CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepata pigo baada ya Naibu Meya wa Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Vicent Remoy, kufariki ghafla jana.
Akithibitisha kutokea kwa kifo hicho, Meya wa Manispaa hiyo, Jafary Michael (CHADEMA), alisema Remoy ambaye pia alikuwa ni Diwani wa Kata ya Kiboriloni, zahanati ya Jafary iliyoko katikati ya mji wa Moshi.
“Ni kweli amefariki, na mimi nimepokea taarifa hiyo dakika 30 zilizopita, na kwa mujibu wa taarifa za awali, ni kwamba alienda kutizama afya yake hapo zahanati baada ya kuhisi kifua kuwa kizito wakati akiwa shambani kwake Msalanga,” alisema Michael.
Alisema mara ya mwisho kuzungumza naye kuhusu ugonjwa ilikuwa ni wakati wamesafiri kwenda nchini Ujerumani kwa ajili ya mazungumzo na serikali ya nchi hiyo ambako alimwambia kuwa amekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa miguu (gauti).
Mstahiki Meya Michael ambaye pia ni mwenyekiti wa CHADEMA Manispaa ya Moshi, alisema chama kimepokea kifo hicho kwa mshituko mkubwa kutokana na ukweli kwamba Remoy ndiye alikuwa muasisi wa chama katika Manispaa ya Moshi.
“CHADEMA manispaa tumepokea kwa mshituko mkubwa kifo cha huyu mzee. Mbali ya kuwa muasisi wa chama, pia alikuwa kiungo muhimu kama mtu mzima kwa wanasiasa ambao ni vijana bila ya kujali itikadi za kisiasa,” alisema Michael.
Alisema pia marehemu alikuwa Diwani wa Kata ya Kiboriloni kwa vipindi vitatu mfululizo kuanzia mwaka 2000 hadi sasa, huku akiwa mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya CHADEMA katika Manispaa ya Moshi.
“Naweza sema alikuwa ni kiongozi mwandamizi ndani ya CHADEMA, na pia ameshikilia nafasi ya naibu meya kwa vipindi vyote vitatu. Mara ya mwisho alichaguliwa kwa kura zote ambazo zilipigwa na madiwani wa CHADEMA na CCM,” alisema Michael.
Alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya KCMC na kwamba hadi sasa chanzo cha kifo chake hakijafahamika.
R.I.P Mh naibu meya
ReplyDelete