanaoishi katika nyumba za NHC na menejimenti ya shirika hilo.
Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodlucky Olemedeye, alisema wizara yake inakiri kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wanaopinga miradi ya ubia ilikuwa ikiendeshwa baina ya shirika hilo na wawekezaji wa  sekta binafsi.
Alisema msingi wa malalamiko hayo ni kiwango cha uwazi katika kuingia mikataba, usimamizi wa miradi na masilahi madogo kwa upande wa NHC.
“Kwa mfano, mikataba iliyo mingi ilikuwa inatoa asilimia 25 ya hisa zote za mradi kwa NHC na inayobaki inachukuliwa na wawekezaji,” alisema naibu waziri.
Alifafanua kuwa kufuatia malalamiko hayo mwaka 2009 serikali ilisimamisha zoezi la NHC kuingia mikataba mipya ya miradi ya ubia.
Menejimenti na bodi mpya ilipoanza kazi Machi 2010, serikali iliagiza kufanya tathmini ya utekelezaji wa mikataba ya miradi ya ubia kwa  lengo la kuiboresha na hususan kubainisha taratibu zilizofuatwa hadi kufikia mikataba ya miradi hiyo na kuyafanyia kazi malalamiko ya wananchi ipasavyo.
Akijibu swali la Mnyika, naibu waziri huyo alisema yuko tayari kufika katika eneo hilo la Ubungo akiwa na menejimenti yake ili waweze kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.

No comments:

Post a Comment