Thursday, November 7, 2013

Selasini ahimiza matumizi majiko bunifu

MBUNGE wa Rombo, Joseph Selasini, amehoji serikali ni kwa nini haichukui hatua za makusudi kusambaza majiko bunifu yanayotumia nishati ndogo ya kuni kwa lengo la kupunguza uharibifu wa mazingira.
Selasini alitoa kauli hiyo bungeni  jana alipokuwa akiuliza swali la nyongeza.
“Ni dhahiri tusipochukua hatua za haraka nchi yetu itageuka jangwa kutokana na ongezeko kubwa la uharibifu wa mazingira,” alisema.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Same Mashariki, Anne Malecela, alitaka kujua taifa linapata athari gani kwa kuzalisha mkaa  tani milioni moja.
Pia mbunge huyo alitaka kujua kama serikali haioni kuwa Mkoa wa Dar es Salaam hauna haja ya kutumia kiasi hicho cha mkaa kwa kuwa nyumba nyingi zina umeme kuliko mikoa mingine.
Katika swali jingine la nyongeza, Mbunge wa Kisarawe, Suleiman Jafo, alitaka kujua kama serikali haioni haja ya kurudisha suala la mistu kwenye halmashauri, ili iweze kusimamiwa kwa karibu.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Charles Kitwanga, alikiri majiko hayo kusaidia kupunguza matumizi ya kuni na kuongeza kuwa tayari kuna miradi inaendelea ili kuhakikisha majiko kama hayo yanatumika.
Alisema ipo sheria ya mazingira ambayo inazitaka ngazi ya kata, vijiji na halmashauri kusimamia na kuhakikisha wanatunza mazingira.
Akiendelea kujibu maswali hayo, alikiri taifa kupata athari kubwa katika kuzalisha mkaa kwa kiasi kikubwa kwa kuwa Tanzania inapoteza hekta za misitu zipatazo 400,000 kwa mwaka.
Aidha, alisema athari inayopatikana kwa kuzalisha mkaa mwingi ni kusababisha mmomonyoko wa udongo, kupungua kwa malisho, kupungua kwa mvua, na ongezeko la hewa ya ukaa, ambapo huchangia ongezeko la joto duniani na hatimaye mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa bioanuwai ambapo wanyama na baadhi ya mimea vinatoweka.
Pia alisema mtandao wa nishati nchini bado ni mdogo, kwani takriban asilimia 20 ya Watanzania wamefikiwa na huduma hiyo.

No comments:

Post a Comment