TANGA WAKANA UASI
Kwa upande wake, Chadema Mkoa wa Tanga kimekemea viongozi waliyoibuka kupinga maamuzi ya Kamati kuu ya kuwavua nyadhifa Zitto na wenzake na kwamba kitendo hicho ni kinyume cha Katiba ya chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Chadema Mkoa wa Tanga, Jonathan Bahweje, alikemea viongozi hao kuwa wanakiuka katiba kifungu cha saba ibara ya saba na 16 (V) inayoipa mamlaka na uwezo Kamati Kuu ya kuteua na kumuondoa mtu yeyote atakaebainika kwenda kinyume cha katiba.
Bahweje alieleza kuwa viongozi hao wanatenda kosa la kikatiba na kwamba hawana haki ya kuhoji wala kukosoa kilichotendeka kwa kuwa wao ni ngazi za chini, hivyo hawawezi kutengua maamuzi ya chombo kilichopo juu yao.
CHASO YAONYA
Shirikisho la Wanachama wa Chadema Vyuo Vikuu (Chaso) Mkoa wa Dar es Salaam, limesema watu wanaojitokeza hivi sasa na kutoa matamko yanayopinga uamuzi wa kumvua Zitto na wenzake nafasi za uongozi wanatumiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mratibu Mkuu wa Chaso, Elihuruma Jackson Himida, alisema hayo jana alipozungumza na NIPASHE na kusema katika kutekeleza mbinu zao alizoziita ‘chafu’, watu hao wamekuwa wakijitambulisha kuwa ni wanachama wa Chadema wakati siyo kweli.
Alisema Chaso itatoa majibu leo kuhusiana na matamko yanayoendelea kutolewa na watu hao ili Watanzania wajue ukweli halisi wa kile kinachoendelea juu yao.
Alisema uamuzi huo umefikiwa katika kikao cha Sekretarieti ya Chaso, kilichofanyika jana kujadili watu hao, ambao alisema hawamo hata kwenye kumbukumbu za Chadema kuwa ni wanachama wake, lakini wanashangazwa kuona waandishi wa habari wakiwashabikia.
Kauli hiyo ya Elihuruma imetolewa siku moja baada ya juzi watu waliojitambulisha kuwa ni wanachama wa Chadema, wakiwamo wanafunzi wa vyuo vikuu kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kutangaza kile walichokiita mgogoro wa kiutawala kati ya wapigania demokrasia na wahafidhina ndani ya chama hicho.
IRINGA WANENA
Katika hatua nyingine, Chadema katika mikoa ya Iringa na Tanga kimeunga mkono hatua ya Kamati Kuu kuwavua nafasi za uongozi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu, Zitto na wenzake.
Zitto alivuliwa uongozi Ijumaa iliyopita sambamba na aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu, Dk. Kitila Mkumbo na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba, kwa tuhuma za kukisaliti chama.
Wote wanatuhumiwa kuandaa waraka ambao ulikuwa na tuhuma dhidi ya chama na viongozi wake ngazi ya taifa.
Chadema mkoa wa Iringa kimesema hatua zilizochukuliwa na Kamati Kuu dhidi ya viongozi hao ni sahihi.
Mjumbe wa Kamati ya Uendaji wa Chadema Nyanda za Juu Kusini, Abdu Changawe, aliwaambia waandishi wa habari mjini Iringa jana kuwa chama hicho kinaongozwa na katiba na kama mtu yeyote atakayehusika kutoiheshimu katiba hiyo, lazima katiba itamshughulikia kikamilifu.
“Kutokana na tabia zao za usaliti ndani ya chama sisi kama wanachama wa Chadema Iringa tunapongeza maamuzi yote na pia tunatoa msimamo wetu kuwa yeyote aliye na tabia kama hiyo ajirekebishe haraka kabla sheria haijachukua mkondo wake,”alisema Changawe.
Aidha, alisema kuwa chama hicho kimejipanga kuhakikisha kuwa haki inatendeka sehemu zote na pia wamejipanga kuwa tayari kutokumbatia uovu wa aina yoyote kwani mafanikio ya chama mpaka sasa yamegarimu damu za watu, mali za watu na hata wengine kufungwa magerezani.
No comments:
Post a Comment