Suala la kutimuliwa kwenye madaraka ya uongozi aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Zitto Kabwe, na Mwanazuoni kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitila Mkumbo, sasa limechukua sura mpya.
Shirikisho la wanachama wanafunzi wa Chadema kutoka vyuo vya Elimu ya Juu, mkoa wa Dar es Salaam (Chaso), jana limeibuka na kuunga mkono uamuzi wa Kamati Kuu Chadema kuwavua uongozi waliodaiwa kufanya uasi ndani ya chama
Shirikisho hilo pia limewarushia shutuma Mtela Mwampamba, Habib Mchange, Juliana Shonza na Greyson Nyakarungu, waliofukuzwa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), kutengeneza makundi ya kupinga uamuzi uliofikiwa na Kamati Kuu hiyo.
Akisoma tamko lao kwa niaba ya viongozi wenzake, Mratibu Mkuu wa shirikisho hilo, Himida Jackson, alisema mapema wiki hii kikundi cha vijana wanaojiita viongozi wa Chaso, waliibuka na kutoa taarifa ya kupinga maamuzi yaliyofikiwa na Kamati Kuu Chadema.
Tamko hilo ambalo limesainiwa na mratibu huyo pamoja na Afisa Habari wa shirikisho hilo, Amandus Gomba, limetokana na kikao kilichofanyika juzi Chadema na kufikia uamuzi wa kuliandaa kwa ajili ya umma wa Watanzania.
Alisema taarifa zilizoripotiwa kwenye vyombo vya habari wiki hii kuwa Chaso limepinga uamuzi wa kamati kuu siyo za kweli na kwamba waliozitoa hawatambuliki kwenye kumbukumbu za wanachama wao.
Alifafanua kuwa mapema mwaka huu Bavicha liliwafukuza baadhi ya vijana kwa usaliti wao ambapo waliotajwa hapo juu walikimbilia chama tawala.
“Kikundi hicho (waliofukuzwa) kimekuwa kikipita huko mtaani na kukusanya vijana wa CCM wanaojipachika uanachama wa Chadema na kujipatia vyeo vya Chaso kisha kutoa matamko ya kupinga maamuzi ya chama,” alisema.
Alisema baadhi yao wamekuwa wakijitambulisha ni viongozi wa Chadema Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wakati siyo kweli, huku akitaja majina ya viongozi wanaotambulika kuwa ni Marco Julius ambaye ni mwenyekiti na Daniel Mswelo, katibu.
Aliongeza kuwa, Januari 19, mwaka huu, uongozi wa Chaso Chuo Kikuu cha Ardhi ulisimamishwa kutokana na utendaji mbovu.
Alisema kwa misingi hiyo, vijana hao hawana uhalali wa kufanya shughuli zozote kwa ngazi ya uongozi au chama.
Alisema Jumapili iliyopita vijana hao walifanya jitihada za kushawishi wanafunzi wa vyuo vikuu kuungana nao katika kupinga maamuzi yaliyotolewa na kamati kuu ingawa hawakufanikiwa katika hilo.
Alisema tamko la Jumatano ya wiki hii walilolitoa watu hao ni mwendelezo wa jitihada hizo walizozikusudia. Kutokana na hilo, amewataka wanachama watambue kuwa, tamko hilo siyo halali huku akisisitiza kuwa msimamo wao unaunga mkono maamuzi yaliyochukuliwa na Kamati Kuu hasa kwa kuhakikisha hakuna mtu yeyote aliye juu ya chama.
“Tunasisitiza chama kisiruhusu mmoja wetu abomoe nyumba hii hata kama alishiriki kuijenga au hatuwezi kuruhusu mtu atoboe mtumbwi tunaosafiria,” alisema.
Akizungumzia kuhusu chama, Jackson alisema ni chenye watu wenye nia ya dhati ya kulikomboa taifa na watu wake ambao wanakabiliwa na matatizo ya kiuchumi, kijamii na kisiasa.
“Tunaamini Chadema ndicho chama pekee ambacho ni mbadala Tanzania kilichobeba matumaini ya Watanzania kwa kuwa kinapigania haki za kila mnyonge,” alisema.
Aliwataka wanachama na viongozi kuwa makini na kutosita kuchukua maamuzi dhidi ya mtu yeyote hasa katika kipindi hiki ambacho wamesikia kauli za viongozi wa CCM wanaojiapiza kuwa Chadema haitafika uchaguzi mkuu.
Mwenyekiti wa Chadema UDSM, Julius Michael, alisema kuwa yanayoendelea hivi sasa ni propaganda ya CCM kutaka kukihujumu Chadema na kuonyesha yaliyoamuliwa na kamati kuu ni uonevu kwa sababu chama tawala hakijawahi kuchukua maamuzi magumu kama hayo.
Alisema baadhi ya vyombo vya habari (bila kuvitaja), vimenunuliwa na vimekuwa vikiripoti uamuzi huo wa kamati kuu tofauti.
Mjumbe wa Chaso, Gwamaka Mbughi alisema baadhi ya magazeti yaliandika bila uhalisia hivyo kupotosha umma.
Alisema kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama chao, Chaso hakina mamlaka ya kupinga maamuzi yaliyofikiwa. Mwenyekiti wa Chaso kutoka Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Musa Ndile, alisema maamuzi ya kamati ni halali hivyo inapotokea mtu ameenda kinyume bila kujali anakubalika kwa kiasi gani, hatua zitachukuliwa kwa mujibu wa katiba yao.
No comments:
Post a Comment